• Nairobi
  • Last Updated October 2nd, 2023 8:00 AM
Matimbo hatari ya Kimolwet yanameza watu hasa walevi

Matimbo hatari ya Kimolwet yanameza watu hasa walevi

NA RICHARD MAOSI 

WAKAZI wa kijiji cha Kimolwet eneo la Barut, Kaunti ya Nakuru, wanalalamikia mazingira yao ‘kuvamiwa’ na wachimbaji migodi.  

Tayari, shughuli hiyo imekaribia maboma yao suala linalozua hofu kuhusu usalama wa makazi.

Aidha imekuwa vigumu kuwekeza katika sehemu hii kwa sababu ya upatikanaji wa matimbo ambayo sio salama kwa wapita njia hasa watoto.

Kulingana na Jane Jebet mkaazi wa Barut anasema amekuwa akiishi katika sehemu hiyo kwa zaidi ya miaka 10, lakini sasa amelazimika kuhamia kwingine baada ya eneo lenyewe kugeuzwa ngome ya kuvuna mchanga.

Akizungumza na Taifa Leo Dijitali, alisema sehemu ya nyumba yake ilikuwa imechimbika na ilikuwa karibu kumezwa na timbo ila rafiki yake mmoja alimshauri ahamie kwingine.

“Wachimba migodi wamekuwa wakilipua mawe kwa kutumia vilipuzi na kusababisha nyumba zetu kuwa hafifu, na hata wakati mwingine huyumbayumba,”akasema.

Jebet anasema tayari mita 10 ya shamba lake imechukuliwa na shughuli yenyewe na anahofia shamba lake lote litapotea,

“Kabla ya shughuli za uchimbaji migodi kuanzishwa nilikuwa nikimiliki kipande kikubwa cha ardhi lakini sasa mambo yamebadilika kwa sababu sina uhuru kuendesha shughuli zangu kama zamani,” asimulia.

Sehemu ya shamba lake tayari imebakia kuwa chini ya udhibiti wa wachimbaji migodi ambao hawajali, hii ikiashiria kuwa kijiji cha Kimolwet kipo katika hatari ya kuzama na kupotea kabisa.

“Kwa muda mrefu niliokaa hapa nimekuwa nikishuhudia watu wengi wakipoteza maisha yao na wengi wao wakiwa ni walevi,” akasema.

Anasema wamekuwa wakiwasilisha malalamishi yao kwa idara husika, mojawapo ikiwa ni NEMA na utawala wa mtaa huku wakijaribu kushirikisha kila kitengo bila mafanikio.

“Tumekuwa tukipeleka malalamishi yetu katika afisi za kaunti ya Nakuru lakini badala yake huwa hatusaidiki, ” Jebet alisikitika.

Mkazi mwingine aliyezungumza na Taifa Leo Dijitali alionyesha nyumba yake ikining’inia katika sehemu ya timbo hilo.

“Wakati mmoja kanisa linalopatikana karibu na eneo la timbo hilo lililalamikia NEMA, lakini uchimbaji ulisitishwa kwa muda. Isitoshe, mgombea wa kiti cha ubunge aliwahi kuhimiza vijana waendelee kuchimba mchanga na tunashindwa jukumu la NEMA ni gani,” alishangaa.

Kipyegon Kiplangat mkazi wa karibu anasema maisha ya watoto wadogo yako hatarini.

“Ninawaonea watoto wa shule huruma wanaopita karibu na timbo asubuhi na mapema wakielekea shuleni, wengi wao hawana ujuzi wa kupenya kwenye matimbo yenyewe” alisema.

Kwa mujibu wa sheria za NEMA 2007, wakazi wanashauriwa kutumia mazingira yao ipasavyo bila kuyaharibu kwani maisha ya baadaye yanayategemea.

“Maelekezo hayo yanazingatia utumiaji wa raslimali za kijamii kwa kuzingatia maisha ya raia wake,” sehemu ya nakala hiyo ilinukuu.

  • Tags

You can share this post!

Azimio yakashifu serikali ikiihusisha na utekaji nyara wa...

Mapenzi ya mzazi: Baba akubali kupoteza maisha mwanawe...

T L