• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 10:21 AM
MCA asikitishwa na wakulima kuendelea kuasi kahawa

MCA asikitishwa na wakulima kuendelea kuasi kahawa

Na SAMMY WAWERU

DIWANI wa wadi ya Murera, Ruiru, John Wokabi ameelezea kusikitishwa kwake na kuendelea kudorora kwa kilimo cha kahawa Kenya.

Kutokana na kugeuzwa kwa mashamba yaliyokuwa yakikuzwa zao hilo kuwa uga wa miradi mingine ya maendeleo, Bw Wokabi ameonya hatua hiyo ni hatari kwa kiungo hicho cha kinywaji.

Takwimu zinaonyesha uzalishaji wa kahawa nchini umeshuka kwa kiwango kikubwa. Kulingana na takwimu za New KPCU, taasisi ya serikali inayojukumika kusaga na kutafutia zao hilo soko ndani na nje ya nchi, mazao yameshuka kutoka tani 140, 000 (uzani wa metric tons) miaka 20 – 30 iliyopita, hadi 36, 000 kwa mwaka.

Upungufu huo mkubwa unatokana na uongozi mbaya hapo awali chini ya Old KPCU, kabla Rais Uhuru Kenyatta kufanya mabadiliko katika shirika hilo la kahawa. Aidha, changamoto zinazozingira sekta hiyo zilichangia pakubwa wakulima kung’oa mikahawa ili kuwekeza kwa miradi mingine.

Mojawapo ni ujenzi wa nyumba za kupangisha na kukodi, na vilevile kukuza mimea mingine yenye thamani na mapato ya haraka. “Kitambo, Murera ilijaa kahawa na kwa sasa inaendelea kuisha,” Bw Wokabi akasema, akielezea kusikitishwa na hatua ya wakulima kung’oa zao hilo.

Bw John Wokabi, MCA Murera, Ruiru, Kaunti ya Kiambu asikitikishwa na kuendelea kung’olewa kwa mikahawa nchini…Picha/ SAMMY WAWERU

“Kahawa ndiyo imesomesha baadhi yetu, ila zao hili limedhulumiwa,” akaongeza MCA huyo. Kaunti ya Kiambu ni miongoni mwa maeneo yanayokuza kahawa nchini, na wakulima wamekuwa wakilalamikia kuumia, kupunjwa na mabroka kilele kikiwa zao hilo kuwa na soko mbovu.

Waziri wa Kilimo, Bw Peter Munya amekuwa akiendeleza mageuzi, Rais Kenyatta majuzi katika kongamano na wajumbe wa Jubilee Sagana State Lodge akimsifia kwa “kuleta afueni na tabasamu kwa wakulima wa kahawa”.

Kiongozi wa nchi, alisema Waziri Munya amesaidia kuboresha sekta ya kahawa akitaja malipo wanayopokea wakulima kwa sasa kama baadhi ya maendeleo aliyoleta. Licha ya kauli ya Rais, MCA wa Murera anasema ingekuwa busara serikali kukaza kamba jitihada zake akisema wakulima wanaendelea kuhangaika.

Mwanasiasa huyo aidha alisema malipo ya kahawa na yale ya ziada – bonasi, hukawia kufikia wakulima. “Serikali ishike mkono wakulima wadogo, ikifanya hivyo tutaendelea kuzalisha kahawa,” Bw Wokabi akasema.

Chini ya Katiba ya sasa, iliyozinduliwa 2010, sekta ya kilimo na ufugaji imegatuliwa. “Serikali za kaunti ziangalie mambo ya kahawa,” diwani huyo akahimiza.

Licha ya sekta ya kilimo na ufugaji kuwa chini ya serikali za ugatuzi, kaunti zinalaumiwa kwa kuipuuza na kukosa kuitengea mgao wa kutosha wakati wa makadirio ya bajeti kila mwaka.

You can share this post!

Maonyesho ya kahawa yaliyoleta pamoja zaidi ya wakulima...

PCPB yaendelea kunyoosha mjeledi kwa wahuni wa dawa bandia...

T L