• Nairobi
  • Last Updated February 26th, 2024 8:50 AM
Muuzaji wa kuku anayefukuzana na ndoto kuwa wakili

Muuzaji wa kuku anayefukuzana na ndoto kuwa wakili

NA VITALIS KIMUTAI

VIJANA wenzake walipokuwa wakijihusisha na kazi na maisha ya familia, Kibet Maritim Agustine kutoka kijiji cha Masare Kaunti ya Bomet alichagua njia tofauti—kuandika upya hadithi yake ya elimu.

Akiwa na umri wa miaka 33 na baba wa mtoto mmoja, Maritim alifanya uamuzi wa kijasiri wa kurudi tena shuleni.

Mhitimu wa Kidato cha Nne ambaye alifanya mtihani wa KCSE miaka 13 iliyopita, alirejea kuendelea na elimu yake ya msingi mapema mwaka huu, 2023, baada ya kutoridhishwa na alama ya D+ aliyopata katika matokeo ya KCSE.

Katika azma ya kutimiza ndoto yake ya kuwa wakili, alijiunga tena na shule ya msingi na kufanya mtihani wa Darasa la Nane (KCPE) 2023 na kupata alama 350.

Azma ya Maritim katika elimu ilianza 2005 alipokamilisha mtihani wake wa KCPE katika Shule ya Msingi ya Merigi eneobunge la Bomet Mashariki, na kuzoa alama 278.

Hata hivyo, ukosefu wa fedha ulimlazimu kuacha shule ya Sekondari ya Olbutyo akiwa katika kidato cha pili.

Bila kukata tamaa, alijiunga na Shule ya Upili ya Kyogong, na hatimaye kupata D+ katika mtihani wa KCSE mnamo 2009.

“Nilikuwa nikisoma binafsi nyumbani kwa zaidi ya mwaka mmoja nilipotafuta nafasi katika shule ya upili ya Kyogong kama mwanafunzi wa kidato cha tatu katika muhula wa pili. Nilifanya mtihani wa kuingia na kufaulu. Niliweka bidii zaidi kama mwanafunzi. Lakini ningeweza tu kupata alama D+ katika mitihani ya KCSE,” Bw Maritim aliambia Taifa Leo Dijitali.

Hakuridhishwa na matokeo na ndoto yake ikawa imeahirishwa kwa muda.

Maritim aligeukia biashara ya kuuza kuku na mayai kando ya barabara huko Bomet.

Anauza wastani wa kuku watano kwa siku, lakini wakati mwingine, anaenda nyumbani mikono mitupu bila kuuza chochote.

Kwa miaka 13, alipitia changamoto za biashara hii ya kubahatisha.

Lakini licha ya magumu hayo, hamu kubwa ya kufufua matamanio yake ya elimu iliendelea na sasa kuna matumaini ya kuyafanikisha.

 

  • Tags

You can share this post!

Niliteswa kama mbwa: Mwanamke asimulia ukatili wa kutisha...

Seneta akemewa kwa kutishia kufunga baa zinazouza pombe...

T L