NA CHARLES WASONGA
KATIBU Mkuu wa muungano wa wafanyakazi nchini (COTU) Francis Atwoli sasa amemgeuka Rais mstaafu Uhuru Kenyatta akimlaumu kwa kuchangia kushindwa kwa kiongozi wa Azimio Rais Odinga katika uchaguzi wa urais mwaka 2022.
Bw Atwoli, ambaye mwishoni mwa mwaka 2022, alitangaza kuwa atafanya kazi na Rais William Ruto, anadai japo Bw Kenyatta alionekana kumuunga mkono Odinga, alichelea kumfanyia kampeni katika ngome yake ya Mlima Kenya hali iliyochangia kushindwa kwake na Dkt Ruto.
“Kabla ya uchaguzi, nilimuuliza mtoto wa shangazi yangu (Raila) kuhusu iwapo kweli Bw Kenyatta anatuunga mkono kwa dhati. Nilimuuliza ni kwamba hajawahi kuitisha mkutano wa kumfanyia kampeni hata kule kwao Gatundu. Lakini kwa kuwa Uhuru alikuwa mkubwa wake niliamua kutomsukuma sana,” Bw Atwoli akasema Jumatano kwenye hafla ya mazishi eneo la Khwisero, kaunti ya Kakamega.
Kulingana na kinara huyo wa Cotu, Bw Kenyatta hakumfaidi Bw Odinga jinsi ilivyotarajiwa kwa sababu umaarufu wake katika ngome yake ya Mlima Kenya ulikuwa umedidimia zaidi kutokana na uhasama kati yake na Dkt Ruto.
Alielezea jinsi yeye na Gavana wa zamani wa Kakamega Wycliffe Ambetsa Oparanya walivyofanikisha kampeni za Azimio katika kaunti ya Kakamega na kuchangia muungano huo kushinda viti vingi.
“Mimi na Oparanya tulifanya kazi kubwa hapa nyumbani na kuwezesha mrengo wetu kushinda viti 12 vya ubunge, isipokuwa viti vya Malava na Shinyalu ambako tulidhamini wagombeaji wenye ushawishi finyu. Tulishinda viti vya ugavana na hata mwakilishi wa kike,” akaeleza.
Wadadisi wa masuala ya kisiasa wanasema kuwa Bw Atwoli anatoa kauli ili kuonyesha Rais Ruto faida ya kisiasa ambayo atapata kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027 akishirikiana naye (Atwoli).
“Kwa sababu mwishoni mwa mwaka 2022, Rais Ruto alikubali kushirikiana na Atwoli, pamoja na wanasiasa wengine wa magharibi mwa Kenya, sasa Bw Atwoli anamthibitishia Ruto umuhimu wa ushirikiano huo,” anasema Suba Churchill.
“Isitoshe, Atwoli ni mwanasiasa mjanja zaidi kwani anafahamu fika kwamba ni kwa kuunga mkono serikali iliyoko mamlakani ambapo atalinda masilahi yake haswa katika COTU. Kwa hivyo, kwa kumlaumu Uhuru na kuvumisha uwezo wake kisiasa katika kaunti ya Kakamega anamwonyesha Rais Ruto anaweza kumsaidia kupata kura zote ambazo Odinga alipata kutoka eneo hilo,” anaongeza Bw Suba, ambaye ni mshirikishi wa kitaifa ya muungano wa mashirika ya kijamii nchini.
Kulingana na matokeo ya uchaguzi urais wa Agosti 9, 2022 Bw Odinga alizoa jumla ya kura 369,827 kutoka kaunti ya Kakamega. Naye Dkt Ruto alipata kura 131,567 katika kinyang’anyiro hicho.
Mbw Atwoli na Oparanya ndio waliongoza kampeni za muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya katika eneo hilo.
Lakini baada ya Dkt Ruto kutangazwa mshindi katika kinyang’anyiro hicho, Bw Atwoli alibadili msimamo wake kisiasa na kuamua kufanya kazi na kinara huyo wa muungamo wa Kenya Kwanza.
Aidha, Bw Atwoli alipiga abautani nyingine kisiasa na kumtangaza tena Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi kama kinara wa eneo la Magharibi mwa Kenya.
Itakumbukwa kuwa mapema mwaka 2022, Bw Atwoli alimvua Bw Mudavadi wadhifa huo aliompa Desemba 31, 2016 katika hafla iliyoandaliwa katika uwanja wa michezo wa Bukhungu mjini Kakamega.
Subscribe our newsletter to stay updated