• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 11:55 AM
MIKIMBIO YA SIASA: Faida na zigo la KK kama wengi bungeni

MIKIMBIO YA SIASA: Faida na zigo la KK kama wengi bungeni

NA CHARLES WASONGA

KUTAWAZWA kwa mrengo wa Kenya Kwanza (KKA) kuwa mrengo wa walio wengi katika bunge la kitaifa sasa kutamwezesha Rais William Ruto kupitisha ajenda zake kwa urahisi katika bunge hilo.

Katika uamuzi aliotoa Alhamisi, Spika Moses Wetang’ula alibainisha kuwa KKA una wabunge 179 huku Azimio la Umoja-One Kenya ikiwa na wabunge 157.

Bw Wetang’ula alisema alifikia uamuzi huo baada ya kupokea barua kutoka kwa jumla ya wabunge 14 wa vyama vinne vilivyoko ndani ya Azimio, wakidai kugura muungano huo na kujiunga na KKA.

Vyama hivyo ni; United Democratic Movement (UDM), Maendeleo Chap Chap (MCC), Pamoja African Alliance (PAA) na Movement for Development and Growth (MDG) viliwasilisha kesi kortini vikitaka viondolewe kwenye orodha ya vyama tanzu katika Azimio.

Lakini wadadisi wanaonya kuwa japo hilo limempa kiongozi wa taifa nafasi nzuri ya kutekeleza ahadi zilizoko kwenye manifesto yake, huenda akatumia nafasi hiyo kupitisha miswada na maamuzi yanayoumiza raia.

Kulingana na Bobby Mkangi tija ya kwanza ambayo Rais Ruto amepata kufuatia uamuzi huo wa Spika Moses Wetang’ula ni kwamba wandani wake ndio watadhibiti kamati muhimu za bunge.

“Uamuzi huo sasa unaupa mrengo wa Kenya Kwanza nafasi ya kupata uwakilishi mkubwa katika kamati yenye ushawishi mkubwa kama ile ya kuratibu shughuli za bunge (HBC) na ile Kamati ya Uteuzi. Hii ina maana kuwa matakwa ya Rais Ruto yatapitishwa pasina upinzani mkali,” anasema Mkangi.

Kutawazwa kwa KKA kama mrengo wa walio wengi sasa kunamaana kwamba itawakilishwa na wabunge wengi katika kamati hiyo ambayo huamua ajenda za bunge.

Kwa upande mwingine, muungano huo unaoongwa na Rais Ruto pia utawakilishwa na wabunge wengi katika kamati ya uteuzi itakayowapiga msasa watu 22 waliopendekezwa kushikilia nyadhifa za uwaziri.

Hii ina maana kuwa japo wabunge wa Azimio walikuwa wametishia kuwaangusha baadhi ya wateule wenye dosari za kimaadili, huwatafaulu.

Sababu ni kwamba maamuzi katika kamati hufanywa kwa njia ya upigaji kura, mrengo wa walio wengi ndio hushinda.

Mbunge wa Ugunja Opiyo Wandayi, ambaye sasa ndiye kiongozi wa wachache, juzi alitisha kuwa Azimio itawakataa aliyekuwa

Mbunge wa Malindi Aisha Jumwa na aliyekuwa Seneta wa Meru Mithika Linturi, walipendekezwa kuwa mawaziri wa Utumishi wa Umma na Kilimo, mtawalia.

Bi Jumwa anakabiliwa na kesi za mauaji na ufisadi ambazo zingali zikishughuliwa mahakamani. Naye Bw Linturi anakabiliwa na kesi ya kupata mkopo kuwa kuwasilisha stakabadhi ghushi kwa shirika moja la kifedha.

Lakini wabunge wa Kenya Kwanza wamewatetea wawili hao wakishikilia kuwa hawafai kuzuiwa kushikilia nyadhifa za uwaziri kwa sababu hawajapatikana na hatia kuhusiana na makosa yanayodaiwa kutenda.

Kwa upande mwingi, Bw Mkangi anasema kutawazwa kwa Kenya Kwanza kama mrengo wa walio wengi kumeuwekea mzigo mzito wa kutekelezwa ahadi zote ambazo Rais Ruto alitoa kwa Wakenya.

“Bungeni ndiko sheria, sera na maongozi yote ya serikali hupitishwa. Muhimu zaidi ni kwamba bunge la kitaifa ina mchango mkubwa zaidi katika utayarishaji wa bajeti na ugavi wa fedha baina ya serikali kuu na serikali za kaunti. Kwa hivyo, mrengo huo hautakuwa na sababu ya kutotekeleza ahadi zote ifikapo mwaka wa 2027 kwani umedhibiti bunge,” anaeleza.

Aidha, KKA itapata nafasi ya kuongoza kamati zote za bunge zitakazoshughulikia ajenda za serikali. Hii ina maana kuwa wabunge wa mrengo huo watakuwa na kibarua kizito cha kuhakikisha kuwa serikali ya Dkt Ruto anawatumikia Wakenya kulingana na matarajio yao.

  • Tags

You can share this post!

JUNGU KUU: Ruto atakavyopanga ‘wazee’ Uhuru, Raila

KIGODA CHA PWANI: Maendeleo Pwani yanahitaji umoja wa...

T L