• Nairobi
  • Last Updated March 5th, 2024 12:43 PM
MIKIMBIO YA SIASA: Gumzo mtaani MaDVD kupewa afisi kichochoroni

MIKIMBIO YA SIASA: Gumzo mtaani MaDVD kupewa afisi kichochoroni

NA CHARLES WASONGA

UTATA umegubika uhalali wa cheo cha Kinara wa Mawaziri ambacho Rais William Ruto alimtunuku kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi huku wabunge kesho Jumatatu wakianza kuwapiga msasa watu 22 waliopendekezwa kushikilia nyadhifa za uwaziri katika serikali ya Kenya Kwanza.

Haya yanajiri huku wandani wa Bw Mudavadi wakilalamikia agizo la Dkt Ruto kwamba afisi yake itakuwa katika makao makuu ya Shirika la Reli Nchini (KRC).

Wanadai kuwa hatua hiyo inaashiria kuwa cheo hicho ni cha hadhi ya chini ilhali Rais Ruto mwenyewe alitangaza kuwa Bw Mudavadi ndiye atakuwa wa tatu kwa ubabe katika serikali yake baada ya Naibu Rais Rigathi Gachagua.

“Bw Mudavadi ni kiongozi wa hadhi ya juu nchini na hafai kudunishwa kwa kupewa afisi katika makao makuu ya shirika la reli mahala ambapo hali usafi na usalama ni ya kutiliwa shaka. Huyu ni kiongozi ambaye amewahi kutumikia taifa hili katika nyadhifa za makamu wa rais, naibu waziri mkuu kando na kuhudumu katika wizara za Fedha, Serikali za Wilaya na Uchukuzi kama waziri. Apewe afisi katika majengo ya serikali yaliyoko barabara ya Harambee Avenue,” Mbunge mmoja wa ANC, ambaye aliomba tulibane jina lake, ameaimbia safu hii.

Awali, duru zilisema kuwa Bw Mudavadi angerithi afisi za Naibu Rais katika jumba la kifahari la Harambee Annex huku Bw Gachagua akihamishwa hadi jumla ya Harambee House, ambako kuna Afisa za Rais.Makao makuu ya shirika la KRC yako kando ya barabara ya Haile Salassie ambayo hushuhudia kelele nyingi kutoka kwa mamia ya magari ya uchukuzi wa umma na treni za abiria ambazo hubeba na kushukisha wasafiri katika Kituo Kikuu cha Gari Moshi jijini Nairobi.

Lakini kile kinachoonekana kuwa pigo kubwa kwa Bw Mudavadi ni hatua ya wabunge wa muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya kudai kuwa cheo hicho ni haramu kwani hakitambuliwi katika katiba ya sasa.

Wakiongozwa na kiongozi wa wachache Opiyo Wandayi wabunge hao wanamtaka Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula kutoa mwelekeo kuhusu suala hilo wakiapa kutoshiriki shughuli ya kumpiga msasa Bw Mudavadi.

“Hatuwezi kuhalalisha ukiukaji wa katiba kwa kuketi katika Kamati ya Uteuzi kumpiga msasa Bw Mudavadi. Nilimfahamisha Spika kwamba cheo hiki hakitambuliwi katika Katiba. Wanaweza kukipa jina jingine kwani hili la Mkuu wa Mawaziri halitambuliwi na Katiba. Rais anaweza kumteua waziri asiyesimamia asasi zozote badala ya kubuni cheo batili,” Bw Wandayi, ambaye ni Mbunge wa Ugunja akaeleza.

Kulingana na ratiba iliyotolewa na Bunge la Kitaifa Alhamisi, Bw Mudavadi ndiye ameratibiwa wa kwanza kuhojiwa mbele ya kamati hiyo ya wabunge 28, chini ya uenyekiti wa Spika Wetang’ula katika majengo ya bunge, Nairobi.

Spika Wetang’ula ameahidi kutoa uamuzi kuhusu suala hilo lililoibuliwa na Bw Wandayi, kabla ya shughuli ya mahojiano kuanza.

Lakini itakumbukwa kwamba, kulingana na mkataba uliobuni muungano wa Kenya Kwanza, Rais Ruto, Bw Wetang’ula na Mudavadi waliahidi kwamba wakishinda urais wataifanyia marekebisho katiba ili kubuni wadhifa wa Mkuu wa Mawaziri.

“Mswada utapelekwa bungeni kwa ajili ya kuifanyia marekebisho sheria ya Ushirikishi wa Majukumu ya Serikali ya Kitaifa ya 2013 ili kujumuisha Afisi ya Mkuu wa Mawaziri. Hatua hii italainisha majukumu ya afisi hiyo na sheria hiyo,” ikasema sehemu ya mkataba huo ambao ulitiwa saini na watatu hao.

Hata hivyo, kufikia sasa, mrengo wa Kenya Kwanza haujaonyesha nia ya kuwasilisha mswada wa marekebisho ya sheria hiyo bungeni.

  • Tags

You can share this post!

Griezmann afikisha mabao 100 akivalia jezi za Atletico...

Teuzi: Mwanachama wa PAA ashtaki IEBC

T L