• Nairobi
  • Last Updated April 15th, 2024 2:58 PM
MIKIMBIO YA SIASA: Kamket aliichakaza Kanu bondeni kwa kuunga Ruto

MIKIMBIO YA SIASA: Kamket aliichakaza Kanu bondeni kwa kuunga Ruto

NA CHARLES WASONGA

HATUA ya Mbunge wa Tiaty William Kamket kujiunga na muungano wa Kenya Kwanza (KKA) imetajwa kama mwanzo wa mwisho wa Kanu katika kaunti ya Baringo na eneo zima la Kaskazini mwa Bonde la Ufa.

Inaashiria ushindi wa Rais Mteule William Ruto katika juhudi zake za kudhibiti eneo hilo kisiasa kwa kuwazima wapinzani wake wote.

Hii ni kwa sababu Bw Kamket, ndiye mbunge wa kipekee, ambaye alikaidi mawimbi ya kisiasa ya chama cha United Democratic Alliance (UDA) katika kaunti ya Baringo na kuhifadhi kiti chake kwa tiketi ya chama pinzani katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Alizoa kura jumla ya kura 17,933 akifuatiwa na mpinzani wake wa karibu, Asman Kamama wa chama cha Kenya Union Party (KUP) aliyepata 13,037.

Peter Ng’eleiyo aliyewania kiti hicho kwa tiketi ya UDA alipata kura 110, ishara kwamba chama hicho kinachoongozwa na Rais Mteule William Ruto hakishabikiwi na wakazi wa eneo hilo.

Mgombea wa Azimio

Hali hiyo pia ilithibitishwa katika matokeo ya uchaguzi wa urais kwani mgombea wa Azimio la Umoja One Kenya Raila Odinga alizoa kura nyingi kuliko Dkt Ruto.

Bw Odinga alijishindia jumla ya kura 25,282 huku Ruto akipata kura 5,708 pekee. Sababu ni kwamba Kanu, inayoongozwa na seneta wa zamani wa Baringo Gideon Moi, ni moja kati ya vyama tanzu katika Azimio.

Lakini jaribio la Gideon kuhifadhi kiti chake cha useneta kwa muhula wa tatu, lilifeli alishindwa na mbunge anayeondoka wa Baringo Kaskazini William Cheptumo.

Isitoshe, juzi kakake mkubwa, Raymond Moi, alipoteza kiti chake cha ubunge Rongai.

Hii ni baada yake kubwagwa na mgombeaji wa kiti hicho kwa tiketi ya chama cha UDA Paul Chebor, almaarufu “Mamba” katika uchaguzi uliofanyika mnamo Alhamisi Agosti 29.

Shoka la UDA

Shoka la UDA pia lilimwangukia Katibu Mkuu wa Kanu Nick Salat ambaye alipoteza katika kinyang’anyiro cha ubunge katika eneo la Bomet Mashariki.

Bw Salat aliweza kupata kura 13, 425 pekee nyuma ya Richard Yegon wa chama cha UDA aliyezoa jumla ya kura 35,431.

Wachanganuzi wa siasa za eneo la Bonde la Ufa wanasema kuwa ilikuwa vigumu kwa Bw Kamket kusalia ndani ya Kanu na Azimio katika eneo hilo ambalo ni ngome ya kisiasa ya Dkt Ruto.

“Kwa hivyo, ili kujiondolea upweke wa kisiasa, haswa baada ya kubwagwa kwa mwenyekiti wake Gedion Moi, Katibu Mkuu Nick Salat na mbunge wa Rongai Raymond Moi, Kamket alilazimika kutafuta hifadhi katika Kenya Kwanza,” anasema Dkt Philip Chebunet.

“Bila shaka hii inaashiria kuwa kuna uwezekano mkubwa kwamba Kanu itazikwa katika kaburi la sahau kisiasa katika eneo la Bonde la Ufa ambako kilikuwa na ushawishi mkubwa zaidi wakati wa utawala wa Hayati Daniel Moi,” anaongeza msomi huyo ambaye ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Moi, Eldoret.

Kulingana na mchanganuzi huyo kuyeyushwa kwa Kanu katika eneo la Bonde la Ufa sasa kunathibitisha Dkt Ruto ndiye mshindi katika vita vya ubabe wa kisiasa kati yake na Gideon.

Baada ya kifo Mzee Moi mnamo 2020, Gideon ndiye alitwikwa wajibu wa kuvumisha Kanu kwa lengo la kurejesha sifa zake za zamani katika eneo hilo na kitaifa.

Hata hivyo, matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu yameonyesha amefeli na kusababisha Kanu kumezwa na UDA.

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: Magavana wapya waelimishwe kuhusu Sheria ya Ajira

Lusaka aahidi kuajiri wafanyakazi wa afya kuboresha huduma

T L