• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 9:12 AM
MIKIMBIO YA SIASA: Kwa mkakati huu, Sakaja yuko vizuri!

MIKIMBIO YA SIASA: Kwa mkakati huu, Sakaja yuko vizuri!

NA CHARLES WASONGA

UAMUZI wa Gavana wa Nairobi Johson Sakaja kuteua wafuasi wa Azimio la Umoja-One Kenya katika baraza lake la mawaziri umeonekana kama sehemu ya mkakati wa kuzima uasi kutoka kwa madiwani wa mrengo huo wa walio wengi.

Wadadisi wa siasa za Nairobi wanasema Bw Sakaja alichukua hatua hiyo, inayokinzana na msimamo wa mrengo wake wa Kenya Kwanza, kuboresha nafasi yake ya kusalia mamlakani baada ya uchaguzi mkuu wa 2027.

Duru zilieleza safu hii kwamba Bw Sakaja alikataa kuteua wengi waliopendekezwa kwake na vigogo wa muungano wa Kenya Kwanza (KKA) na badala yake kuteua watu anaoamini watamsaidia kufikia malengo sasa na miaka ijayo.

Akitangaza baraza lake la mawaziri Jumatano, Gavana Sakaja aliwataja alimrejesha Charles Kerich katika Wizara ya Fedha na Mipango ya Kiuchumi, Brian Mulama (Wizara ya Ukuzaji Talanta), Patrick Mbogo (Uchukuzi na Ujenzi), Stephen Mwangi (Mipango ya Jiji) na Ibrahim Auma (Utawala na Masilahi ya Wafanyakazi).

Rosemary Kariuki (Biashara Ndogo Ndogo), Maureen Njeri (Mazingira na Usafi), Anastacia Mutethia (Afya) na Michael Gumo (Ubunifu na Uchumi wa Kidijitali) na Susan Silantoi ambaye ameteua waziri atakayesimamia idara ya ushirikishwaji wa umma na uhusiano mwema.

Bi Kariuki, ambaye ameteuliwa kuwa Waziri wa Biashara, ni Mkurugenzi wa ODM anayesimamia idara ya usajili wa wanachama wapya.

Ni bintiye aliyekuwa mwanasiasa mashuhuri na Mbunge wa Nyandarua JM Kariuki na ni mshirika wa karibu wa kiongozi wa ODM Raila Odinga.

Bw Michael Gumo ni mwanawe aliyekuwa Mbunge wa Westlands na mwanasiasa mwenye ushawishi mkubwa Nairobi Fred Gumo.

Awali, duru zilisema ODM ilipanga kumteua kuwa mwakilishi wa Kenya katika Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) kama asante ya kujiondoa katika kinyang’anyiro cha ubunge Westland kumpisha mbunge wa sasa Tim Wanyonyi.

Ibrahim Auma ambaye ameteuliwa kuwa Waziri wa Utawala na Masilahi ya Wafanyakazi pia ni mshirika wa karibu wa Bw Odinga, ambaye pia ndiye kiongozi wa Azimio.

“Gavana Sakaja aliamua kujumuisha wafuasi wa Azimio katika baraza lake la mawaziri kwa misingi kuwa atafanyakazi kazi na bunge linalodhibitiwa na madiwani wa mrengo huo. Isitoshe, Spika wa Bunge hilo Ken Ngondi alidhaminiwa na muungano huo wa upinzani,” anasema mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Javas Bigambo.

Katika bunge hilo, mrengo wa Azimio unawakilishwa na madiwani 67 waliochaguliwa huku ule wa KKA ukiwa na madiwani 53.

Hii ndio maana mrengo huo unaoongozwa na Bw Odinga ndio umetoa kiongozi wa walio wengi katika bunge la kaunti ya Nairobi ambaye ni Diwani wa Makongeni Peter Imatwok.

Bunge hili la kaunti ya Nairobi ni miongoni mwa mabunge machache nchini ambayo idadi kubwa ya madiwani wanatoka mrengo wa upinzani ilhali Gavana anatoka mrengo wa walio wachache au hakudhaminiwa na chama chochote cha kisiasa.

“Katika hali kama hii, Gavana Sakaja hana budi ila kufanya kazi na mrengo wa Azimio kusudu afaulu kupitisha ajenda zake katika bunge hilo. Isitoshe, Gavana Sakaja anataka kujikuza kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa 2027 ikizingatiwa kuwa Nairobi ni ngome ya kisiasa ya mrengo wa upinzani,” anaongeza Bw Bigambo.

You can share this post!

TAHARIRI: Gavana Mwangaza asafiane nia na madiwani wake

Jumuiya ya kaunti za Pwani: Raia wanataka kuona vitendo,...

T L