• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 10:55 AM
MIKIMBIO YA SIASA: Ongwae, Ong’era wamtaliki Baba kudoea minofu ya Ruto

MIKIMBIO YA SIASA: Ongwae, Ong’era wamtaliki Baba kudoea minofu ya Ruto

HATUA ya Gavana wa zamani wa Kisii James Ongwae na aliyekuwa Mbunge Mwakilishi wa kaunti hiyo Janet Ong’era kugura ODM imefasiriwa kama mwanzo wa kufifia kwa chama hicho eneo zima la Gusii.

Wadadisi wa masuala ya kisiasa wanabashiri kwamba hivi karibuni wanasiasa wengine wa mrengo wa Azimio watafuata nyayo za wawili hao ambao wamekuwa wandani wa Raila Odinga kwa zaidi ya miaka 20.

“Hii ni kionjo tu, hivi karibuni nyota wengi wa kisiasa kutoka kaunti za Kisii na Nyamira watagura vyama tanzu vya Azimio, haswa ODM na Jubilee. Na bila shaka ni wazi kuwa wanasiasa hao wanaelekea kujiunga na muungano tawala, wa Kenya Kwanza,” anasema mchanganuzi wa masuala ya kisiasa na uongozi Dismus Mokua.

Hata hivyo, walipotangaza kuhama ODM, Bw Ongwae na Bi Ong’era hawakufichua chama ambacho watajiunga nacho.

Hata hivyo, waliahidi kujitengenezea mkondo wao wa kisiasa ambao, kwa mtazamo wao, “utalinda masilahi ya jamii ya Abagusi”.

“Leo (Alhamisi) tumefikia uamuzi huu baada ya kutathmini kwa makini matukio ya kabla ya uchaguzi mkuu uliopita na haswa jinsi chama hicho kilitudhulumu na wafuasi wetu. Kwa hivyo tumeamua kugura ODM na hivi karibu tutatangaza mwelekeo tunaohisi utatetea na kuendeleza masilahi yetu kama jamii ya Gusii,” Bw Ongwae akasema huku akiwa ameandamana na Bi Ong’era.

Itakumbukwa kwamba wanasiasa hao wawili ni miongoni mwa wengine 12 waliomtembelea Rais William Ruto katika makazi ya rasmi ya Naibu Rais Karen, Nairobi, mnamo Septemba 9.

Wanasiasa hao walielezea kuwa wako tayari kufanya kazi na serikali ya Dkt Ruto kwa manufaa ya jamii ya Abagusi.

“Tulifanya mazungumzo na Rais mteule (sasa Rais) na tukamhakikishia kuwa tuko tayari kufanya kazi naye na kuunga mkono serikali yake,” Bw Ongwae akawaambia wanahabari baada ya mkutano huo.

Ujumbe huo pia ulishirikisha Bi Ong’era na wabunge wa zamani, Jimmy Angwenyi (Kitutu Chache North), Zepedeo Opere (Bonchari), Ben Momanyi (Borabu), Manson Nyamweya (South Mugirango), Zadock Ogutu (Bomachoge Borabu) na Stephen Manoti (Bobasi).

Wengine walikuwa ni aliyekuwa Waziri Msaidizi wa Uchukuzi Chris Obure, Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Jamii ya Gusii John Matundura na aliyekuwa mwaniaji wa kiti cha Mbunge Mwakilishi wa Kike Nyamira, Emily Nyagarama.

Ziara ya viongozi hao Karen, iliashiria wazi kwamba nia yao ni kutalikiana kisiasa na Bw Odinga na kumkumbatia Rais Ruto.

Wakosoaji wa Bw Ongwae na wenzake wanadai kuwa wanasiasa hao wanaongozwa na masilahi yao kama watu binafsi wala sio jamii ya Abagusii kwa ujumla.

“Hawa ni watu ambao wanapigania tumbo zao wala sio jamii yetu. Kwa nini hawazungumzii hatua ya Rais Ruto kuacha nje kaunti za Kisii na Nyamira katika uteuzi wa makatibu wa Idara za Wizara za serikali?” anauliza Wakili Danstan Omari.

You can share this post!

KIGODA CHA PWANI: Madeni, ufisadi vyadumaza ukuaji wa...

JUKWAA WAZI: Gachagua, Mutua walumbana kuhusu...

T L