• Nairobi
  • Last Updated May 22nd, 2024 5:30 PM
MIKIMBIO YA SIASA: Raila amempisha Kalonzo kuongoza Azimio la Umoja?

MIKIMBIO YA SIASA: Raila amempisha Kalonzo kuongoza Azimio la Umoja?

NA CHARLES WASONGA

KIONGOZI wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka anaonekana kama ambaye ndiye amechukua wajibu wa kuongoza muungano wa Azimio la Umoja One Kenya katika utekelezaji wa wajibu wa kuhakiki utendakazi wa serikali ya Kenya Kwanza.

Duru za kuaminika zimeiarifu safu hii kwamba aliyekuwa mgombea urais wa muungano huo Raila Odinga na rais wa zamani Uhuru Kenyatta wamekubaliana kumpa Bw Musyoka wajibu huo kujijenga kwa ajili ya kinyang’anyiro cha urais 2027.

Hii ndio maana katika siku za hivi karibuni, Bw Musyoka, amechukua sura ya kiongozi wa Azimio kwa kuwaongoza wabunge wa mrengo huo kukosoa baadhi ya maamuzi ya serikali changa ya Rais William Ruto.

Mnamo Ijumaa, makamu huyo wa rais wa zamani alihutubia kikao na wanahabari jijini Naironi ambapo aliwarai wabunge wa Azimio kutoidhinisha mawaziri wateule wenye dosari za kimaadili.

“Baadhi ya wale ambao wamependekezwa kuhudumu kama mawaziri serikalini wanakabiliwa na kesi za uhalifu mahakamani. Uteuzi wao ulikiuka hitaji la Sura ya Sita ya Katiba na hivyo tunawataka wabunge wetu kuwakatalia mbali,” Bw Musyoka akasema katika mtaa wa Karen akiandamana na zaidi wa wabunge 30 wa Azimio.

Lakini itakuwa vigumu kwa Azimio kufanikisha mpango huo ikizingatiwa kuwa baadhi ya wabunge waliochaguliwa kwa baadhi ya vyama tanzu katika muungano huo “wamehama” na kujiunga na mrengo wa Kenya Kwanza.

Aidha, kulingana na sheria za bunge hoja ya kuidhinisha au kukataa watu waliopendekezwa na Rais haihitaji thuluthi mbili ya idadi jumla ya wabunge (wabunge 233), bali wingi wa wabunge watakaokuwa ukumbini wake wa upigaji kura.

Bw Musyoka alitumia jukwaa hilo, la mkao na wanahabari, kuendelea kuiwekea presha serikali ya Kenya Kwanza akiitaka kupunguza bei ya mafuta namna Dkt Ruto na wandani wake waliwaahidi wananchi wakati wa kampeni za kuelekea uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

“Waliondoa ruzuku ya mafuta ambayo iliwakinga Wakenya kutokana na bei ya juu ya mafuta lakini sasa wamekataa kutekeleza mbinu mbadala za kuondolea Wakenya mzigo huo. Kama Azimio tunataka serikali ipunguze bei ya mafuta ili gharama ya maisha ipungue,” akasema.

Wakati mwingine ambapo Bw Musyoka alionekana kuwa “kiongozi” wa Azimio ilikuwa ni mnamo Septemba 17, 2022 alipoongoza uzinduzi wa majina ya viongozi wa Azimio katika Bunge la Kitaifa na Seneti.

Japo, Bw Odinga na aliyekuwa mgombea mwenza wake Martha Karua walikuwepo katika shughuli hiyo, iliyofanyika katika afisi za Wakfu wa Jaramogi Oginga Odinga, Nairobi, Bw Musyoka ndiye alitwikwa hadhi ya kusoma orodha ya majina wabunge na maseneta hao.

Mbunge wa Ugunja Opiyo Wandayi aliteuliwa kuwa kiongozi wa Azimio katika Bunge la Kitaifa huku Seneta wa Kilifi Stewart Madzayo akatunukiwa wadhifa sawa na huo katika Seneti.

Kulingana na mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Tom Mboya, nafasi ambayo Bw Musyoka amepewa wakati huu katika Azimio inaashiria kuwa yeye ndiye ‘kiongozi wa upinzani’.

“Dalili zaonyesha kuwa Bw Odinga ameanza kuvua joho hilo la kiongozi wa upinzani ambalo amelivalia kwa zaidi ya miongo miwili. Inaonekana kwamba kuna mwafaka, japo usio rasmi, ndani ya safu ya uongozi wa Azimio kwamba Bw Musyoka ndiye aongoze wafuasi wa mrengo huo katika mapambano yake na serikali ya Dkt Ruto,” anaeleza Dkt Mboya ambaye ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Maseno.

Hata hivyo, haijabainika wazi ikiwa huu ni mkakati wa muda tu ambao Azimio inaendesha au inaashiria kuwa Mbw Odinga na Kenyatta wameastaafu rasmi kutoka siasa shindani na kumpisha Bw Musyoka.

Hata hivyo, akiongea juzi katika hafla za mazishi katika maeneo bunge ya Yatta (Machakos) na Mwingi ya Kati (Kitui), kiongozi huyo wa Wiper aliwahimiza wabunge na viongozi wengine wa Azimio kudumisha umoja huku akitangaza kuwania urais 2027.

  • Tags

You can share this post!

KIGODA CHA PWANI: Teuzi za Jumwa, Mvurya zaleta mkondo mpya...

JUKWAA WAZI: Wandayi na Kamande watofautiana vikali kuhusu...

T L