• Nairobi
  • Last Updated June 12th, 2024 4:24 PM
MITAMBO: Hiki hapa kipima ubora wa kahawa

MITAMBO: Hiki hapa kipima ubora wa kahawa

NA RICHARD MAOSI

KUPUNGUA kwa ardhi inayotumika kuendesha kilimo ni mojawapo ya changamoto ambazo zimekuwa zikiwakumba wakulima wa kahawa katika maeneo ya Mlima Kenya na Mt Elgon.

Pili, wakulima hawajakuwa wakipata hela nzuri kutokana na zao la kahawa kwa sababu ya ukosefu wa teknolojia inayoweza kutengeneza bidhaa nyinginezo ambazo zinatokana na zao hili.

Mbula Musau kutoka eneo la Athi River, Kaunti ya Machakos na mmiliki wa Utake Coffee anasema wakulima wanashauriwa kukumbatia teknolojia ya kuongezea kahawa thamani ili waweze kujipatia hela nzuri.

Kulingana na Mbula kwa siku nyingi kahawa imekuwa ikiwapatia hela ndogo sana kwa sababu imekuwa ikiuzwa kama mazao ghafi kwenye soko la kimataifa.

Ndiposa Mbula akaanzisha shirika la kuhakikisha wakazi wanafurahia kahawa iliyoongezewa thamani na ya hali ya juu na kwa wakati huo kuwakwamua wakulima kutoka kwenye lindi la umaskini ambapo wanaweza kuuza kahawa yao kwa hela nzuri.

Hii ni baada ya Mbula kugundua kuwa zao la kahawa lina uwezo wa kurutubisha mchanga na kustahimili hali ngumu ya anga au wadudu.

Mnamo 2022, Mbula aliratibiwa kama mnunuzi wa tano nchini ambaye hununua kahawa kutoka kwa wakulima kwa hela nzuri.

Anasema kuwa ili mjasiriamali afanikiwe katika kilimo-biashara cha kahawa, anahitaji vyombo maalum vinavyotumika kuunguza(kuchoma) kahawa, hii ikiwa ni njia mojawapo ya kuongezea zao hili thamani, ambapo mkulima anaweza kupata faida kutokana na zao lake kwa zaidi ya maradufu.

“Ikiwa mkulima atakua na mtaji wa kutosha anaweza kutengeneza bidhaa nyingi zinazotokana na kahawa hii ikimaanisha atakuwa amepanua soko la wanunuzi,” akasema.

Mtambo wa roast analyser

Anasema usimamizi au uangalizi wa kahawa ni wa manufaa sana ili kupunguza upotevu na tathmini bora ni ile ya kuchunguza kiwango cha unyevu mara tu baada ya kuvuna.

Ikumbukwe kuwa ni muhimu kukausha kahawa baada ya kuvuna ili kufikia unyevu unaoshauriwa, ili kukinga mazao dhidi ya ukungu au vimelea vingine.

Pili, hatua ya kukagua kahawa ni hatua ya kimsingi katika usindikaji wa zao hili kwani mkulima atahitaji vyombo vya roast analyser na moisture metre.

Michael Muki akionyesha kifaa cha moisture metre ambacho hutumika kupima kiwango cha unyevu ndani ya kahawa ghafi. PICHA | RICHARD MAOSI

Mtaalam Michael Muki anasema matumizi ya mtambo wa roast analyser huwasaidia wajasiria mali wanaokaanga kahawa kubaini muda mwafaka unaostahili kwa bidhaa hii kukaa kwenye meko.

Hii husaidia kahawa kudumisha ubora wa hali ya juu, kudumisha rangi na ladha ikizingatiwa kuwa kahawa inapobakia mekoni kwa muda mrefu inaweza kuharibika.

Roast analyser kifaa cha kubaini muda ambao unahitajika kwa kahawa kusalia mekoni wakati wa usindikaji. PICHA | RICHARD MAOSI

Kwa kawaida, kifaa hiki huelekezwa kwenye kahawa iliyokopolewa kutoka mekoni na huwa na aina maalum ya sensa inayoonyesha vipimo vinavyohitajika kwa mujibu wa bidhaa inayoandaliwa.

Aidha, mtambo wa moisture metre vilevile hutumika kupima kiwango cha unyevu unaopatikana ndani ya kahawa ghafi.

“Unyevu ni adui nambari moja kwa kahawa, hivyo basi inastahili kuwa na unyevu usiozidi asilimia 12.5.”

  • Tags

You can share this post!

MAZINGIRA: Mchango wa kilimo-bustani katika kuimarisha...

UJASIRIAMALI: Alitalii, akapata wazo la kuuza utalii na...

T L