• Nairobi
  • Last Updated February 26th, 2024 10:10 AM
MITAMBO: Mseto wa mitambo 2 kuandaa lishe kamilifu

MITAMBO: Mseto wa mitambo 2 kuandaa lishe kamilifu

NA RICHARD MAOSI

UHAKIKA wa kupata malisho ni mojawapo ya changamoto zinazowakumba wakulima na wafugaji hasa kipindi hiki cha ukame.

Hii ikimaanisha kuwa wakulima wengi wanataabika, na kwa sababu hiyo wanastahili kuhamasishwa kuhusu kilimo cha malisho ili kuepuka makali ya njaa.

Julia Ogola kutoka Eshiembekho eneo la Matungu Kaunti ya Kakamega anasema vijijini majani hukatwa kwa kutumia upanga na hatimaye kuhifadhiwa ili yatumike msimu wa kiangazi.

Kibinafsi anaona kuwa hii haitoshi kwani pia wanatakiwa kufahamu nyenzo faafu za kuhifadhi malisho mengi na kwa kipindi kirefu.

“Njia mojawapo ambayo imezoeleka ikiwa ni ile ya kukaushwa na kupitizwa kwenye mtambo wa chaffcutter kuunda vipande vidogo,” akasema.

Alifichulia Akilimali kuwa wakazi wengi kutoka eneo la Matungu ni wakulima wa mboga za kiasili, viazi tamu na maharagwe ya soya, ingawa ni wachache sana wanaofugaji wa ng’ombe na mbuzi.

Kwa upande mwingine anasema kuwa malisho ya mifugo kutokana na mseto wa kunde, mafuta ya canola, viazi tamu, shayiri na nyasi za napier huboresha uzalishaji wa maziwa.

Julia Ogola kutoka Eshiembekho eneo la Matungu Kaunti ya Kakamega akiwalisha mbuzi wake.
PICHA|RICHARD MAOSI

Kitaaluma mkulima anashauriwa asiwalishe mifugo wake majani mabichi, kwani ni asilimia 12 tu ambayo huwa imebeba virutubisho na kwa sababu hiyo ajizatiti kuyakausha.

Kulingana na Ogola, wakulima wengi kutoka Matungu wanatumia aina spesheli ya mtambo wa mixer ambao umeongezewa sehemu ya chaffcutter kwa ajili ya kukatakata malisho vipandevipande.

Kinyume na awali ambapo mtambo wa mixer umekuwa ukitumika tu kuchanganya sehemu mbalimbali za malisho ambayo tayari huwa yamekatwa vipande vidogo.

Aina hii ya mtambo ni uvumbuzi wa wataalam wa Juakali humu nchini na manufaa yake ni mengi, kwanza mkulima anaweza kutengeneza chembe ndogondogo za malisho na kwa wakati huo akatumia aina hii maalum ya mixer kuchanganya lishe ya sampuli moja na nyinginezo.

Aliongezea kuwa lishe sahihi kwa mifugo au mbuzi wa maziwa ni ile ambayo imebeba virutubisho vya protini, wanga , vitamini na madini ya calcium phosphorus na potassium.

Kuboresha ujuzi wake, Ogola alipokea mafunzo kutoka shirika la Anglican Development Services eneo la Magharibi na akabaini kuwa mimea kama vile soya huwa na kiwango cha juu cha protini.

Kwa hivyo mkulima anaweza kusaga viazi tamu, ambavyo huchanganyika na mseto wa mikunde au unga wa samaki katika sehemu ya pili ya mtambo wenyewe.

Na mseto wenyewe ukatokea chini ukiwa lishe kamilifu, kwa matumizi ya mifugo.

Pili humsaidia mkulima kutekeleza hatua mbili za uandaji wa malisho ya mifugo kwa kutumia aina moja ya mtambo.

Anasema ili kufaidi matumizi ya aina hii ya mtambo kwanza ni lazima mkulima aweze kubaini aina ya malisho ambayo anataka kuwalisha mifugo wake.

Aidha malisho huwa yamegawika katika sehemu mbili kuu ikiwa ni aina za kunde na nyasi za kawaida ambazo kwa kawaida hufanya vyema katika sehemu zinazopokea kiasi kidogo cha mvua.

  • Tags

You can share this post!

Ufugaji bata wanawiri kupitia lishe ya wadudu

ZARAA: Kifaa cha mkono kuchuma chai, kupunguza gharama

T L