• Nairobi
  • Last Updated February 26th, 2024 11:20 AM
Mshangao chatu mkubwa akipatwa jumba la kifahari wakati wa ubomozi

Mshangao chatu mkubwa akipatwa jumba la kifahari wakati wa ubomozi

SHABAN MAKOKHA na CECIL ODONGO

Kulikuwa na mshangao Jumatano Novemba 29, 2023 baada ya joka kubwa kupatikana kwenye makazi ya kifahari ya bwenyenye wakati ubomozi ulipokuwa ukiendelea katika mtaa wa Milimani, viungani mwa mji wa Kakamega.

Mtaa wa Milimani huwa ni wa kifahari kwa kuwa upo karibu na Ikulu ndogo ya Kakamega, Hoteli za Milimani Resort na Golf na pia Kanisa la Kianglikana (ACK).

Ndio mtaa wa mabwenyenye mjini Kakamega na kuna majumba mengine na hoteli nyingine za kifahari eneo hilo ambalo magari ya kifahari ndio huyapitia mabwenyenye wakitoka na kurejea makwao.

Aidha, miundomsingi ni bora zaidi mtaani Milimani kwa kuwa barabara zote zimewekwa lami, hakuna msongamano wa magari na kuna mazingira tulivu ambayo bila shaka yanaakisi utajiri wa mtaa huo.

Wakati wa ubomozi ambao ulikuwa ukiendeshwa na serikali mtaani humo jana, tukio la kushangaza lilishuhudiwa baada ya joka na kobe wawili kupatikana kwenye nyumba ya mfanyabiashara mmoja maarufu tena tajiri.

Jengo hilo ni kati ya majengo ambayo yalikuwa yanabomolewa ili kutoa nafasi kwa ujenzi wa majumba ya gharama nafuu yanayoendeshwa serikali kuu.

Licha ya wengi kufikiria kuwa wanyama hao wangeuawa kutokana na hatari ambayo ipo, wafanyakazi wa mfanyabiashara huyo bwenyenye waliwalinda na kuwaelekeza katika eneo salama.

Saa chache baadaye, maafisa kutoka Shirika la Huduma kwa Wanyamapori walifika na kuenda na wanyama hao wa porini bila kuguswa wakiwa salama wa salmini.

Hata hivyo, tukio hilo limezua gumzo kuwa mfanyabishara huyo huenda alikuwa akiwatumia kulinda utajiri wake ambao huenda hakuupata kwa njia halali.

Aidha, kuna dhana kuwa wanaofuga majoka, kobe na wanyama wa porini kama chui ni wachawi.  Inaaminika kuwa kuwafuga kunaleta utajiri na husaidia mtu kuongeza utajiri wake.

Watu wengi wakiwemo wasanii wanawafuga wanyama hao wa porini ili kuendelea kuwika ulingoni na kuwazima maadui wao hasa wale ambao huwapa ushindani.

Kwa mujibu wa Mzee Yusuf Olwichi, 83, kutoka Navakholo ambaye hutumia dawa za kitamaduni kuwatibu wagonjwa, watu huwafuga majoka ili kuwa na pesa na pia kujilinda kutoka kwa matajiri wenzao ambao wanashindana nao.

Bw Olwichi alisimulia kuwa majoka hao hupewa majina ambayo huendana na kitita na uwepo wao humaanisha kuwa tajiri ambaye amewafuga hatafilisika.

Aidha mzee huyo anasema kuwa mtu huweza kujilimbikizia utajiri usiomithilika kwa kuwafuga majoka.

“Ndiyo majoka husababisha mtu kuwa na utajiri mwingi sana. Ukijiunga na ushirikiana kwa sababu ya utajiri, kuna sheria ambayo lazima uzifuate.

“Lazima utakuwa na siri ya aina yake na utakuwa na chumba ambacho hakuna mtu huingia. Maisha yako huzunguka kwa mtindo fulani ambao mara nyingi ni wa siri,” akasema Mzee Olwichi.

Aliongeza kuwa majoka au wanyama wa pori wengine ambao wamefungwa, huwa hawaonekani mchana na huachiliwa kutembea nyakati za usiku.

Kuzururazurura kwao hasa kwenye vijiji ndiko huwaingiza hofu wanakijiji hasa watoto ambao hutakiwa kufika nyumbani mapema na kukatazwa kupitia karibu na makazi ya watu wanaoaminika ni matajiri na wametumia uchawi

  • Tags

You can share this post!

Mume analala nje kama kuku na ninapomuuliza anazua ugomvi,...

Uasin Gishu sasa ndio kitovu cha wizi wa ardhi, ujio wa...

T L