• Nairobi
  • Last Updated October 1st, 2023 9:40 PM
Mtego wa Azimio ulivyomnasa Ruto

Mtego wa Azimio ulivyomnasa Ruto

NA BENSON MATHEKA

MAZUNGUMZO kuhusu maridhiano yanayohusisha wabunge wa miungano miwili ya kisiasa nchini yameonyesha dalili za kugonga ukuta kufuatia misimamo ya vinara na washirika wa pande zote mbili – Kenya Kwanza na Azimio la Umoja One Kenya kuhusu kufunguliwa kwa sava za Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Kwa kukubali mazungumzo hayo, huenda Rais William Ruto alijiweka kwa mtego wa muungano wa Azimio ambao unataka mzozo wa kisiasa usuluhishwe kisiasa badala ya bungeni alivyopendekeza kiongozi wa nchi.

Misimamo mikali ya pande zote kuhusu suala hilo imevutia mawaziri ambao japo kisheria, hawafai kujihusisha na siasa wanalaumu muungano wa Azimio One Kenya huku wadadisi wakisema kuhusika kwao katika mchakato huo wa kisiasa kutaufanya usipige hatua.

Waziri wa Uchukuzi Kipchumba Murkomen, mmoja wa wandani wa Rais William Ruto Ijumaa aliongeza sauti yake kwenye mchakato huo kwa kupuuza takwa la Azimio la Umoja One Kenya la kufunguliwa kwa sava ambazo Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ilitumia katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022.

Kulingana na Murkomen na mwenzake wa Biashara Moses Kuria ambao walikuwa wanasiasa wa miaka mingi kabla ya kuteuliwa mawaziri miezi sita iliyopita, Azimio inapaswa kusahau kufunguliwa kwa sava.

Wawili hao wanasisitiza kauli ya Rais Ruto na Naibu Rais Rigathi Gachagua kwamba lengo la Azimio ni kutaka serikali ya nusu mkate na kwamba hakuna hitaji lolote la kikatiba la Rais Ruto kufungua sava hizo.

“Iwapo Raila anafikiria sava za IEBC zinaweza kufunguliwa na Rais ajue kwamba Rais Ruto hajawahi kuwa na funguo za sava za IEBC. Raila anaweza kwenda kufungua sava lakini tunajua lengo lake sio sava anataka serikali ya nusu mkate na hatapata,” akasema Murkomen.

Wadadisi wanasema kwamba takwa la kufunguliwa kwa sava huenda likawa tata na kulemaza mazungumzo kwa kuwa Azimio inasisitiza lazima zifunguliwe huku kiongozi wa chama cha Narc Kenya Martha Karua akionekana kuweka wazi lengo la muungano huo wa upinzani.

Kulingana na Bi Karua, iwapo sava zitaonyesha Kenya Kwanza ilishinda, watakubali na kuiachia minofu itafune wakimeza mate, lakini iwapo zitaonyesha Azimio ilishinda, basi Ruto na serikali yake italazimika kuondoka mamlakani na kupisha Raila na Azimio.

Kulingana na mchambuzi wa siasa Dkt Isaac Gichuki, shinikizo za Azimio kuhusu kufunguliwa kwa sava na kukataa kabisa kwa Ruto na Kenya Kwanza kunaonyesha huenda kuna kitu pande zote mbili zinakifahamu na ambacho serikali inaogopa.

“Ukweli kwamba kikatiba, Rais hana mamlaka ya kufungua sava za tume huru kama IEBC. Lakini alijiweka kwa mtego alipokubali mazungumzo ya maridhiano ambayo ni ya kisiasa kumaanisha alikubali mchakato wa kisiasa kusuluhisha mzozo wa kisiasa kufuatia maandamano ya upinzani nao Azimio wakauchangamkia,” akasema Dkt Gichuki.

Japo Rais Ruto na muungano unaotawala wa Kenya Kwanza wanataka mazungumzo ya maridhiano yawe ndani ya Bunge na pande zote zimechagua wabunge saba kila mmoja, Azimio inataka suala la kufunguliwa kwa sava liwekwe kwenye meza; takwa ambalo serikali imekataa kiwango cha kufanya mawaziri kama Murkomen na Kuria kulizamia.

“Hili ndilo suala tata ambalo linaweza kulemaza mazungumzo,” asema Dkt Gichuki.

  • Tags

You can share this post!

‘Uhaba mkubwa wa kondomu mjini Eldoret’

DINI: Kusamehe ni uhodari na ushujaa mkubwa

T L