• Nairobi
  • Last Updated June 12th, 2024 4:24 PM
Muda uliosalia kabla ya mtihani wa kitaifa unatosha kujiandaa

Muda uliosalia kabla ya mtihani wa kitaifa unatosha kujiandaa

MTIHANI huzua changamoto kwa yeyote anayepania kuufanya. Nakisia ni kwa sababu ya ushindani unaohusishwa nao, hasa nchini mwetu. Aghalabu mtihani humfanya anayehusika kuingiwa na wasiwasi ambao hudumaza uwezekano wake wa kufuzu anavyoazimia. Huanza kukata tamaa kwa kuhisi hawezi kuumudu mrundiko wa kazi anayopaswa kuidurusu kabla ya mtihani kuwadia.

Wengine huzidiwa na dhana ya uchechefu. Hii ni dhana ambapo mtu huziona nafasi za kushindaniwa kuwa chache mno hivi kwamba hata akijitahidi hawezi kuwa miongoni mwa washindi.

Kwa msingi huu, yeye hukata tamaa na kufanya maandalizi yake bila madhumuni maalum. Hivi ndivyo watu wengi wenye fursa aali za kuupasi mtihani hupoteza nafasi zao.Hatua ya awali zaidi ya maandalizi kabambe kwa mtihani ni kuutambua uwezo wako. Ukisha, jiaminishe kwamba una nafasi maalum ya kuibadilisha jamii yako.

Vigezo vilivyowekwa na jamii ambavyo vimegeuka kuwa vikwazo visikuhadae ukaanza kujionea imani. Linalokupasa kufanya ni kujitolea kikamilifu; yaani usisaze hatua itakayokuwezesha kuupita mtihani kisha ukaijutia baadaye.Nina hakika kuwa kila mtahiniwa huwa na lengo la kujishughulisha na elimu yake.

Hata hivyo, ni wachache wanaoyahusisha malengo yao na hatua zao za kila siku. Wengi hukosa au kushindwa kuibuka na mikakati ya kuzigeuza ndoto zao, malengo yao kuwa matokeo halisi.

Unapojiandaa kwa mtihani wako, ni muhimu uibuke na mikakati ya kuitimiza ndoto yako.Katika mkakati wako, jambo moja ni la kimsingi; kuutambua uwezo na udhaifu wako.

Ikiwa utaweza kuukiri udhaifu wako sawa na uwezo wako, una uwezekano mkubwa wa kufaulu. Nakili masomo unayoyamudu na yale usiyoyamudu. Katika masomo unayoyamudu, orodhesha faslu usizozielewa kikamilifu ili kujua kina cha msaada utakaouhitaji ili kuzimudu. Je, una mwao kuhusu faslu fulani hata kwenye masomo yanayokulemea? basi ziorodheshe vilevile.

Orodha

Ukiisha kuorodhesha faslu zitakazokuzuia kuibuka na alama bora zaidi katika masomo unayoyamudu, tafuta msaada wa wenzio kuhusiana na vipengele hivyo.

Ikiwa vipo vipengele wasivyovielewa wenzio vilevile, tafuta msaada wa walimu/mwalimu wa somo hilo. Hatua hii itakuhakikishia alama bora zaidi katika somo hilo ili kuimarisha alama yako ya jumla.

Aidha, itakuwezesha kuimarisha uwezekano wako wa kusomea taaluma uitakayo kwa kujipa nafasi bora ya kutimiza alama faafu katika masomo manne ya kimsingi ya taaluma hiyo.

Kuzamia faslu unazozielewa kiasi katika masomo usiyoyamudu kutakupa ujasiri wa kuupita mtihani kwa jumla. Hivi ni kwa sababu kila unapokuwa na atiati kuhusiana na udhaifu wako, hata unayoyamudu hutoweka. Ndiposa ni muhimu kwa mwanafunzi kukuza ujasiri wake wa kuukabili mtihani licha ya maandalizi mengine.

Ugawe muda wako kihalisia. Tenga muda mfupi wa kuyanoa makali yako katika masomo unayoyamudu. Orodhesha mada ndogo mahsusi za kuangazia na kwa kipindi bainifu ulichokitenga. Ukishazisoma, jitathmini ili kujifahamisha ukubwa wa hatua uliyoipiga.Tengea vipengele vinavyokutatiza muda zaidi ili kuimarisha uwezo wako kwavyo.

Tafuta msaada zaidi katika vipengele hivi. Kuzidi kuvisoma mwenyewe bila msaada wa mwalimu kutakupotezea muda. Mwalimu wako anajua mbinu itakayokufaa zaidi ili kuyaweka masuala haya kwenye kumbukumbu yako.

Suala ambalo lingekuhitaji saa mbili kulielewa laweza kueleweka kwa dakika kumi msaada wa mwalimu ukiwapo. Usipoteze muda wako!Hatimaye, amini kwamba una nafasi muhimu ya kuubadilisha ulimwengu.

Si lazima uwe rais, katibu wa kudumu, mhandisi, mwanasheria, mwalimu ili kutoa mchango wako. Taaluma zipo nyingi wala hakuna iliyo dhalili kuliko nyingine. Nina hakika zipo nyingine zitakazobuniwa kadri mazingira na mahitaji ya binadamu yanavyobadilika na kuibua changamoto mpya.

Huenda itakayobuniwa itakuhusisha, nawe upo mbioni kukata tamaa! Usimtazame mtu mwingine yeyote na kujihisi dhalili mbele yake, kamuulize Muumba wako azma yake ya kukuumba na punde uijuapo, jizatiti kuitimiza.

You can share this post!

Maswali anayopaswa kujiuliza mwandishi yeyote wa kubuni...

Ruto na Raila hawafai kupuuza agizo la Rais