• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
MWALIMU WA WIKI: Mbunifu, mtafiti na mwajibikaji pia

MWALIMU WA WIKI: Mbunifu, mtafiti na mwajibikaji pia

NA CHRIS ADUNGO

FAHARI kubwa ya mwalimu ni kuona mtoto aliyeingia shuleni bila kujua lolote akipiga hatua kubwa katika safari ya elimu na kuanza kufahamu stadi za kusoma na kuandika.

Kufundisha wanafunzi wa madarasa ya chini kunahitaji mwalimu kutumia mbinu anuwai zitakazomwezesha kukuza ubunifu wa watoto na kuwaamshia ari ya kuthamini masomo.

Zaidi ya vifaa vya kidijitali ambavyo husisimua wanafunzi wa umri mdogo na kuchochea bongo zao kufanya kazi; matumizi ya nyimbo, video, vibonzo, michezo ya kuigiza, michoro na picha za rangi ni namna nyingine ya kufanya shughuli za darasani kuwa za kuvutia.

Haya ni kwa mujibu wa Bi Maria Wangui Thairu ambaye kwa sasa ni Naibu Mwalimu Mkuu katika shule ya msingi ya North Riara Ridge Academy, Kaunti ya Kiambu.

“Shughuli za ujifunzaji na ufundishaji zitakuwa nyerezi iwapo mwalimu atasikiliza wanafunzi, kubaini mahitaji ya kila mmoja wao, kushughulikia baadhi ya changamoto zinazowakabili na kuwaelekeza ipasavyo hatua kwa hatua,” anatanguliza Bi Maria.

Kwa mtazamo wake, mwalimu bora anastahili kuteka saikolojia ya wanafunzi kwa wepesi, kupalilia vipaji vyao na kuwatia moyo wale wanaotatizika kulimudu somo lake.

“Wanafunzi wanahitaji mazoezi mengi iwezekanavyo ili wajiamini katika usomaji na ujifunzaji wa dhana mpya. Wanastahili kupewa fursa nyingi za kuhusisha wanachokisoma darasani na matukio ya kawaida katika jamii,” anahoji.

“Mwalimu bora ni mwajibikaji, mbunifu na mtafiti. Anatawaliwa na mapenzi ya dhati kwa taaluma yake, anajituma kazini bila kushurutishwa na ana msukumo wa kutaka kujifunza mambo mapya. Ni mnyumbufu katika maandalizi ya vipindi vya somo lake na anaelewa masuala yote yanayofungamana na mtaala,” anasisitiza.

Maria alizaliwa Mabroukie Tea Estate, eneo la Limuru, Kiambu.

Ndiye mwanambee katika familia ya watoto wanane wa Bi Mary Njoki na marehemu Bw Stephen Waiganjo.

Alianza safari ya elimu katika shule ya msingi ya Rwaka, Limuru (1981-1988) kabla ya kujiunga na shule ya upili ya Maryhill Girls, Thika (1989-1992) kisha Chuo cha Mafunzo ya Ualimu cha St Mark’s Kigari, Kaunti ya Embu (1997-1999).

Ingawa alitamani kusomea uuguzi, aliyemhimiza kujitosa katika ulingo wa ualimu ni Bw Josphat Ng’ang’a aliyemfundisha somo la Kiingereza na kumpokeza malezi bora ya kiakademia katika shule ya msingi ya Rwaka.

Baada ya kuhitimu, Maria alianza kufundisha Kiswahili na somo la Dini katika shule ya North Riara Ridge mnamo Septemba 1999.

Alipanda ngazi kuwa Naibu Mwalimu Mkuu mnamo 2005 na akawa Mkuu wa Idara ya Kiswahili kati ya 2007 na 2017.

Amefundisha idadi kubwa ya wataalamu ambao sasa wanashikilia nyadhifa za hadhi katika sekta mbalimbali ndani na nje ya ulingo wa Kiswahili.

Kubwa zaidi katika maazimio yake ni kuzamia uandishi wa hadithi za watoto ili kuendeleza kipaji cha utunzi wa kazi bunilizi kilichoanza kujikuza ndani yake utotoni. Kwa pamoja na mumewe Bw Peter Thairu, wamejaliwa watoto watatu – Esther, Paul na Steve.

 

You can share this post!

TUSIJE TUKASAHAU: Walioathiriwa na wanyamapori eneo la...

TAHARIRI: Njaa: Wanafunzi katika maeneo kame walishwe...

T L