• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 11:05 AM
MWALIMU WA WIKI: Mwalimu bambam na mwanamitindo stadi

MWALIMU WA WIKI: Mwalimu bambam na mwanamitindo stadi

NA CHRIS ADUNGO

MWALIMU bora anastahili kuchangamkia masuala yanayohusiana na mtaala na kuwa mwepesi wa kubuni mbinu anuwai za ufundishaji.

Kwa kuwa safari ya elimu ni sawa na vidato vya ngazi, wanafunzi wanahitaji mazoezi mengi ili wajiamini katika usomaji na ujifunzaji wa dhana mpya.

Haya ni kwa mujibu wa Bi Anne Otieno Adhiambo ambaye kwa sasa ni mwalimu katika shule ya St Mary’s Aberdare, Kaunti ya Nyandarua.

Kwa mtazamo wake, mwanafunzi anapaswa kupanda ngazi ya elimu kwa utaratibu ufaao na kuelekezwa ipasavyo katika kila hatua.

“Mwalimu bora ni mwajibikaji, mbunifu na mtafiti. Ana mapenzi ya dhati kwa taaluma yake, anajituma kazini na ana msukumo wa kutaka kujifunza mambo mapya. Anastahili kuwa karibu na wanafunzi wake, alee vipaji vyao na awaamshie hamu ya kuthamini masomo,” anasema.

Anne alizaliwa na kulelewa katika kijiji cha Sasi, eneo la Ndhiwa, Kaunti ya Homabay. Ndiye wa nne kuzaliwa katika familia ya watoto wanane wa Bw Marcel Otieno na Bi Dorine Akinyi.

Alisomea katika shule za msingi za Sasi (1996-2000) na Kemba Academy, Ndhiwa (2001-2003) kabla ya kujiunga na shule ya upili ya Ogande Girls, Homabay (2004-2007) kisha Chuo Kikuu cha Kenyatta (2009-2012).

Japo matamanio yake yalikuwa kusomea taaluma ya uanahabari, aliyemchochea kujitosa katika ulingo wa ualimu ni babaye mzazi ambaye kwa sasa ni mwalimu mkuu na mmiliki wa shule ya msingi ya Kemba Academy.

Kabla ya kufuzu chuoni, Anne alishiriki mafunzo ya nyanjani katika shule ya Likoni Boys, Kaunti ya Mombasa. Nafasi hiyo ilimpa jukwaa mwafaka la kuzima kiu ya ualimu na akaamsha ari ya kuthaminiwa kwa masomo ya Dini na Historia miongoni mwa wanafunzi.

Mbali na ualimu, Anne pia ni mwanamitindo, mjasiriamali na mtaalamu wa masuala ya fasheni na ulimbwende. Aliwahi kushiriki mashindano ya uanamitindo mnamo 2021 na akatawazwa Miss Universe Nyandarua baada ya kuwapiku washindani wengine 65.

Asipokuwa darasani, Anne hutumia ujuzi wake wa ualimu kuwaelekeza wasichana katika masuala ya maadili, namna ya kujikuza kisanaa kupitia fasheni za Kiafrika na jinsi ya kujitegemea na kukabili changamoto mbalimbali maishani.

Kwa kuibuka mshindi wa Miss Universe, alitwikwa majukumu ya kuwalea vijana kinidhamu na kuwafundisha ujuzi wa kuchangia maendeleo ya jamii kwa uzalendo na ukakamavu.

Aidha, anaendesha kampeni maalumu ya kusambaza sodo shuleni kupitia mpango wa Kenya Women Initiative Network (KWIN) ambao pia hutoa mafunzo ya afya ya uzazi kwa wanafunzi. Zaidi ya kuhakikisha kuwa mahudhurio ya wanafunzi wa kike shuleni yanaongezeka, azma yake pia ni kupigana na ukeketaji, ndoa za mapema na dhuluma dhidi ya wanawake.

Anne anajivunia kuwa kiini cha motisha inayotawala wanataaluma wengi ambao hutangamana naye katika ngazi na viwango tofauti katika sekta ya elimu na uanamitindo.

You can share this post!

Tiba rahisi za nyumbani kwa mzio wa ngozi na vipele

TAHARIRI: Serikali izidi kuweka hatua kuokoa waathiriwa wa...

T L