• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 6:55 AM
MWALIMU WA WIKI: Ni mwalimu afunzaye kwa kutumia nyimbo

MWALIMU WA WIKI: Ni mwalimu afunzaye kwa kutumia nyimbo

NA CHRIS ADUNGO

MATUMIZI ya nyimbo darasani hufanya wanafunzi kuelewa mambo haraka, huwaamshia hamu ya kujifunza dhana mpya na huwafanya kutosahau wanachofundishwa.

Haya ni kwa mujibu wa Bw Abel Nyaruri Okenye ambaye ni Mwalimu Mkuu katika shule ya msingi ya The Ark Junior iliyoko South ‘B’ jijini Nairobi.

Kwa mtazamo wake, nyimbo na vifaa mbalimbali vya kidijitali husisimua wanafunzi wa umri mdogo na kuchochea bongo zao kufanya kazi.

“Kuzoesha wanafunzi kutumia vyombo anuwai vya kiteknolojia huwapa fursa ya kufanya mambo kwa kujiamini zaidi. Nyimbo pia huwapa majukwaa ya kutambua na kutononoa vipaji vyao. Mawanda ya fikira zao hupanuka kwa wepesi na maarifa wanayoyachota kwa walimu na vitabuni huwachochea kuwa wavumbuzi,” anasema mwalimu huyu wa Kiswahili na somo la Jamii.

Abel alizaliwa 1990 katika kijiji cha Monga kilichoko Nyamaiya, Kaunti ya Nyamira. Ndiye kitinda mimba katika familia ya watoto sita wa Bw Yuvenalis Okenye na Bi Jane Nyanchama.

Alianza safari ya elimu katika shule ya msingi ya ELCK Bondeka, Nyamaiya (1996-2004) kabla ya kujiunga na shule ya upili ya Nyansabakwa Boys, Nyamira (2005-2008).

Baada ya kukamilisha KCSE, alipata kibarua cha kufundisha Nyansabakwa Boys na akaamsha ari ya kuthaminiwa kwa Kiswahili miongoni mwa wanafunzi.

Ndoto yake ya kusomea uanasheria ilizimika ghafla na akahiari kujiunga na Chuo cha Ualimu cha Egoji, Kaunti ya Meru (2010-2012). Alijiendeleza kitaaluma kwa kusomea shahada ya ualimu (Kiswahili/Historia) katika Chuo Kikuu cha Kenya Methodist (KeMU) kati ya 2015 na 2018.

Abel alifundisha katika shule ya msingi ya Consolata, Meru (2013-2014) kabla ya kuwa Mkuu wa Idara ya Kiswahili katika shule ya msingi ya Mary Immaculate iliyoko Nanyuki, Kaunti ya Laikipia (2015-2017).

Hadi alipohamia The Ark Junior School mnamo 2020, alikuwa Naibu Mwalimu Mkuu katika shule ya msingi ya Fadhili Junior, Nairobi (2017-2019).

Mbali na ualimu, Abel pia ni mshairi shupavu na mwimbaji stadi wa nyimbo za kizalendo. Kipaji cha kutunga na kughani mashairi kilianza kujikuza ndani yake akiwa mwanafunzi wa kidato cha pili.

Alijitosa rasmi katika fani ya muziki mwanzoni mwa 2020 baada ya janga la corona lililoingia humu nchini kusitisha shughuli za masomo kwa muda. Kufikia sasa, amefyatua vibao vinne – ‘Haya ni Maombi’, ‘Naipenda Kenya’, ‘Tuungane’ na ‘ Usinipite’ akitumia jina la kisanii, Abel The Blessed.

Zaidi ya kuwa mtunzi maarufu wa kazi bunilizi na kupanua wigo wake wa ujasiriamali, kubwa katika maazimio yake ni kusomea shahada za uzamili na uzamifu na kuwa mhadhiri wa Kiswahili katika vyuo vikuu mbalimbali duniani.

Abel anaistahi familia yake inayozidi kuiwekea taaluma yake thamani na mshabaha. Kwa pamoja na mkewe Bi Jackline Atancha, wamejaliwa mtoto Malaika Nyaruri.

Bi Jackline kwa sasa ni mwalimu wa Kiingereza na Fasihi katika shule ya upili ya Moi Equator Girls mjini Nanyuki.

  • Tags

You can share this post!

PAUKWA: Makopo adhihirisha ‘ukupigao hukufunza’

Brazil wala njama ya kufinya Korea Kusini

T L