• Nairobi
  • Last Updated February 26th, 2024 10:37 AM
Nafasi ya kilimo cha miti kugeuza Kenya kuwa Sweden

Nafasi ya kilimo cha miti kugeuza Kenya kuwa Sweden

Na SAMMY WAWERU

SWEDEN, taifa la Nordic lililoko Scandinavian Peninsula Kaskazini mwa Bara Uropa ni mojawapo ya nchi utakayotamani kuishi. 

Mataifa mengi ulimwenguni yakiendelea kulemewa na athari za mabadiliko ya tabianchi, Sweden haihisi makali hayo.

Kila mji au jiji, limezingirwa na msitu shukran za dhati kwa serikali ya nchi hiyo kufuatia sheria za uhifadhi wa mazingira zilizozinduliwa miaka 150 – 200 iliyopita.

Upanzi wa miti umekuwa mila ya wananchi, kanuni ikiwa kila mti unaokatwa lazima miwili ipandwe.

Ni mikakati ambayo imesaidia Sweden kufikia kiwango cha zaidi ya asilimia 70 ya misitu.

Balozi wa Sweden hapa Kenya, Mheshimiwa Caroline Vicini anasema taifa hilo limefanikiwa kuwa na misitu licha ya kustawi kwa sekta ya viwanda inayotegemea miti na mbao kwa kiwango kikuu, kufuatia sheria kali kuhifadhi mazingira.

Kando na mila kupanda miti, Caroline anasema ukumbatiaji misitu ya kibiashara umesaidia kuboresha na kuhifadhi mazingira.

“Nilikua katika familia ambayo baba alifanya kazi katika sekta ya msitu,” Balozi akumbuka.

Kulingana na mwakilishi huyu wa UNEP na UN-HABITAT, misitu ya kibiashara miti ina thamani.

Ni uwekezaji wa kudumu ambao umeweka Sweden katika ramani ya nchi zilizostawi kimaendeleo ulimwenguni, Caroline asisitiza.

Nyumba nyingi humo zimejengwa kwa miti na mbao iliyoongezwa thamani, yakiwemo majengo ya ghorofa.


Balozi wa Sweden hapa Kenya, Mheshimiwa Caroline Vicini. Picha / SAMMY WAWERU

Taswira ya makazi Sweden ni maridadi na ya kuvutia katikati ya misitu, Balozi Caroline akihimiza Kenya kukumbatia mkondo huo katika ujenzi wa nyumba.

“Majengo mengi Kenya na Afrika, yameundwa kwa saruji na vyuma, na si bora kwa mazingira. Ni mojawapo ya kiini cha gesi hatari,” aonya.

Akionyesha baadhi ya vitabu vyenye picha za miji Sweden, wakati wa mahojiano ya kipekee na Akilimali katika makazi yake rasmi Nairobi, taswira ya nchi hiyo inaweza kukushawishi kuhamia humo bila kusita.

Ikikadiriwa kuwa na idadi ya watu milioni 10 kwa mujibu wa data ya Worldometer la Shirika la Umoja wa Mataifa (UN), miji Sweden imezingirwa na misitu kubwa.

Ipo misitu inayomilikiwa na serikali, wananchi, kampuni za kibinafsi katika uwekezaji, Balozi Caroline akifichua makanisa yanamiliki idadi kubwa.

Kimsingi, vijana na kina mama wanahusishwa katika mpango kuhifadhi mazingira.

Wote wanaomiliki misitu, wamewekeza katika kilimo cha miti ya kibiashara, ambapo inapokomaa inavunwa na kutumika katika ujenzi, uongezaji thamani – kupitia sekta ya viwanda.

Ni kutokana na hilo, Sweden imeingia kwenye daftari la mataifa yanayouza miti, mbao na vifaa vilivyoongezwa thamani nje ya nchi hiyo, katika mataifa ya Bara Uropa, Nchi za Kati Uarabuni, Kaskazini Marekani, na zinginezo ulimwenguni ikiwemo Kenya.

Mpango na mkondo wa Sweden, unawezekana kuigwa Kenya?

Mheshimiwa Caroline, anakiri inawezekana ikizingatiwa kuwa kiwango kikubwa cha ardhi Kenya kimesalia tupu.

Karibu asilimia 80 inakadiriwa kuwa jangwa na nusu-jangwa (Asal), na Balozi huyu anasema mikakati maalum na sheria zikiwekwa kuhusu upanzi wa miti yenye thamani kibiashara kuna uwezekano kurejesha hadhi ya maeneo kame.

Hatua hiyo, kadhalika itasaidia kukabiliana na kero ya upungufu wa mvua.

“Upanzi wa miti hasa misitu iwe ya uwekezaji, utasaidia kuhifadhi mazingira,” asema.

Kulingana na Shirika la Huduma za Misitu Nchini (KFS), kiwango cha miti Kenya kimetimu asilimia 12.13, huku kile cha misitu kikipanda kutoka asilimia 5.9 (2018) hadi asilimia 8.83 (2022).

“Tumepiga hatua mbele kuhifadhi misitu, japo tusilegeze kamba,” asema Julius Kamau, Mhifadhi Mkuu wa Misitu KFS.

Afisa kutoka KFS akielezea jinsi ya kupanda miti. Picha / SAMMY WAWERU

Rais mstaafu, Uhuru Kenyatta akiwa mamlakani 2018 alipiga marufuku ukataji miti katika misitu ya umma, akizindua kampeni ya upanzi zaidi.

Mwaka uliopita, Rais wa sasa William Ruto aliweka shabaha nyingine kuafikia asilimia 30 kiwango cha miti kufikia 2032.

Kupitia afisi yake, Dkt Ruto alizindua mpango maalumu, Special Presidential Forestry and Rangeland Acceleration Program, unaoleta pamoja wahusika kutoka serikalini, sekta za kibinafsi na mashirika yasiyo ya kiserikali (NGO) kuwahi kiwango hicho.

Mpango huo aidha unanuwia kukuza miti bilioni 15, chini ya miaka 10 ijayo na Balozi Caroline anahimiza wadau kuwekeza katika misitu ya kibiashara.

Unakadiriwa utagharimu kima cha Sh600 bilioni.

“Uwe mpango unaojumuisha mavuno ya miti, kila baada ya miaka 15 hadi 20 itumike katika ujenzi na kufanikisha sekta ya viwanda,” ashauri Mwanadiplomasia huyu.

  • Tags

You can share this post!

Kenya yaweka hai matumaini ya kushinda raga ya Barthes...

Kizaazaa Eric Omondi apeleka maandamano Kisumu

T L