• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Naibu Rais: Nimeokoka na majina yangu kamili ni Geoffrey Rigathi Gachagua

Naibu Rais: Nimeokoka na majina yangu kamili ni Geoffrey Rigathi Gachagua

NA SAMMY WAWERU

NAIBU Rais wa sasa wa Kenya, wengi wanamjua kwa majina mawili pekee, ndiyo Rigathi Gachagua.

Ujasiri na ukakamavu wake kisiasa, umemvunia umaarufu kiasi cha kutundikwa majina ya utani Riggy G.

Kila anaposhika mikrofoni kuhutubia au kuzungumzia umma, Bw Gachagua hakosi kuporomosha neno au maneno mawili, matatu yatakayoacha ukivunjika mbavu.

Tangu, pamoja na bosi wake, Rais William Ruto watwae uongozi 2022, Gachagua hajakuwa mchache kukosoa serikali iliyowatungulia ya Rais mstaafu Uhuru Kenyatta.

Kilichozua ucheshi zaidi na wakati huohuo kushtua taifa, ni dai kuwa walirithi serikali ambayo haikuwa na chochote kwenye kapu la Hazina ya Kitaifa, akitetea matamshi yake kwamba walianzia chini kuendesha nchi.

Isitoshe, naibu rais amekuwa mkosoaji mkuu wa kinara wa Azimio la Umoja Bw Raila Odinga akihoji Handisheki kati yake na Rais mstaafu Kenyatta, akiwa mamlakani, Machi 2018 ilichangia kudorora kwa uchumi na kuhangaisha rais wa sasa, Dkt Ruto wakati huo akihudumu kama naibu wa rais.

Kufuatia kesi ya ufisadi na ubadhirifu wa mali ya umma (japo iliondolewa na Mkurugenzi Mkuu Mashtaka ya Umma kwa kile alisema ni kukosa ushahidi), Gachagua alidai aliandamwa kisiasa.

Kwa sasa, Bw Gachagua amezamia kuzima kero ya pombe haramu Mlima Kenya na dawa za kulevya, akiahidi kuwa oparesheni hiyo pia itaelekezwa sehemu zingine za nchi.

Katika mukhtadha huo, Mei 2023 kwenye mkutano na viongozi wa kisiasa Bonde la Ufa na wale wa usalama, naibu rais alisema endapo vita dhidi ya pombe haramu na mihadarati ndivyo vitamuondoa serikalini alisisitiza “Mama Rigathi ana boma na atanipokea nyumbani”.

Ameapa kuhakikisha kuzima kero ya pombe haramu Kenya, akisema lengo lake ni kuona kizazi chenye maaadili mema na msingi bora.

Wengi wakimjua kwa majina; Rigathi Gachagua pekee, na jina lake la kwanza je?

Jumatano, Juni 7, 2023 katika hafla ya maombi ya kitaifa Hoteli ya Kifahari ya Safaripark, Nairobi, naibu rais alifichua jina hilo.

“Wengi mnanijua kama Rigathi Gachagua, na leo acha niwafichulie jina la kwanza; Ninaitwa Geoffrey Rigathi Gachagua,” aliambia umati wa watu uliohudhuria maombi hayo yaliyoongozwa na Rais Ruto.

Kilichozua ucheshi zaidi, ni dai kuwa ameokoka.

“Mkitaka kuthitibisha ukweli, mke wangu ni mhubiri; Pasta Dorcas Gachagua,” alielezea.

Kabla kuwa naibu rais, Bw Gachagua alihudumu kama mbunge wa Mathira, Nyeri.

Ni mume na baba ya watoto wawili, aliyekuwa Gavana wa kwanza Kaunti ya Nyeri marehemu Nderitu Gachagua akiwa nduguye.

  • Tags

You can share this post!

Polisi wadaiwa kupalilia mbegu ya uhalifu jijini Nakuru

Messi ateua kuhamia Amerika kuchezea Inter Miami licha ya...

T L