• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
NDIVYO SIVYO: Tofauti ya maneno angalau na aghalabu

NDIVYO SIVYO: Tofauti ya maneno angalau na aghalabu

MARA nyingi, watu hujikuta wakilitumia neno ‘angalau’ katika muktadha wa ‘ingawa’ au ‘aghalabu’.

Maumbo yanayoelekea kufanana ya maneno haya yamkini ni chanzo cha utata huo. Neno ‘ingawa’ ni kiunganishi cha kutofautisha.

Vinapotumiwa katika sentensi, viunganishi vya kutofautisha huonyesha ukinzani katika mahusiano fulani au mtawalia wa mambo.

Hubainisha kuwa tukio fulani limeenda kinyume na jinsi watu walivyotarajia au jinsi linavyotarajiwa liwe.

Kwa hivyo, matukio yanayounganishwa na ‘ingawa’ sharti yaoneshe ukinzani. Isingalikuwa sahihi, kwa mfano, kukitumia kiunganishi hicho katika sentensi kama hii: *Ingawa aliamka mapema, alipata gari la kusafiria. Sentensi hii itachukuliwa kuwa sahihi iwapo magari ya kusafiria hayatarajiwi kuondoka mapema.

Neno ‘angalau’ linapotumiwa katika sentensi huibua dhana ya ‘kiasi au kiwango cha kuridhisha’. Mfano katika sentensi: Iwapo huna shilingi mia moja, basi nipe angalau hamsini. Kwa mujibu wa sentensi hii, kupewa shilingi hamsini ni afadhali badala ya kukosa kabisa. Hata hivyo, ni muhimu kufahamu kuwa si lazima neno angalau litumiwe katika sentensi yenye uhusiano wa aina mbili kama ule unaojitokeza katika sentensi ya hapo juu. Wakati mwingine, linaweza kutumiwa katika sentensi nyepesi kama hii: Angalau sasa tunaweza kupumua.

Neno ‘aghalabu’ nalo hutumiwa kuibua dhana ya ‘mara kwa mara’. Maneno ‘mara kwa mara’ hayana maana ya ‘siku zote’, ‘kila siku’ au ‘kila wakati’. Yanamaanisha kuwa kitendo hutokea zaidi ya mara moja au kwa kujirudiarudia. Alhasili, uzingatifu unahitajiwa wakati wa kuvitumia viunganishi vitatu tulivyovijadili.

You can share this post!

Serikali yapanga kuanza huduma za uchukuzi wa feri Lamu

Sakaja aahidi kuboresha hospitali ya Mama Lucy

T L