Na FAUSTINE NGILA
NINA imani kuwa iwapo kufikia sasa hujawahi kuelewa teknolojia ya blokcheni, leo utaelewa kwa kuwa jana uliathirika pakubwa kutokana na kukosa huduma ulizozoea za WhatsApp, Facebook na Instagram.
Naam, hukuweza kutuma picha, video au gumzo la vikundi vya WhatsApp ulivyozoea, hukuweza kuchangia kwenye mada katika kurasa za Facebook huku picha zako ulizotengea Instagram zikisalia kwa simu bile yeyote kuziona.
Najua ulipigia marafiki kadhaa kujua iwapo pia walikuwa na tatizo hilo, kabla ya mashirika ya Habari kukuarifu kuwa huduma zote za kampuni ya Facebook zilikuwa na kasoro.
Zilisalia kuzimwa kwa zaidi ya saa sita, na kurejea usiku wa manane huku ripoti ya gazeti la Fortune ikifichua kuwa kampuni hiyo ilipoteza takribani Sh11 bilioni kutokana na hali hiyo.
Hii imenichochea kufikiria kuhusu jinsi intaneti na kampuni za huduma za mitandao ya kijamii kama Facebook, Twitter, Google (YouTube), Microsoft (LinkedIn) na WeChat zinavyoweza kujiokoa kutokana na hali hii iwapo zitapanua akili na kufikiria kuhusu uwezo wa blokcheni.
Kimsingi, huduma za WhatsApp, Messenger, Instagram na Oculus zilipotea kwa kuwa huduma za mtandao wa Facebook zilitoweka.
Hii inamaanisha kuwa huduma hizo zinategema seva za Facebook, hali ambayo haifai katika nyakati hizi za Mageuzi ya Nne ya Viwanda (4IR).
Iwapo mitandao ya huduma za Facebook ingekuwa chini ya mfumo wa blokcheni, basi baada ya Facebook kupotea, ungeendelea tu kupiga gumzo kwenye WhatsApp, Instagram na Messenger.
Mnamo Januari, mkurugenzi mkuu mtendaji wa mtandao pinzani wa Twitter, Bw Jack Dorsey alitangaza kuwa kampuni yake inafadhili mradi wa kuhakikisha kuwa matumizi ya mitandao ya kijamii yanaendeshwa kwa blokcheni ambapo kila huduma inajitegemea na hivyo kuwapa wadukuzi ugumu wakati wananuia kuangusha huduma.
Mradi huo kwa jina BlueSky ni mfano wa jinsi wadau katika sekta ya teknolojia duniani wanavyofaa kuanza kuchukulia jambo hili kwa uzito kwa kuwa mustakabali wa matumizi ya huduma za intaneti uko kwenye mifumo isiyoweza kutatizwa.
Ikumbukwe kuwa kutokana na kupotea kwa huduma za Facebook jana usiku, biashara nyingi zilipoteza mapato, hali inayopunguza mapato ya mataifa pia.
Twitter ilipata matatizo pia.
Kukosa kutumia blokcheni kunamaanisha kuwa suluhu ambazo Facebook imejitahidi kuletea wateja wake wapatao zaidi ya bilioni tatu kama Facebook MarketPlace, WhatsApp for Business na Instagram zilisalia bila maana kwa saa sita.
Ukiangalia intaneti ya sasa, inahusu viungo vingi vilivyounganishwa pamoja, kumaamisha kiungo kimoja kikifeli basi vingine vingi vitafeli kwani vinategemeana.
Watafiti wa intaneti ya blokcheni wamekuwa mbioni kuunda mifumo ya kisasa, hasa kutokana na ukosefu wa usalama wa data ya sisi ya watumizi ambayo kampuni kubwa za teknolojia zimekuwa zikivuna kutoka kwa watumizi bila idhini na kujizolea mabilioni ya faida.
Tukio la kupotea kwa huduma za Facebook ni funzo kwa serikali zote duniani kuwa kuendelea kutegemea mifumo ya kikale ya huduma za mtandao kutatuponza siku moja.
Tumejionea mengi katika nyakati za kampeni za urais, tunakumbuka jinsi sakata ya Cambridge Analytica ilivyoanika uozo katika mauzo ya data za wateja na kubatilisha chaguo la wananchi.
Dunia isipobuni mikakati ya kulinda huduma za mitandaoni dhidi ya wadukuzi au kupotea, basi tutaendelea kutarajia huduma mbovu katika siku za usoni, na kupunguza imani iliyopo kuhusu manufaa ya teknolojia.