• Nairobi
  • Last Updated February 26th, 2024 10:30 AM
Niliteswa kama mbwa: Mwanamke asimulia ukatili wa kutisha akiwa mjakazi Saudi Arabia

Niliteswa kama mbwa: Mwanamke asimulia ukatili wa kutisha akiwa mjakazi Saudi Arabia

NA MERCY KOSKEI

Lucy Wanjiku, mwenye umri wa miaka 45 kutoka kijiji cha Ngodu, Njoro, Kaunti ya Nakuru, aliondoka Kenya kuelekea Saudi Arabia mnamo Juni 2021 akiwa na matumaini ya kusaidia familia yake.

Baada ya kukabiliwa na changamoto za kifedha, alitafuta fursa bora zaidi nje ya nchi, ili kumudu mahitaji ya watoto wake wawili, mmoja akiwa na ulemavu.

Lakini hakujua kwamba safari yake ingechukua mkondo tofauti, na kupelekea mateso, unyanyasaji na ukosefu wa mshahara.

Uamuzi wake wa kufanya kazi kama mfanyakazi wa nyumbani huko Riyadh, kwa mapato ya Sh29,000 kila mwezi, ulionekana kuwa mpango mzuri mwanzoni.

Hata hivyo, baada ya kufanya kazi kwa miezi miwili, mwajiri wake alibadilika, na kuanza mateso.

Lucy alivumilia mateso hayo licha ya mawasiliano na familia yake kukatwa na mwajiri wake.

Hali yake ilipozidi kuwa ngumu, Lucy alifikia mawakala huko Saudi Arabia, akitumai kuwa wataingilia kati na kumsaidia.

Mazungumzo kati ya wakala na mwajiri wake yalizaa makubaliano ya kulipwa mshahara, lakini baada ya miezi mitano malipo yalikoma, na hata kunyimwa chakula.

Kulingana na Lucy, akiwa Saudi Arabia, aliishi kwa mlo mmoja kwa siku licha ya kufanya kazi kwa masaa mengi.

Wakati fulani, mwajiri wake alitishia maisha yake. Jioni moja, alisikia mazungumzo kuhusu mipango ya kumuua na mwili wake kutupwa.

Kwa hofu, alikataa kufanya kazi, na kupelekea kufungiwa kwa chumba kimoja bila chakula kwa siku tatu.

Baadaye mwajiri wake alimhadaa kuwa angempeleka kwa ofisi ya wakala, lakini akaachwa msikitini kwa wiki moja.

Kwa bahati nzuri, aliokolewa na maafisa wa polisi ambao walimwezesha kurejea Kenya.

“Baada ya kufika uwanja wa ndege, wasamaria wema walinisaidia, walinilipa nauli ya basi kutoka Nairobi hadi Nakuru. Nina furaha nimerudi nyumbani. Sina cha kuonyesha kuwa nilifanya kazi Saudi Arabia, nimebaki na kumbukumbu ya niliyopitia mikononi mwa mwajiri wangu. Walichukua pesa zote nilizozifanyia kazi. Wanaotaka kwenda Saudi Arabia watafute tu ajira nyumbani hata kama wanalipwa pesa duni,” alisema.

Kwa sasa Lucy anaendelea kujenga upya maisha yake, akisaidiwa na ndugu zake.

Teresia Wambui, mamake Lucy, alielezea huzuni yake, akisema kuwa alimwona bintiye baada ya miaka mitatu na kufichua kuwa afya yake ilikua imedhorora.

Kwa sasa Bi Wambui anaomba serikali kuingilia kati na kumrejesha bintiye, Hannah Ruguru ambaye bado yuko Saudi Arabia.

Alisema kuwa mama huyo wa watoto wawili aliondoka kwenda Saudi Arabia mwaka 2014, na kufanya kazi kwa mwaka mmoja kabla ya kufukuzwa baada ya mwajiri wake  kumshutumu kuiba dhahabu.

Anasema Ruguru alilazimika kukimbilia kwa Wakenya wengine nchini Saudia ambapo anaishi bila kibali jambo ambalo linahatarisha maisha yake.

“Sitaki kufa kabla sijamuona binti yangu, sijamuona kwa miaka tisa sasa. Nimeachwa tu kuwatunza wajukuu wangu,” alisema mama huyo wa watoto watano mwenye umri wa miaka 78.

Hannah Ruguru mamake Lucy Wanjiku aliyedhulumiwa na mwajiri wake Saudi Arabia azungumza na wanahabari nyumbani kwao, Njoro, Kaunti ya Nakuru. Anataka watoto wake kurudi nyumbani na kutafuta kazi humu. PICHA|BONIFACE MWANGI
  • Tags

You can share this post!

Uasin Gishu sasa ndio kitovu cha wizi wa ardhi, ujio wa...

Muuzaji wa kuku anayefukuzana na ndoto kuwa wakili

T L