• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 11:55 AM
ODONGO: Wetang’ula atumie Matungu na Kabuchai kujifufua kisiasa

ODONGO: Wetang’ula atumie Matungu na Kabuchai kujifufua kisiasa

Na CECIL ODONGO

SENETA wa Bungoma Moses Wetang’ula anafaa kutumia chaguzi ndogo za Matungu na Kabuchai zitakazofanyika Machi 4 kuokoa umaarufu wake wa kisiasa na kukirejeshea chama cha Ford Kenya hadhi yake ya zamani.

Kiti cha Matungu kinachopatikana Kaunti ya Kakamega kilisalia wazi baada ya mauti ya aliyekuwa mbunge marehemu Justus Murunga wa ANC.

Kile cha Kabuchai nacho kipo wazi baada ya mauti ya marehemu James Lusweti Mukwe mwezi uliopita.

Mnamo 1992, Ford Kenya chini ya marehemu Jaramogi Oginga Odinga ilikuwa maarufu sana na ilikuwa na viti si haba katika uliokuwa mkoa Magharibi.

Hali ilikuwa vivyo hivyo kati ya 1994-2003 ambapo aliyekuwa Makamu wa Rais Michael Wamalwa alihakikisha chama hicho cha Simba kilikuwa na umaarufu mkubwa si tu Magharibi bali hata maeneo mengine nchini.

Hata hivyo, uongozi mbaya wa mbunge wa zamani wa Webuye Musikari Kombo aliyechukua usukani wa chama baada ya Bw Wamalwa na Bw Wetang’ula aliyempindua uongozini 2011, umezamisha umaarufu wa Ford Kenya, Magharibi na taifa zima.

Si uongo kuwa sasa Ford Kenya inahesabiwa kati ya vyama vidogo nchini. Kina wabunge sita pekee, wawakilishi wa wanawake wawili, Gavana moja na Seneta moja ambaye ni Bw Wetang’ula.

Kina wabunge Vincent Kemosi (Mugirango Magharibi) na Richard Onyonka wa Kitutu Chache Kusini ambao ndio pekee wanatoka nje ya kaunti za Bungoma na Trans Nzoia ambako chama kilishindia viti vingine.

Aidha umaarufu wa Bw Wetang’ula ulipungua sana baada yake kupokonywa wadhifa wa Kiuongozi wa Wachache mnamo 2018 na nafasi hiyo kutunukiwa Seneta wa Siaya James Orengo wa ODM.

Katika uchaguzi wa 2013, Bw Wetang’ula alikuwa na ushawishi mkubwa Magharibi mwa Kenya ndani ya Muungano wa CORD ambao pia ulimshirikisha Raila Odinga wa ODM na Kalonzo Musyoka wa Wiper.

Seneta huyo ambaye ni wakili alishawishi eneo hilo kumpuuza Kinara wa ANC Musalia Mudavadi aliyewania Urais na wakazi wengi wakampigia kura Bw Odinga ambaye alipeperusha bendera ya Muungano wa Cord.

Hata hivyo, kurejea kwa Bw Mudavadi katika kambi ya Bw Odinga mnamo 2017 kulionekana kumziba Bw Wetang’ula ikizingatiwa mbunge huyo wa zamani wa Sabatia ndiye sasa anatazamwa kama msemaji wa jamii ya Mulembe.

Ingawa hivyo, Bw Wetang’ula anafaa kuweka mikakati ili kushinda chaguzi ndogo za Kabuchai na Matungu ili kudhihirisha kuwa makali yake bado yapo katika siasa za kitaifa

Ford Kenya haifai kukosa kuwasilisha mwaniaji Matungu ili iungwe mkono na ANC Kabuchai kwa sababu ushindi Matungu utadhihirisha chama kinaimarika nje ya Bungoma na Trans Nzoia.

Hasa kiti cha Kabuchai kina umuhimu kwake kwa sababu ndiko eneobunge lake la nyumbani. Iwapo atakipoteza basi litakuwa pigo kubwa sana kwake ikizingatiwa tayari imetangaza kuwa analenga kuwania Urais mnamo 2022.

Pia ushindi Kabuchai na Matungu utampa Bw Wetang’ula udhabiti wa Ford Kenya ambayo kwa sasa inakumbwa na mzozo wa uongozi kati ya mirengo miwili tofauti.

Mbunge wa Kimilili Dkt Eseli Simiyu na mwenzake wa Kanduyi Wafula Wamunyinyi wamekuwa na uhasama mkubwa na Bw Wetang’ula kuhusu uongozi wa Ford Kenya.

Iwapo wawaniaji wanaovumishwa na Seneta huyo wa Bungoma watashinda chaguzi hizo, basi atakuwa amechukua udhibiti wa kisiasa wa chama na kuwafungia nje mrengo wa Dkt Eseli na Bw Wamunyinyi.

You can share this post!

Wanafunzi 110 walazimika kurudi nyumbani baada ya kukosa...

WARUI: Changamoto tele shule zikifunguliwa leo