• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 8:55 PM
JIPANGE KABLA UPANGWE: Ratiba ya asubuhi ndio silaha yako ya siri

JIPANGE KABLA UPANGWE: Ratiba ya asubuhi ndio silaha yako ya siri

NA MARGARET MAINA

[email protected]

NI muhimu uwe na ratiba ya asubuhi ambayo itakuongoza wewe na familia yako kuwa na mpangilio maalum kutoka wakati wa kuamka.

Kuunda ratiba ya asubuhi ni mojawapo ya mambo muhimu zaidi unayoweza kufanya kwa ajili ya nyumba yako ili pia shughuli za siku ziendeshwe kwa mpango.

Usiwe kama baadhi ya watu ambao huamka asubuhi wakihisi wanakabiliwa na shughuli nyingi kiasi cha kwamba wanakuwa na msongo wa mawazo.

Usianze siku kwa kuzima kengele ya saa mara moja, kukimbia mbio kuoga, kuwatupa watoto ndani ya gari wakiwa hawajavalia mabegi migongoni kisawasawa, na kukimbia kwenda kazini huku unatafakari kwamba nyumbani vitu haviko sawa kwa sababu umesahau au hili au lile.

Kufuata ratiba ya asubuhi si kuwa na seti ya sheria za kufuata au orodha ya kazi zisizowezekana kukamilika hiyo asubuhi yako ambayo tayari una shughuli nyingi. Unachotakiwa kufanya ni kutazama orodha na kujua ni nini hasa kinachohitajika kufanywa, badala ya kuuchosha ubongo wako kila siku na kisha kuishi na hisia hiyo ya kusumbua kwamba unasahau kitu. Gundua tu utaratibu ambao unakufaa.

Kwa mfano, unatakiwa kufanya mambo ya kimsingi kama vile kupika kiamsha kinywa, kupakia au kutayarisha chakula kitakacholiwa mchana au kuanzisha mashine ya kuosha vyombo. Vile vile ratiba itakusaidia kukumbuka kufanya kazi kama vile kuweka chupa za maji kwenye friji, kumwagilia maji kwenye mimea, au kulisha wanyama wa nyumbani kama paka na mbwa.

Unapozoea kufuata ratiba ya msingi ya asubuhi, unaweza kuongeza baadhi ya vitu vya ziada vitakavyokusaidia kuendelea na shughuli za nyumbani na kazi za nyumbani kama vile kutandika kitanda chako, kuosha nguo, kupangusa bafu, au kusafisha jikoni.

Hakikisha tu kwamba unaanza kidogo – kidogo sana – unapoongeza kazi za ziada kwenye orodha yako. Ongeza kazi moja au mbili kwa wakati mmoja.

Labda unataka kuanza siku yako kwa kusoma Neno la Mungu, kufanya mazoezi, kunywa maji ya chupa au kula kiamsha kinywa chenye afya. Kufanya shughuli hizo kwanza asubuhi ndiyo njia bora ya kuhakikisha unatenga muda kwa ajili ya mambo ambayo ni muhimu kwa afya yako ya kiakili, kimwili na kiroho.

Unaweza hata kuanza kutazamia nyakati hizo za asubuhi. Fikiria muda unaotumika kujitunza kama zawadi unayojipa.

Ukijipanga vizuri asubuhi unahisi kana kwamba una udhibiti wa mambo ya kimsingi, na familia yako inakywa na imani kwamba unaitunza vyema.

Kwa hivyo, kuunda ratiba ya asubuhi ambayo inakufaa wewe na familia yako kutafanya mabadiliko makubwa katika nyumba yako. Jaribu kuanzia leo.

  • Tags

You can share this post!

DJ Brownskin ataka afisa wa upelelezi akaangwe mahakamani...

Shahidi aeleza korti dili bandia ya kompyuta ilisukwa kwa...

T L