• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 7:55 PM
PAUKWA: Bobu amtoa kijasho Harara baraza la wazee

PAUKWA: Bobu amtoa kijasho Harara baraza la wazee

NA ENOCK NYARIKI

MBUZI wa Babu Nyakebagendi walikuwa wameshiba na kuning’iniza vitumbo vyao upande wa kulia na kushoto kama sogi kwenye mgongo wa punda.

Babu aliwapongeza wajukuu wake kwa kazi nzuri na kuwaambia wawafungie bandani. Mara Bwana Harara aliingia kiamboni huku akiyumbayumba.

“Mzee Nyakebagendi! Nyakebagendi, eeh?’’ Harara aliita kwa sauti ya juu.

Babu Nyakebagendi aliyekuwa akiota moto kwenye nyumba yake ya msonge alitoka nje ili kukutana na Harara.

“Kunani mzee mwenzangu?” babu alimwuliza.

Bwana Harara alisimama ghafla, akamtazama kwa kufumba jicho moja alivyozoea kufanya wakati wowote alipolewa kisha akasema kwa hasira: “Usinizeeshe mimi wala usinifunze Kiswahili! Viko wapi hivyo vijitu vyako viwili unavyoviita sijui Dovu na Pofu?”

“Unamaanisha wajukuu wangu, Dobu na Bobu?” Babu Nyakebagendi aliuliza.

“Mimi sitaki kujua kama ni Dofu na Bofu! ila swali langu ni moja: kwa nini waliwaingiza mbuzi kwenye shamba langu la mihindi wakayaharibu mahindi yangu?” Harara alikuja juu.

Bobu na Dobu waliokuwa wakimsaidia bibi yao kunyunyizia mboga maji bustanini walipoyasikia mashtaka ya Mzee Harara walikuja mbio ili kujitetea.

Harara alipowaona, aliuinua mkongojo wake mrefu na kuwashtua.

“Mzee Harara, sisi hatukuwaingiza mbuzi kwenye shamba lako. Tulikuwa tukiwachunga vilimani,’’ Bobu alijitetea.

“Waongo! Sema ukweli ama nivigote hivyo vichwa vyenu! Nyayo nilizoziona shambani ni za mbuzi wala si za ng’ombe au tembo!’’ Mzee Harara aliendelea kupinga.

Babu Nyakebagendi aliwageukia wajukuu wake na kuwaambia: “Dobu, Bobu, nenda mkamsaidie bibi yenu bustanini. Si vyema kubishana na watu wazima.’’

HADITHI ITAENDELEA

You can share this post!

Amerika yarai Ukraine izungumze na Urusi

Raila apinga sera za serikali ya Ruto

T L