• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 2:08 PM
PENZI LA KIJANJA: Valentino yabisha hodi huku mapenzi yakiyumba

PENZI LA KIJANJA: Valentino yabisha hodi huku mapenzi yakiyumba

NA BENSON MATHEKA

NI mwezi wa mapenzi na zimebaki siku tisa kuadhimisha Valentine’s Day, yaani siku ya wapendanao na baadhi ya watu – vidosho na mabarobaro – na hata wengine walio katika ndoa, wanasema wako fully booked kumaanisha wanamezewa mate na watu wengi wanaotaka kuwa nao siku hiyo.

Hii pia inaweza kumaanisha wako na wapenzi watakaojumuika nao siku hiyo na hawana nafasi ya wengine wanaoweza kuwa wanawamezea mate.

Valentino ni siku ya wapendanao, sio ya wanaomezeana mate ingawa imetumiwa na baadhi ya watu kuwaingiza boksi wanaowatamani kwa gharama nyingi sana.

Gharama hii huwa ya kuandaa miadi ya valentino katika mikahawa ya kifahari ambako wanatumia mamilioni kadhaa ya pesa kwa mapochopocho na zawadi wakitaka kudhihirisha wanavyowapenda wanaowatamani.

Kuna pia watu walio katika ndoa wanaotumia siku hii na mipango ya kando wakijua kwamba uhusiano wao ni haramu. Hii, kulingana na Padre Gabriel Osu, sio maana halisi ya siku ya wapendanao.

“Inatumiwa vibaya,” asema Osu kwenye makala yaliyosambazwa mtandaoni.

“Maana halisi ya valentino ni mapenzi ya kweli, ya dhati. Inapaswa kuwa siku nzuri ya wanaopendana na walio katika ndoa kukariri mapenzi na hisia zao za dhati kwa kila mmoja wao,” asema Osu.

Kulingana na Osu, kwa wale ambao hawajaoana, siku hii haipaswi kuwa ya kushiriki ufuska wanavyofanya wengi.

“Wanafaa kuonyesha upendo wa Mungu, sio ule wa kuchangamkiana kimwili,” asema padre huyo.

Wataalamu wa mahusiano ya mapenzi wanasema siku ya Valentino imegeuzwa kuwa ya kupima mapenzi ya mtu kwa mchumba wake kwa kutegemea zawadi anayoweza kumudu ilhali muhimu zaidi ni mtu kuwa tayari kujitolea kukuza uhusiano wake wa kimapenzi.

“Hii inajiri na kuwajibika kwingi. Inajiri na mabonde na milima kwa kuwa sio rahisi kutimiza ahadi na viapo vya ndoa. Hivyo basi, valentino ni siku muhimu ya kusisitizia mtu wako kwamba unampenda hata kama haujaweza kumtimizia matakwa na matarajio ya ndoa,” asema Osu.

Kinachofanya siku hii kukosa maana yake halisi ni ukosefu wa mapenzi ya dhati.

“Imetekwa na ufuska na uchu, imetekwa na tamaa, unapata mtu akinunia mpenzi wake kwa kukosa kumnunulia maua, zawadi na kutompeleka miadi siku ya wapendanao jambo linalotia doa uhusiano wao,” asema Ruth Kamau 36, mkazi wa Nairobi.

Kulingana na Osu, ukosefu wa mapenzi ya dhati umefanya ulimwenguni kukosa kitu cha thamani.

“Tunahitaji mapenzi ya dhati katika ulimwengu ili kuponya mioyo inayovunjika na kuyeyusha iliyo ngumu kama chuma,” asema.

  • Tags

You can share this post!

JUKWAA WAZI: Uhuru, Methu waelekezeana mishale kuhusu suala...

KIGODA CHA PWANI: Uamuzi wa mahakama utaunganisha viongozi...

T L