• Nairobi
  • Last Updated May 22nd, 2024 6:07 PM
Prof Kindiki: Rais Ruto hulala saa zisizozidi tatu, anawazia Kenya 

Prof Kindiki: Rais Ruto hulala saa zisizozidi tatu, anawazia Kenya 

Na SAMMY WAWERU 

WAZIRI wa Usalama wa Ndani Kithure Kindiki ameunga mkono kauli ya Rais William Ruto anayodai kuwa hapati usingizi kwa sababu anawazia jinsi ya kukomboa Kenya kutoka kwa hali mbaya kiuchumi. 

Wakati wa maadhimisho ya Madaraka Dei, Juni 1, 2023, Dkt Ruto alidai huwa hapati usingizi kwa ajili ya majukumu mengi kukuza nchi yanayomzingira.

Huku kauli hiyo ikizua kejeli miongoni mwa Wakenya, Waziri Kindiki Jumapili, Juni 4, 2023 alipiga jeki matamshi hayo akikiri rais hapati usingizi wa kutosha.

Prof Kindiki alisema Rais Ruto hulala saa chache mno, kwa sababu ya mawazo mengi kuboresha taifa.

“Mnaposema mimi silali ninaposhughulikia masuala ya usalama, kuna asiyelala. Rais,l hulala muda wa saa mbili hadi tatu pekee kwa sababu anawazia jinsi ya kukuza Kenya,” alisema Waziri.

Kindiki alitoa matamshi hayo akizungumza katika Kanisa la KAG, Sagana, Kirinyaga ambapo alialikwa kuhudhuria ibada ya misa.

Akipigia upatu serikali ya Kenya Kwanza inayoongozwa na Dkt Ruto, Kindiki alidai rais amejitolea mhanga kuhakikisha Kenya inakua.

“Ana nia njema ya nchi hii, na baada ya miaka mitano tutaona mabadiliko.”

Hata ingawa hakutangaza wazi wazi kuunga mkono Mswada tata wa Fedha 2023, matamshi yake yaliashiria ameutia kidole upitishwe.

Alionya mrengo wa upinzani kwa kutishia kuandaa maandamano kupinga mswada huo tata, akisema wahusika wanapaswa kutumia mkondo wa sheria.

“Mnaposkia upinzani ukipinga, hiyo ni kazi ya yake – upinzani,” alielezea Waziri, akionya kuhusu maandamano yenye vurugu.

Azimio la Umoja, limetishia endapo matakwa yake kuhusu Mswada wa Fedha 2023 hayataangaziwa, hautakuwa na budi ila kuitisha maandamano kote nchini.

Mswada huo unapendekeza nyongeza ya ushuru (VAT), na umevutia hisia mseto Wakenya wengi na mashirika mbalimbali wakiupinga.

Prof Kindiki hata hivyo alielezea imani yake kwa Rais William Ruto, akisema hataacha Kenya alipoipata aliporithi uongozi kutoka kwa mtangulizi wake Uhuru Kenyatta.

“Atakuwa kama hayati Rais Mzee Mwai Kibaki aliyepata nchi ikiwa chini na kuisukuma mbele.”

 

  • Tags

You can share this post!

Dj Brownskin akamatwa kwa kusaidia mkewe kujitia kitanzi  

Maisha yamenipiga chenga, Baha akiri akigeukia wafuasi wake...

T L