• Nairobi
  • Last Updated April 15th, 2024 2:15 PM
Raia kupoteza Azimio isipong’ata bungeni

Raia kupoteza Azimio isipong’ata bungeni

NA CHARLES WASONGA

MUUUNGANO wa Azimio la Umoja-One Kenya unakabiliwa na kibarua kikubwa cha kukosoa serikali ya Rais William Ruto wabunge na maseneta wanapotarajiwa kuanza rasmi vikao hivi karibuni.

Japo, kisheria, idadi ya wabunge wa muungano huo iko juu ikilinganishwa na wabunge wa Kenya Kwanza, idadi hiyo ilipungua juzi baada ya baadhi yao kuamua kuegemea mrengo wa Kenya Kwanza.Azimio ina wabunge 174 huku Kenya Kwanza ikiwa na wabunge 162.

Lakini karibu wabunge 14 waliochaguliwa kwa tiketi ya vyama tanzu vya Azimio “walihamia” Kenya Kwanza baada ya Dkt Ruto kutangazwa mshindi katika kinyang’anyiro cha urais.

Aidha, 10 kati ya wabunge huru 12 walitangaza kuwa wataegemea mrengo huo unaoongozwa na Rais Ruto.

Kufuatia hatua hiyo, mrengo huo unaoongozwa na Dkt Ruto uliweza kushindi viti vya uspika wa bunge la kitaifa na seneti kwa urahisi mno katika shughuli iliyoendeshwa wiki moja iliyopita.

Aliyekuwa Seneta wa Bungoma Moses Wetang’ula, ambaye ni kiongozi wa Ford Kenya sasa ndiye Spika wa Bunge la Kitaifa huku aliyekuwa Gavana wa Kilifi Amason Jeffa Kingi, akiwa ndiye Spika wa Seneti.

Manaibu wao Bi Glady Shollei (Mbunge Mwakilishi wa Uasin Gishu) na Kathuri Murungi (Seneta wa Meru), mtawalia.

Wadadisi wa masuala ya kisiasa sasa wanasema kuwa hatua ya Rais Ruto kufaulu kudhibiti Bunge la Kitaifa na Seneti kwa kunyakua baadhi ya wabunge wa Azimio italemaza ushawishi wa upinzani ndani na nje ya bunge.

“Ingawa kisheria, Azimio ina idadi kubwa ya wabunge katika Bunge la Kitaifa, hatua ya Rais Ruto kuvutia baadhi ya wabunge wake imedhoofisha uwezo katika asasi hiyo. Japo Raila amewashauri wabunge wa Azimio wadumishe umoja, hilo halitawezekana kwani ushawishi wa Ikulu ni mzito zaidi na umewahi kuonekana hata katika serikali ya Uhuru Kenyatta,” anasema Bw Mark Mwita, ambaye ni mchanganuzi wa masuala ya kisiasa.

“Kimsingi, wabunge wa Azimio wanapaswa kutekeleza wajibu wao wa kukosoa serikali ili iweze kuwajibika kwa wananchini. Lakini hilo halitawezekana katika bunge hili (sawa na ilivyokuwa katika bunge la 12) kwa sababu wabunge ni wepesi wa kuweka masilahi yao mbele ya yale ya wanananchi wa kawaida,” anaongeza Bw Mwita, ambaye ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Rongo.

Kwa upande wake, wakili Martin Oloo anasema hakuna uwezekano kwamba Azimio itajisuka upya na kuwa upinzani thabiti.

“Baada ya kushindwa katika kinyang’anyiro cha urais, Azimio haitakuwa na rasilimali na nguvu ya kuiwezesha kudumisha umoja miongoni mwa vyama tanzu na viongozi wake. Kuna uwezekano kuwa changamoto zilizoandama uliokuwa muungano wa Nasa, huenda ukajitokeza tena na kuchangia kusambaratika kwa Azimio,” anasema Bw Oloo, ambaye pia ni mchanganuzi wa masuala ya kisiasa.

Anasema Rais Ruto yuko katika nafasi nzuri ya kutumia rasilimali za umma, vyombo vya dola na mamlaka ya afisi yake kuvuruga kabisa jaribio lolote la Azimio kuvuruga ajenda zake serikali ndani na nje ya bunge.

“Isitoshe, Katiba ya sasa haijatenga nafasi ya Afisi ya Kiongozi wa Upinzani ambayo itatengewa fedha kutoka kwa bajeti ya kitaifa. Hii ina maana kuwa Azimio haitaweza kuunda baraza la mawaziri la pembeni (shadow cabinet) ambalo litahakiki utendakazi wa mawaziri watakaoteuliwa na Rais Ruto,” anaongeza Bw Oloo.

Afisi hiyo ya Kiongozi Rasmi wa Upinzani ilipendekezwa katika Mswada wa Marekebisho ya Katiba kupitia mpango wa maridhiano (BBI) lakini mchakato huo ukazimwa na mahakama mnamo Septemba 2021.

Licha ya uwepo wa wasiwasi kuhusu uwezo wa Azimio wa kuhakiki ipasavyo utendakazi wa serikali ya Kenya Kwanza, Raila Odinga ameshikilia kuwa muungano huo utasalia thabiti na kutumia wabunge wake kutetea masilahi ya raia.

Akiongea Ijumaa katika mkutano wa kundi la wabunge wa Azimio (PG), Waziri Mkuu huyo wa zamani aliwahimiza kudumisha umoja wao na kukinga jaribio lolote “la kugawanywa na Serikali Kuu.”

“Ikiwa hamtashikana pamoja kama wabunge na kukosoa serikali ndani na nje ya bunge wizi wa mali ya umma utaendelea. Tayari mwaweza kuona kuwa wameanza kufuja na kuiba mali ya umma,” Bw Odinga akawaambia wabunge wa Azimio katika mkahawa wa Stoni Athi, Machakos.

Huku akiendelea kukosoa uamuzi wa Mahakama ya Upeo, ulioidhinisha ushindi wa Dkt Ruto, Bw Odinga alisema muungano huo unapanga kuwasilisha mswada wa kufanyia marekebisha Idara ya Mahakama na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

“Kama Azimio, tunataka kukinga asasi hizo dhidi ya kuwekwa mateka na Ikulu. Nyote mwaona kuwa utendakazi wa IEBC na Idara ya Mahakama sio wa kuridhisha. Kwa mfano, juzi walitupokonya ushindi katika uchaguzi uliopita,” Bw Odinga akasema.

Mtihani wa kwanza wa Azimio bunge utakuwa hoja ya kuwafuta kazi makamishna wanne walimkaidi mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati kwa kupuuzilia mbali matokeo ya urais aliyotangaza mnamo Agosti 15 katika ukumbi wa Bomas.

Hoja hiyo imedhaminiwa na kiongozi wa chama cha Farmers Party Irungu Nyakera, ambaye ni mmoja wa viongozi wakuu katika muungano wa Kenya Kwanza.

Makamishna hao ni; Naibu Mwenyekiti Juliana Cherera, Justus Nyang’aya, Irene Masit na Francis Wanderi ambao waliondoka Bomas na kukataa kutambua ushindi wa Rais Ruto.

  • Tags

You can share this post!

FATAKI: Sharti kuwe na mipaka katika utekelezaji wa majukumu

JUNGU KUU: Rigathi, Mudavadi wazozania wizara

T L