• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 6:45 PM
Rais apuuza itifaki za kijeshi na kuamuru waliofungiwa nje ya uwanja waruhusiwe kuingia

Rais apuuza itifaki za kijeshi na kuamuru waliofungiwa nje ya uwanja waruhusiwe kuingia

NA SAMMY WAWERU

RAIS William Ruto Alhamisi, Juni 1, 2023 alipuuza itifaki za kijeshi kuhusu hafla za kitaifa, ambapo baada ya kiongozi wa nchi kuingia ukumbini hakuna yeyote anayeruhusiwa kumfuata.

Katika maadhimisho ya Madaraka Dei 2023, yaliyofanyika Kaunti ya Embu, Dkt Ruto kabla kualika baadhi ya wageni mashuhuri kuzungumza na kutoa rasmi hotuba yake, aliagiza wananchi waliofungiwa nje ya uwanja wa Moi waruhusiwe kuingia.

Sikukuu ya Madaraka, huadhimishwa kila mwaka na Rais Ruto alisema ni haki ya Wakenya wote kusherehekea siku ambayo Kenya ilipata uhuru wa ndani kwa ndani kujitawala kutoka kwa mbeberu.

“Tafadhali hiyo milango ifunguliwe, watu ni wengi huko nje waruhusiwe kuingia waadhimishe siku hii maalum na ya kipekee nchi kupata uhuru wa ndani kwa ndani kujitala,” Rais Ruto aliamuru.

Alichukua dakika kadhaa kuhakikisha waliofungiwa nje wameingia.

Baadhi walioonekana wakirukia uani na kutani.

Akiwa ndiye Amiri Jeshi Mkuu Kenya, baada ya kuingia milango ya ukumbi au uwanja ambapo hafla ama sherehe inafanyika hufungwa.

Hilo ni kwa mujibu wa mila, tamaduni na itifaki za kijeshi (KDF) kwa minajili ya usalama.

Wakenya kutoka maeneo mbalimbali nchini, waliungana na Rais Ruto kuadhimisha Madaraka Dei, Juni 1, 2023 katika Uwanja wa Moi, Embu.

Baadhi, walikiri kwa vyombo vya habari kwamba waliwasili saa nane usiku wa kuamkia Juni 1, usalama ukiimarishwa ndani na nje ya uga huo.

 

 

  • Tags

You can share this post!

Wasioonyesha uzalendo kuadhibiwa nchini Zimbabwe

Msitilie shaka Ada ya Ujenzi wa Nyumba, Rais awasihi Wakenya

T L