• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 6:25 PM
RIWAYA: Kielelezo cha swali la dondoo na namna ya kulijibu mtihanini

RIWAYA: Kielelezo cha swali la dondoo na namna ya kulijibu mtihanini

JUMA hili tutarejelea swali la dondoo.

Dondoo hurejelea msemaji wa maneno fulani, msemewa, mahali walipo na msemewa na chanzo cha kauli husika.

Mfano: “…wewe hujui kwamba umaskini unaweza kuupujua utu wa mtu, akatenda hata asiyoyakusudia kutenda?”

(i) Eleza muktadha wa dondoo hili

Msemaji ni Kimondo. Anajisemea/anajizungumzia, wakiwa shuleni baada ya Kimondo kusikiliza hotuba ya Lunga kuhusu uhifadhi wa mazingira.

(ii) Onyesha jinsi umaskini unavyoweza kuupujua utu wa mtu, akatenda hata asiyokusudia kutenda, ukirejelea riwaya yote.

Lunga Kiriri-Kangata anaporudi kwao (msitu wa Mamba) baada ya kufutwa kazi; alidhamiria kumtoa babake msituni, ila anapofika huko,anakuwa miongoni mwa watu wanaokata miti ili afanye kilimo. Kinyume na mawazo yake ya awali ya kuyaifadhi mazingira.

Hazina hakuwa na makazi wala walezi. Umaskini unamsukumiza kuwa ombaomba na kulala mitaani ili kukidhi mahitaji yake.

Baada ya madhila na kadhia alizofanyiwa Sauna na Bwana Maya pamoja na mamake, Sauna anauza maji ghushi, kufanya kazi katika machimbo na kulangua watoto ili kujikimu kimaisha.

Daktari Ridhaa anapojipata katika kambi ya wakimbizi katika msitu wa Mamba, anakuwa mtegemezi. Umaskini unamlazimisha kung’ang’ania chakula na kula mizizi mwitu.

Madhila anayopitia Pete ya kuozwa kwa lazima na baadaye kutalikiana na Mzee Fungo, yanamfanya maskini. Ili kujikimu kimaisha anajihusisha na kazi duni za kudhalilisha. Anajaribu kuavya mimba na kujiua ili kuepuka maisha ya kimaskini. Aidha, umaskini wa mamake Pete, unamfanya kukosa kumthamini Pete, anamwoza ili apate pesa za kuwasomesha watoto wake wa kiume, hata kama ni kinyume na haki ya Pete.

Shamsi alipofutwa kazi na kuona jinsi babake anavyoaga dunia kwa kunyang’anywa shamba, anaingilia ulevi ambao unamwacha mtegemezi.

Baada ya Lunga Kiriri- Kangata kuhamishwa kutoka msitu wa Mamba na kuhamia Mlima wa Simba, uhitaji unamfanya Naomi kumwacha mumewe na kuwatoroka watoto wake. Anamjuza mumewe kuwa angependa kutamba na ulimwengu na akifanikiwa angerudi kumsaidia.

Vijana katika chuo kikuu wametamauka kwa sababu ya hali ngumu ya maisha. Ili kujiliwaza, wanajiingiza katika ulevi. Baadhi ya vijana waliosoma, kwa sababu ya umaskini na ukosefu wa kazi – wanatumiwa na viongozi kuzua rabsha baada ya uchaguzi. Kijana aliyevaa shati lililoandikwa Hitman anajihusisha na uharibifu wa mali na ulaghai wa kuwadanganya wapiga kura kuhusu yupi wa kumpigia kura.

Diwani Kute aliigawa familia yake mara tatu ili apate chakula kingi kuonyesha tamaa inavyopujua utu wa mtu.

Swali la tathmini: Jadili sifa na umuhimu wa msemaji wa maneno haya.

 

Joyce Nekesa

Kapsabet Boys High School

  • Tags

You can share this post!

GWIJI WA WIKI: Kelsy Kerubo

Mkenya aliyetumia ujanja kujaribu kuenda Canada atozwa...

T L