• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Ruto anavyomfufua Uhuru kisiasa

Ruto anavyomfufua Uhuru kisiasa

NA WANDERI KAMAU

HATUA ya serikali ya Rais William Ruto kumpunguzia walinzi Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta na baadhi ya waliokuwa mawaziri wake wa karibu, imetajwa kuwa kama hatua itakayompunguzia umaarufu wake wa kisiasa katika ukanda wa Mlima Kenya.

Baadhi ya watu ambao wameathiriwa na ‘mabadiliko’ hayo ya kiusalama ni aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i na Katibu katika wizara hiyo, Dkt Karanja Kibicho.

Ijapokuwa Inspekta Jenerali wa Polisi Japheth Koome ametaja hatua hiyo kama “mageuzi ya kawaida ya kiusalama”, wadadisi wanataja mwelekeo huo kama utakaomwathiri sana Rais Ruto kisiasa katika ukanda wa Mlima Kenya, kwani ataonekana kama analipiza kisasi.

Wadadisi wanasema kupitia hatua hiyo, Rais Ruto atakuwa akiufufua tena umaarufu wa Bw Kenyatta katika ukanda huo, kwani wenyeji watamgeuka kwa kuonekana “kumlenga” mmoja wao.

“Kilicho dhahiri ni kuwa wenyeji wa Mlima Kenya bado wanamheshimu Uhuru kama kiongozi wa kisiasa. Bado ana ufuasi wake. Huenda isiwe nadra wafuasi hao wachache kuamka na kuasha moto wa kisiasa kwamba Rais Ruto analenga kumwangamiza Bw Kenyatta, hivyo si vigumu kwao kuwageuka,” asema Bw Kipkorir Mutai, ambaye ni mchanganuzi wa siasa za ukanda huo.

Licha ya serikali kujitetea kuhusu hatua hiyo kama “utaratibu wa kawaida wa kiusalama”, wadadisi wanasema kuwa machoni mwa raia, hilo linaonekana kuwa kisasi, kwani Rais Ruto alipitia yayo hayo mwaka uliopita alipokuwa akihudumu kama Naibu Rais.

Wengine wanataja hilo kama “onyo” la mapema kwa ukanda huo, kwamba si rahisi likaanza kutengwa kisiasa na Rais Ruto ielekeapo 2027.

Wanasema kuwa taswira hii inajirudia kama ilivyokuwa kati ya 1978 na 1982, wakati Rais Mstaafu (marehemu) Daniel Moi alichukua uongozi kutoka kwa Mzee Kenyatta na kuahidi kudumisha urafiki na baadhi ya vigogo wa kisiasa waliokuwa washirika wa karibu wa Mzee Kenyatta.

Baadhi ya wanasiasa hao ni marehemu Geoffrey Gitahi Kariuki (GG), Charles Njonjo kati ya wengine.

“Baada ya Moi kuchukua uongozi, aliendelea kudumisha ukaribu na vigogo hao. Hata hivyo, mambo yalibadilika baada ya jaribio la mapinduzi mnamo 1982, wakati Moi aliwatuhumu baadhi ya viongozi hao kuwa wapangaji wakuu wa jaribio hilo. Huo ndio ulikuwa mwanzo wa Moi kuwatenga viongozi hao pamoja na eneo hilo kisiasa na kiuchumi kwa karibu miaka 24 ya uongozi wake,” asema Bw Mutai.

Vivyo hivyo, anasema kuwa si vigumu Rais Ruto kuanza harakati za kulipiza kisasi dhidi ya “mateso” aliyoelekezwa na Rais Kenyatta kwa kumlenga yeye binafsi na familia yake, na baadaye kuelekeza mishale yake kwa wenyeji.

Hata hivyo, wadadisi wanataja mwelekeo huo kama “kosa la kisiasa” ambalo huenda likamfufua upya kisiasa Bw Kenyatta, kwani ataonekana “kuteswa” kwa niaba ya ukanda huo.

“Wenyeji wa Mlima Kenya wana historia ya kusimama na kuwaunga mkono viongozi wao, hasa ikionekana kama wanaelekezwa vita na serikali. Ndivyo walivyowaunga mkono mwanasiasa Kenneth Matiba na Mwai Kibaki ilipoibuka walikuwa wakipigwa vita vya kisiasa na utawala wa Moi. Vivyo hivyo, walimuunga mkono Bw Kenyatta aliposhtakiwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kutokana na ghasia zilizotokea baada ya uchaguzi tata wa 2007/2008. Hivyo, si vigumu kwao kuanza kumuunga tena Uhuru ikiwa ataonekana kuhangaishwa na utawala wa Ruto,” asema Prof Ngugi Njoroge, ambaye ni mchanganuzi wa siasa.

Kulingana naye, mwelekeo anaochukua Ruto ni ‘kosa’ la kisiasa, litakalompa umaarufu tena Uhuru Mlimani.

  • Tags

You can share this post!

Korti yakataa ombi la kukagua kura za ugavana

JUNGU KUU: Vita vya Uhuru na Ruto kufaidi Raila

T L