• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 8:55 AM
Ruto na Gachagua: Tutawachukulia hatua kali wabunge wanaopinga Mswada wa Fedha 2023  

Ruto na Gachagua: Tutawachukulia hatua kali wabunge wanaopinga Mswada wa Fedha 2023  

Na MWANDISHI WETU

RAIS William Ruto na naibu wake Rigathi Gachagua waliapa kuwachukulia hatua kali wabunge watakaopinga Mswada wa Fedha wa 2023.

Akizungumza katika hafla ya kufurahia uteuzi wa Waziri wa Mazingira Soipan Tuya katika Kaunti ya Narok, Rais Ruto alisema kuwa uchaguzi wa kupitisha au kukataa mswada huo utakuwa wazi.

Isitoshe, alieleza kuwa njia hiyo itawasaidia Wakenya kujua ni viongozi gani ambao hawataki kusaidia vijana nchini kupata njia za kujitafutia mapato ilhali walichaguliwa kufanya hivyo.

“Viongozi wengi wamechukua rehani (mortgages) kutoka kwa ushuru unaolipwa na Wakenya. Mbona muwanyime vijana fursa kama yenu? Si haki yetu kuwajua wale watakaopinga mswada huo?” akauliza.

“Wale wanaokataa mswada huo ninasubiri sana kusikia sababu zao za kupinga.”

Aliwaonya wabunge dhidi ya kutojipenda na kutaka kufanikisha malengo yao binafsi bila ya kufikiria Wakenya.

Kwa upande wake naibu Gachagua, wabunge watakaopinga mswada huo watanyimwa fedha za kuendeleza eneo bunge zao.

“Nilikuwa Kitui jana na mbunge wa huko alipinga sana mswada huu wa fedha huku watu wakimshabikia. Baadaye akanieleza kuwa wakazi wanahitaji barabara, sasa mnataka nitoe wapi pesa za kujenga barabara?

“Viongozi wengine hapa mnawadanganya Wakenya lakini mjue kuwa mkikataa mswada huu basi msije kuniitisha barabara,” akaonya.

  • Tags

You can share this post!

Mishi Dorah atoka soko, si ‘singo’ tena

Njugush: Kuna wakati nilisafiri nje ya nchi kuwachekesha...

T L