NA WANDERI KAMAU
NAIBU Rais Rigathi Gachagua sasa ameanza kufuata nyayo za Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta kuandaa vikao vya Sagana katika Ikulu Ndogo ya Sagana, Kaunti ya Nyeri, kwenye juhudi za kuliunganisha eneo la Mlima Kenya.
Kulingana na Bw Gachagua, vikao hivyo vitakuwa njia atakayotumia kujadiliana na wananchi kutathmini pale serikali imefikia katika kutekeleza ahadi zake kwao na kuimarisha umoja wa kisiasa.
Kwenye mahojiano na kituo cha televisheni cha Inooro, Jumapili iliyopita, Bw Gachagua alisema vikao hivyo vitawashirikisha viongozi wa kisiasa, wazee, wakulima na wadau wengine, ambapo watakuwa huru kutoa hisia zao kuhusu mwelekeo wa kiuchumi na kisiasa katika ukanda huo.
“Tunataka kuhakikisha tunawapa wananchi uhuru wa kuamua mwelekeo wa kisiasa na kiuchumi ambao wangetaka eneo hili kuchukua. Sitaki kutoa maagizo kwao bila kuwashirikisha ifaavyo,” akasema Bw Gachagua.
Alisema kuwa kikao cha Sagana I kitafanyika mara tu baada ya serikali ya Kenya Kwanza kuanza utendakazi wake.
Kufuatia tangazo hilo, wadadisi wanasema Bw Gachagua analenga kutumia mbinu zilizotumiwa na Bw Kenyatta kuliunganisha eneo hilo, kila wakati alihisi kuna jambo alilotaka “kuieleza jamii”.
Duru zinasema kuwa kuna uwezekano kauli ya Bw Gachagua imesukumwa na juhudi ambazo zimekuwa zikiendeshwa na baadhi ya wazee kutoka jamii ya Agikuyu, kumtaka kiongozi huyo, Rais William Ruto na Bw Kenyatta kufanya handisheki ili kuondoa uhasama wa kisiasa ambao umekuwepo tangu Bw Kenyatta alipobuni urafiki wa kisiasa na kiongozi wa Azimio, Bw Raila Odinga.
Juhudi hizo zilianzishwa wiki iliyopita na Baraza la Wazee wa Agikuyu (KCE) katika Uwanja wa Ol Kalou, Kaunti ya Nyandarua.
Kulingana na wazee waliohutubu, wengi walimpendekeza Bw Gachagua kuwa kiongozi wa juhudi hizo za upatanishi.
Akihutubu wakati wa hafla hiyo, mwenyekiti wa baraza hilo, Bw Wachira Kiago, alisema wakati umefika kwa vigogo hao wawili kurejesha urafiki uliokuwepo baina yao kwa manufaa na ufanisi wa nchi yote kwa jumla, hasa ukanda wa Mlima Kenya.
“Ni jukumu letu kama viongozi kuziunganisha jamii mbalimbali nchini. Tunapoanza Mwaka Mpya, jukumu letu la kwanza litakuwa kuwaunganisha Bw Kenyatta na Rais Ruto,” akasema Bw Kiago.
Licha ya wazee hao kumtwika Bw Gachagua jukumu hilo, walisema ni lazima asuluhishe tofauti zake na Bw Kenyatta “ili kupata baraka za uongozi wa kisiasa na kuwa msemaji wa Mlima Kenya”.
Chama kingine cha wazee, Kiama Kia Ma (Chama cha Ukweli), pia kilieleza kuunga mkono juhudi hizo.
Kulingana na mwenyekiti wake, Bw Ndung’u Gaithuma, usuluhishaji wa tofauti zote za kisiasa zilizopo utakuwa hatua ya kwanza kuliunganisha eneo hilo, hivyo kumpa Bw Gachagua mazingira mazuri kuendesha mikakati ya kisiasa na kiuchumi.
“Chini ya uwepo wa mazingira tulivu ya kisiasa, hilo litampa Bw Gachagua na viongozi wengine nafasi nzuri kuendeleza mikakati ya kutetea maslahi ya eneo hilo,” akasema.
Wachanganuzi wanasema kuwa Bw Gachagua anafaa kuzingatia pendekezo la wazee kusuluhisha tofauti zake na Bw Kenyatta, kwani hilo “litampa baraka wa kisiasa atakapoanzisha vikao vya Sagana.”
“Bw Kenyatta ndiye aliyeanzisha vikao vya Sagana. Kiafrika, ndiye bado ‘mmiliki’ wa Ikulu ya Sagana na anahitaji kutoa “baraka” kwa yeyote atakayechukua urithi wake. Hivyo, kitakachongojewa ni kuona ikiwa Bw Gachagua atazingatia ushauri wa wazee kwa kubuni handisheki na Bw Kenyatta kabla ya kuanza kuandaa vikao hivyo,” asema mdadisi wa siasa Kipkorir Mutai.
Subscribe our newsletter to stay updated