• Nairobi
  • Last Updated February 23rd, 2024 12:48 PM
Sarakasi za Akothee Ufaransa akizuiwa kutumia majanichai ya Kenya

Sarakasi za Akothee Ufaransa akizuiwa kutumia majanichai ya Kenya

NA MERCY KOSKEI

MWANAMUZIKI Esther Akoth ‘Akothee’ alishangaza wengi baada ya kufika katika mkahawa mmoja nchini Ufaransa na kutaka kutumia majanichai ya Kenya.

Hata hivyo, wahudumu wa mkahawa huo walimzuia jambo ambalo lilimkasirisha Akothee akisema kuwa ana uzoefu wa chai ya Kikenya.

Kupitia mtandao wake wa Instagram, Akothee ambaye alikuwa na mwanawe alisema kuwa alikuwa tayari kufurahia kikombe cha chai wakati mhudumu alipokaribia meza yao na kumtaka asitumie ‘tea bag’.

“Wewe Bwana una tatizo gani? Nitanunua chai lakini pia nitakunywa majani yangu kutoka Kenya. Ninapokunywa chai ya Ufaransa kichwa huniuma. Chai yako ni pesa ngapi nitalipa na pia nilipe maji moto mtakayonipa muradi tu ninywe chai ya Kikenya,” mama huyo wa watoto watano alisikika akisema.

Hata hivyo, binti yake Fancy Makadai alimwambia kuwa alipaswa kufuata sheria ya mkahawa huo ili kuepuka mambo mengi, akinukuu; “Unapokwenda Roma, fanya yale ambayo Warumi hufanya.”

“Ili kuepuka matatizo, ukienda Ugiriki, unafanya kile watu wa Ugiriki hufanya. Kwa vile tuko nchi ya wenyewe na hatuko Kenya, ukitaka kuepuka ubaguzi wa rangi na yote yanayoambatana nayo usijiweke katika hali ambayo utakabiliwa,” alishauri Makadia

Mwimbaji huyo hata hivyo alikasirishwa na matukio hayo na kusema kwamba hawezi taka kuishi Ulaya kwa sababu kama hizo.

Fancy alijaribu kumtuliza mamake, huku akimshauri ingekuwa busara endapo angeacha tabia fulani za Kikenya.

“Nadhani unaweza, kuna mambo utafanya ukiwa nyumbani ambayo huwezi kufanya hapa. Mhudumu amekueleza kuwa kubeba chakula chako na kuja mkahawani ni kama kuleta nyama yako mwenyewe, jambo ambalo haliruhusiwi,” aliongeza Fancy.

Akionekana kupandwa na mori, Akothee aliendelea kutumia begi la chai na kusisitiza kwamba yeyote anayetaka kuwaita polisi afanye hivyo.

Kulingana naye, kubeba begi la chai hadi kwenye mkahawa sio uhalifu.

Katika tetesi zake, alisema kuwa wakati wowote wazungu wanapotembea Kenya hubeba vitu vyao wenyewe, kuanzia kwa sigara na bidhaa zingine na hivyo hawapaswi kumhukumu.

 

  • Tags

You can share this post!

Dadake Betty Kyalo aajiri mtunzi wa watoto wa mbwa wake

Kiongozi wa zamani wa Mungiki mafichoni akisakwa na DCI

T L