• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 7:55 AM
SHINA LA UHAI: Selimundu huua watoto 10,000 nchini Kenya kila mwaka

SHINA LA UHAI: Selimundu huua watoto 10,000 nchini Kenya kila mwaka

WANGU KANURI NA LEONARD ONYANGO

MICHAEL Onyonyi hakupata fursa ya kuwaona watangulizi wake wawili kwani waliaga dunia kabla yake kuzaliwa miaka 23 iliyopita.

Lakini Michael aliambiwa na wazazi wake kuwa ndugu zake hao walifariki wakiwa chini ya umri wa miaka mitano kutokana na ugonjwa wa selimundu (sickle cell anemia).

Ugonjwa huu ambao ni wa kijenetiki, huathiri seli nyekundu za damu na kutatiza mzunguko wa damu mwilini.

“Sasa tungekuwa saba katika familia yetu lakini ugonjwa wa selimundu ulitupokonya ndugu wawili na tumesalia watano,” anasema huku akionekana mwenye huzuni.

Michael pia ni mwathiriwa wa selimundu na hali hiyo iligunduliwa akiwa na umri wa miezi tisa.

“Ilipogunduliwa kuwa nami pia naugua selimundu, mamangu alilazimika kuacha kazi aliyokuwa akifanya na kusaka ajira hospitalini ili kujifahamisha mengi zaidi kuhusu ugonjwa huu,” anaelezea Michael ambaye anasomea Ualimu katika Chuo Kikuu cha Kenyatta.

Michael na ndugu zake wengine wawili wanaugua ugonjwa huu.

“Tunatumia dawa kila siku au kila mwezi ili kuepuka kulemewa na ugonjwa huu. Tunahakikisha kuwa tumekula kwa wingi vyakula vyenye protini na vitamini,” anasema.

Wenzake walioaga dunia ni miongoni mwa zaidi ya watoto 10,000 ambao hufariki kila mwaka nchini kutokana na maradhi ya selimundu kabla ya kufikisha umri wa miaka mitano.

Michael Onyonyi anayeugua ugonjwa wa selimundu wakati wa mahojiano. PICHA | SAMMY WAWERU

Takwimu za Wizara ya Afya zinaonyesha kuwa watoto 14,000 huzaliwa na selimundu humu nchini.

Kati ya asilimia 60 na 90 ya watoto hao hufariki kabla ya kufikisha umri wa miaka mitano bila kutambulika kuwa wanaugua selimundu, kulingana na Dkt Rashid Aman, Waziri Msaidizi wa Afya (CAS).

“Hali hiyo inatokana na watoto kutofanyiwa vipimo vya kina pindi baada ya kuzaliwa na ukosefu wa vifaa mwafaka vya matibabu,” anasema.

Dkt Aman anakiri kuwa serikali haijatia bidii vilivyo kupunguza idadi hiyo ya watoto wa chini ya miaka mitano wanaoaga dunia kutokana na maradhi haya.

“Serikali inalenga kuzindua mwongozo utakaohakikisha kuwa watoto wote wanaozaliwa hospitalini wanapimwa kabla ya kuruhusiwa kwenda nyumbani,” anasema.

Kulingana naye tayari mpango wa kupima watoto mara baada ya kuzaliwa umeanzishwa katika Kaunti ya Kisumu.

Dkt Stella Kisoi wa Hospitali ya Mbagathi anaeleza kuwa wazazi wa mtoto aliye na selimundu anapaswa kuhakikisha kuwa anapata lishe bora yenye virutubisho vyote vinavyofaa kama vile vitamini B, chumvi na kuwaotesha jua ya kutosha.

“Mojawapo ya dalili za ugonjwa huu kwa mtoto ni kufura kwa vidole vya mkono au miguu (hand and foot syndrome),” anasema Dkt Kisoi.

Mtoto mchanga anayeugua anafaa kuanzishwa matibabu akiwa na umri wa miezi miwili.

“Mtoto huyo hupatiwa tembe za penicillin ili kuzuia maambukizi ya mara kwa mara mpaka atakapotimiza miaka mitano. Vile vile, wazazi wanapaswa kuhakikisha kuwa mtoto huyo amechanjwa chanjo zote zinazofaa,” anashauri.

Wakati wa maadhimisho ya mwaka huu ya Siku ya Selimundu Duniani, mnamo Juni 17, Dkt Aman alisema kuwa ugonjwa huu umeshika kasi katika kaunti 18 – haswa Magharibi mwa Kenya na Pwani.

Kulingana na Dkt Kisoi, ugonjwa huu umekolea katika maeneo yaliyo na maambukizi mengi ya malaria kama vile Nyanza, Magharibi na Pwani.

“Lakini kuoana baina ya watu kutoka maeneo yaliyoathirika na wale ambao maeneo yao hayana visa vya ugonjwa huu, kunafanya maradhi haya kusambaa zaidi nchini Kenya,” anasema.

Zaidi ya hayo, Dkt Aman anawashauri wazazi kuwapeleka watoto wao wachanga hospitalini mapema ili wachuguzwe na kuanza matibabu wanapopatikana na maradhi haya.

Selimundu hugunduliwa kupitia upimaji wa damu mtoto anapozaliwa. Mtoto huyo hupata ugonjwa huu kupitia kwa vinasaba vya wazazi wake (genes) – yaani hurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine.

Kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO), takribani asilimia 5 ya watoto duniani huzaliwa na jeni zinazosababisha selimundu.

Katika kaunti ya Kisumu, kati ya asilimia 17 na 21 ya watoto wanaozaliwa huwa na maradhi haya.

Hata hivyo, upimaji na uchunguzi kwa watoto wachanga tayari unafanywa katika Hospitali ya Rufaa ya Jaramogi Oginga Odinga, Kisumu.

Kampuni ya Novartis ya nchini Uswisi mwaka 2021 ilitangaza kuwa imeunda apu ya simu itakayowezesha wazazi kujua ikiwa mtoto wao anaugua selimundu.

Apu hiyo ambayo hurekodi data hata nyakati ambazo hakuna intaneti, inalenga kufanya utambuzi wa mapema wa maradhi haya mtoto akiwa mchanga ili matibabu yaanzishwe upesi iwezekanavyo.

Ili kuzuia matatizo na uchungu unaosababishwa na selimundu, Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (CDC) kinashauri waathiriwa kunywa maji mengi, kujikinga na maeneo yaliyo na viwango vya chini vya oksijeni, miili yao isiwe yenye joto jingi au baridi nyingi na wasiende kwenye maeneo yenye urefu wa juu (high altitudes).

  • Tags

You can share this post!

BI TAIFA JULAI 4, 2022

MUME KIGONGO: Japo kitambi kina madhara tele kiafya, kina...

T L