• Nairobi
  • Last Updated December 9th, 2023 7:54 PM
Shambulizi la bomu 1998 lilivyomtosa kwa usanii

Shambulizi la bomu 1998 lilivyomtosa kwa usanii

NA ABDULRAHMAN SHERIFF

AKIWA miongoni mwa Wakenya walioathiriwa wakati wa maafa ya bomu la Balozi wa Marekani jijini Nairobi mnamo Agosti 7, 1998 angali anakumbuka siku hiyo ambayo hivi leo imefikia miaka 23.

Caroline Muthoka aliyekuwa mmoja wa wale waliobahatika kuokoka, ameamua kutoa wimbo wa kumbukumbu ya tukio hilo ambayo ilizinduliwa rasmi siku ya Ijumaa na ana imani ujumbe wake utawafikia wengi walioathirika na ambao wengi wao akiwemo yeye hawajalipwa chochote hadi sasa.

Wimbo wa ‘Poleni’ aliouimba na Caroline ambaye ni msanii aliyehamia nchini Marekani alishirikiana na msanii mashuhuri wa Tanzania Rose Mhando, ulizinduliwa hapo jana bila kuwako kwake sababu hivi sasa anaishi Marekani.

“Nina matarajio makubwa kuwa wimbo wangu huu wa ‘Poleni’ utaitikiwa hasa na wale wote walioathirika kwa njia moja ama nyingine na bomu hilo na ambao wangali wanakumbuka siku hiyo.

Caroline anasema ameuimba wimbo huo kwa huzuni na akawa na matarajio walioathirika watakumbukwa na kusaidiwa ili waweze kujikimu kimaisha. “Nina huzuni kuwa japo kuna baadhi yetu tunajisaidia, wako wasiojiweza kabisa wanastahili kusaidiwa,” akasema.

Akikumbusha yaliyompata, Caroline anasema yeye binafsi alikuwa katika jumba la Co-operative lilokuwa jirani na balozi hiyo ya Marekani huku akiwa na mimba ya miezi saba na akaambiwa kuwa mtoto wake hatakuwa salama kwa sababu ya tumbo lake lilikatikakatika.

“Lakini ninamshukuru Mungu mbali na kuumia vibaya, nilifurahikia kwa kumzaa mtoto wangu salama salmini!,” akasema msanii huyo mzaliwa wa Kenya ambaye hivi sasa ni raia wa Marekani.

Caroline anajivunia kuwa mwanawe anaendelea vizuri na masomo na amepewa jina la Lucky Baraka. Mbali na kuendelea vizuri na masomo yake, mtoto wake huyo pia ana kipawa cha kuimba na anaongoza kanisani.

Caroline Muthoka ni mmoja wa wale waliobahatika kuponea mauti katika mkasa wa 1998 wa shambulizi la bomu. PICHA/ ABDULRAHMAN SHERIFF

Baadhi ya maneno kwenye nyimbo yake huo ya ‘Poleni’ uliozinduliwa jana yalikuwa: “Pole pole Mungu awape nguvu tena, Pole bado kuna tumaini tena, Ingawa mengi mmeyapitia, Tena magumu kusimulia.

“Lakini bado kuna tumaini tena, Vita magonjwa mmepitia, Wengine kutengwa na kutelekezwa, Bado kuna tumaini tena, Mungu mbinguni ameskia kilio chenu ameskia, Nasema mtakumbukwa tena.

“Wengine kwenu vita haviishi, Magonjwa mengi hayaishi, Lakini bado kuna tumaini tena, Tarehe saba mwezi wa nane tisini na nane, Wengine wetu tuliumia kwa bomu, Wengine wetu waliaga, Mungu tuhurumie Mungu.

“Wengine tulipigwa na mabomu, Mifupa yetu nayo ikaumizwa, Lakini kuna tumaini tena, tukakosa wa kutuhurumia, Tukakosa wakutusaidia, lakini bado kuna tumaini tena, Mungu mbinguni naye aliskia, Machozi yetu akatufutia,” hayo ni baadhi ya maneno yaliyhoko kwenye kibao hicho.

Baadhi ya nyimbo alizoimba mwimbaji huyo ni pamoja na ‘Mimi ni Mzalendo’, One diaspora one nation,’ ‘Arusi’, ‘Bwana Mungu’, ‘This is the Lord’s Doing’, ‘Christmas na ‘Thina ni wa Kavinda’.

Aliambia Taifa Leo Dijitali kuwa nyimbo yake iliyowika zaidi ni ile ya ‘Wambumya vaasa’ aliyoimba pamoja na Stephen Kasolo alipokuja Kenya mwezi wa Januari mwaka huu.

Nyimbo zake nne mpya alizozizindua mwezi uliopita wa Julai, mbili alizoimba na Rose Muhando ni ‘Poleni’, na ‘Step by step’ na nyengine mbili za ‘Ndeto ya muthya’ na ‘Nitashinda yote’ aliimba na Kasolo.

Caroline anasema kwake ana nia ya kufika mbali kimuziki. “Ninaazimia kuendelea na bidii yangu ya kuhakikisha nimefanikiwa kutambulika kote duniani,” akasema mwanamuziki huyo.

Amewaomba mashabiki wa muziki wake waendelee kusikiliza nyimbo zake huku akiwaahidi kuwa ana vibaio kemkem anavyoazimia kuvitoa hivi karibuni. “Nina hamu ya kutaka kuwapa burudani tosha wapenzi wa nyimbo zangu,” akasema Caroline.

You can share this post!

Vigogo wanavyoviziana kuwania ubabe 2022

Kibarua cha IEBC kuandaa duru ya pili ya uchaguzi 2022