• Nairobi
  • Last Updated November 28th, 2023 7:53 PM
Sherehe ya ‘Sapanaa’ kutawaza viongozi katika jamii ya Pokot

Sherehe ya ‘Sapanaa’ kutawaza viongozi katika jamii ya Pokot

NA FRIDAH OKACHI

JAMII ya Pokot Magharibi huandaa sherehe kwa kila mmoja anayepata madaraka au cheo fulani cha uongozi kama njia moja ya kumwezesha mhusika kutakaswa na kukubalika.

Sharti kuu ni; Anayepewa madaraka hayo lazima awe na uwezo wa kuiwakilisha jamii katika hadhara mbalimbali.

Sherehe hiyo inajulikana kama Sapanaa.

Katika eneo la Lomut eneobunge la Sigor, Jacob Tong’ole ambaye ni mwakilishi wadi (MCA), alifanyiwa Sapanaa na wazee.

Ishara ya kutawazwa, Tong’ole alipakwa upako kama njia ya kudhihirisha kuwa sasa amekuwa mzee wa kazi na kuruhusiwa kuitumikia jamii ya Pokot ipasavyo.

Waziri wa Kilimo katika Kaunti ya Pokot Magharibi (CEC), Wilfred Longronyang naye pia alipitia wembe huohuo.

Alipewa baraka na wazee wa jamii hiyo.

Wawili hao walibarikiwa, umuhimu wake ukiwa ni kuiwakilisha jamii hii ipasvyo bila ya kukosea.

Wakati wa sherehe hiyo, densi ziliandaliwa wanajamii wakicheza kuashiria furaha.

Aidha, densi hiyo huitwa ‘Chephlaleyo’.

Wakati wa sherehe hizo, baadhi ya mila zilizofuatwa ni kuchinja ng’ombe, wanawake wakizuiwa kukaribia alipochinjiwa.

Wanawake wanatakiwa kukaa ardhini wakiwa wamejifunga leso kama heshima kwa wahusika waliotawazwa.

“Nyama hii inaweza kuliwa na mtu yeyote anayehudhuria sherehe hiyo. Unachopaswa kufahamu ni kuwa huwa imechomwa kwa ngozi ya ng’ombe na wenyeji wanatakiwa kudumisha heshima kwa kiongozi aliyetawazwa,” alisema John Krop, mzee  wa jamii hiyo.

  • Tags

You can share this post!

Stephen Letoo apamba siku maalum ya kuzaliwa kwa Chemutai...

Abiria Nairobi walia kunguni kuwatafuna kwenye matatu

T L