• Nairobi
  • Last Updated May 24th, 2024 12:59 PM
SHINA LA UHAI: Mabadiliko ya tabianchi yanavyochangia ongezeko la maradhi Afrika

SHINA LA UHAI: Mabadiliko ya tabianchi yanavyochangia ongezeko la maradhi Afrika

NA PAULINE ONGAJI

KATIKA kitongoji duni cha Kangemi, Kaunti ya Nairobi, Bi Beth* anaendelea kupokea matibabu dhidi ya maradhi ya kifua kikuu baada ya kupatikana na maradhi hayo wiki moja iliyopita.

Pamoja na wanawe wawili, mama huyu anaishi pamoja na familia ya dadake, Jane, katika nyumba ya vyumba viwili.

“Nililazimika kuhamia hapa mwezi uliopita baada ya nyumba yangu upande mwingine wa mtaa huu kusombwa na maji wakati wa mafuriko,” anaeleza.

Katika nyumba hii pia dadake anaishi pamoja na mumewe na wanawe watatu. Mumewe anaendelea kupokea matibabu ya kifua kikuu baada yeye pia kugundulika kuugua maradhi hayo majuma mawili yaliyopita.

Majuma kadhaa yaliyopita, baadhi ya maeneo nchini yalikumbwa na mvua nyingi iliyosababisha mafuriko. Kulingana na wataalam, hali hii ya anga imetokana na mabadiliko ya tabianchi.

Kulingana na watafiti, kando na mabadiliko ya hali ya anga kama vile halijoto, unyevu hewani na upepo, ambavyo vimehusishwa na usambazaji wa maradhi ya kifua kikuu, visa vya watu wengi kuhama na kuishi mahali pamoja pia huongeza hatari ya maambukizi ya ugonjwa huu.

Kufikia sasa, imekuwa dhahiri kwamba mabadiliko ya tabianchi yametokana na ongezeko la joto duniani ambalo limechochewa na miaka mingi ya uchomaji wa nishati ya visukuku (fossil fuel) kama vile mafuta na makaa ya mawe (coal).

Mataifa yaliyostawi kama vile Amerika, Ulaya na hata Asia, yamelaumiwa kwa kusababisha hali hii kwani ni hayo ambayo ustawi wao umechangiwa pakubwa na matumizi ya vyanzo hivi vya nishati. Lakini kwa upande mwingine, Afrika inaendelea kubeba mzigo mzito kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi licha ya kuwa haijachangia katika uharibifu huu wa mazingira.

Jopo la serikali tofauti linalohusika na utafiti kuhusu mabadiliko ya tabinchi (IPCC), linatabiri kwamba eneo la Afrika lililoko Kusini mwa Jangwa la Sahara, litaendelea kukumbwa na hatari ya joto jingi kutokana na mabadiliko ya tabianchi. Na tayari mabadiliko hayo yameanza kushuhudiwa katika ongezeko la maradhi mengine mengi, kando na kifua kikuu.

Mabadiliko ya tabianchi yamethibitishwa kuchangia mkurupuko wa magonjwa mengi hapa barani.

Uchanganuzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO), umeonyesha kwamba dharura za kiafya zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi, zimezidi kuongezeka hapa barani.

Kulingana na uchanganuzi huo, asilimia 56 ya visa vya kiafya vilivyonakiliwa barani Afrika kati ya mwaka wa 2001 na 2021, vilihusishwa na mabadiliko ya tabianchi.

Lakini mabadiliko ya tabianchi yanachocheaje kuongezeka kwa maradhi?

Kipindupindu na maradhi mengine yanayosambaa kupitia maji

Uchanganuzi wa hivi majuzi wa WHO, umeonyesha kwamba maradhi yanayosambaa kupitia maji yaliwakilisha asilimia 40 ya dharura za kiafya zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi.

Barani Afrika, maradhi ya kuendesha yameorodheshwa ya tatu miongoni mwa magonjwa yanayosababisha vifo vingi kwa watoto chini ya miaka mitano.

Ukame kama ulivyoshuhudiwa katika maeneo ya Kaskazini Mashariki mwa nchi umesababisha mito mingi ambayo ni vyanzo vya maji safi, kukauka na hivyo kusababisha uhaba wa maji.

“Uhaba wa maji unaathiri uwezo wa watu kufikia maji safi ya kunywa. Uhaba huu husukuma watu kutumia maji chafu na hivyo kuongeza uwezekano wa kusambaa kwa kipindupindu,” aeleza Dkt Alinafe Kasiya, mtaalam wa masuala ya afya nchini Malawi.

Hapa nchini, kufikia Februari 2023, WHO, ilionyesha kwamba Kenya ilikuwa imenakili takriban visa 5,000 vya kipindupindu. Maeneo yaliyokuwa yameathirika pakubwa na ukame kama vile Garissa, na Wajir, ndio yalinakili visa vingi.

Lakini kando na ukame, mafuriko ambayo yameshuhudiwa katika sehemu kadha wa kadha barani na hasa humu nchini, yamehusishwa na mkurupuko wa maradhi yanayosambaa kupitia maji.

Mvua nyingi kama inavyoshuhudiwa sasa nchini ina athari kubwa kwa afya. Kwa mfano, maji haya ya mafuriko yanapotiririka kutoka sehemu moja hadi nyingine, hubeba uchafu na hivyo kuchafua vyanzo vya maji safi ya kunywa na kusababisha maradhi kama vile kichocho na kipindupindu.

Maradhi ya akili

Kulingana na utafiti wa IPCC mabadiliko ya tabianchi yanaathiri maisha ya kila siku ya kiuchumi, kiafya na kijamii, na hivyo kuchochea matatizo ya kiakili kama vile msongo wa mawazo na akili.

Katika eneo la Kaskazini Mashariki hapa nchini, mfululizo wa miaka ya ukame na mafuriko umesababisha maafa mengi huku wakulima wakipoteza mifugo na mimea yao.

“Wengi wa wakulima hawa wanategemea mifugo katika maisha ya kila siku, na hivyo hasara hiyo imesababisha umaskini. Wengi wamejipata katika ufukara, suala ambalo limewafanya kukumbwa na matatizo ya kiakili,” ripoti hiyo inaeleza.

Maradhi yanayosambaa kupitia wadudu

(Malaria)

Kulingana na watafiti, mbu wanaosababisha malaria ambao kwa kawaida wametambulika kukita mizizi katika maeneo ya chini ya pwani ya Kenya na Magharibi, sasa wamekuwa wakihama kutokana na mabadiliko ya hali ya anga.

Hii inamaanisha kwamba katika siku za usoni huenda maradhi haya yakakithiri katika sehemu zingine za nchi na hivyo kuzima jitihada za kupambana na ugonjwa huu hatari.

Maradhi yanayosambaa kutoka kwa wanyama hadi binadamu

Utafiti unaonyesha kwamba ongezeko la joto duniani limesababisha kuongezeka kwa uwezekano wa msambao wa maradhi kutoka kwa wanyama hadi binadamu.

Ripoti ya mwaka 2022 iliyoangazia mchango wa mazingira katika afya- “A health perspective on the role of the environment in One Health”, iliyoratibiwa na kituo cha mazingira na afya cha WHO barani Ulaya, ilionyesha kwamba mabadiliko ya tabianchi yamechochea kuenea kwa maradhi haya kwa njia kadha wa kadha.

Kulingana na Dkt Siro Masinde, Mwanasayansi mkuu wa utafiti katika Makavazi ya Kitaifa nchini, mabadiliko ya matumizi ya ardhi huwalazimu watu kuingilia mazingira ya wanyama.

“Hii huongeza uwezekano wa mtagusano, na hivyo msambao wa maradhi ya aina hii,” aeleza

Pia, Dkt Dino Martins, mtaalam wa utafiti wa wadudu na mwanabiolojia, asema kutoweka kwa baadhi ya viumbe hai hupunguza uwezo wa mazingira kuzimua bakteria, virusi na viumbehai vingine vinavyosababisha maradhi.

Utapia mlo

Kulingana na WHO, Kenya ni miongoni mwa mataifa 12 ambayo yanakumbwa na janga la utapia mlo kutokana na baa la njaa. Kenya ni miongoni mwa mataifa mengine ya upembe wa Afrika ambayo yaliathirika pakubwa na mojawapo ya ukame mkali kuwahi shuhudiwa katika kipindi cha miongo minne iliyopita.

Janga hili lilisababisha mazao duni ya kilimo na sasa maeneo ya Kaskazini Mashariki yaliyoathirika pakubwa yanakodolea macho baa la njaa. Kutokana na hili, mamilioni ya watu na hasa watoto katika maeneo haya wamo katika hatari ya kukumbwa na utapiamlo kwa sababu ya ukosefu wa chakula cha kutosha.

Maradhi ya mfumo wa kupumua

Halijoto ya juu huchochea ongezeko la vichafuzi vya mazingira na mizio. Kulingana na watafiti, haya viwili ndio huchangia pakubwa maradhi ya mapafu na moyo.

Afya ya uzazi

Mabadiliko ya tabianchi yamesababisha hasara kubwa katika jamii za wahamiaji ambazo hutegemea sana mifugo.

Wafugaji wengi wamepoteza mifugo yao ambayo huwa chanzo cha utajiri. Wengi wamebakia kuwa masikini na sasa kuanza kurejelea tamaduni zilizopitwa na wakati kama vile kuwaoza watoto wao wasichana ili kujikimu.

Kutokana na kuwa mara nyingi watoto hawa huolewa wakiwa hawajakomaa, wanaposhika mimba, wao hukumbwa na matatizo wakati wa kujifungua, suala linaloongeza vifo miongoni mwa akina mama na watoto wakati wa kujifungua.

Kulingana na Dkt Ahmed Ogwell Ouma, Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Afrika cha kudhibiti na kuzuia maradhi barani (Africa CDC), athari zinatokana na mabadiliko ya tabianchi husababisha mzigo mzito katika mfumo wa afya barani ambao tayari unakumbwa na changamoto nyingi.

  • Tags

You can share this post!

Maandamano ya Azimio yalivyozimwa

Guterres aanza ziara rasmi ya siku mbili nchini Kenya

T L