• Nairobi
  • Last Updated December 4th, 2023 6:37 PM
SHINA LA UHAI: Matibabu ya kansa nchini yamletea afueni afya ikiimarika

SHINA LA UHAI: Matibabu ya kansa nchini yamletea afueni afya ikiimarika

NA PAULINE ONGAJI

KATIKA kitengo kipya maalum cha matibabu ya kuhamisha uboho (bone marrow transplant) BMT kwenye orofa ya sita ya hospitali ya Nairobi West, jijini Nairobi, Bw Martin Gaitho, 58, anajibu maswali kutoka kwa mwanahabari.

Yuko hapa kuzungumzia safari yake ya kuendelea kupata afueni baada ya kufanyiwa utaratibu wa BMT miezi miwili iliyopita ili kutibu maradhi ya multiple myeloma, ambayo ni aina ya kansa ya uboho.

Bw Gaitho amekuja hospitalini kufanyiwa ukaguzi wake wa tatu, ambapo ameandamana na mkewe, Loise.

Afueni yake imempa furaha sana kiasi kwamba hata walipokuja hospitalini, Bw Gaitho mwenyewe aliendesha gari, jambo ambalo hangeweza kufanya miezi michache iliyopita.

“Huu ni ushuhuda kwamba hali ya mume wangu imeendelea kuimarika tangu kupokea matibabu haya,” aeleza mkewe, Loise.

Mwezi Juni 2022, Bw Gaitho, aligundulika kuugua multiple myeloma, maradhi yaliyomuacha na maumivu makali ya mgongo na kifua.

“Tatizo lilianza Aprili 2022 ambapo nilianza kukumbwa na maumivu makali ya sehemu ya chini ya mgongo, tatizo ambalo lilienea hadi kifuani,” aeleza.

Ni tatizo ambalo liliathiri maisha yake ya kawaida.

“Kutokana na maumivu hayo, wakati huo singeweza kuinama au hata kukaa chini.”

Kwa hivyo, alienda katika hospitali moja jijini Nairobi huku akidhani kwamba hili lilikuwa tu tatizo la kawaida na angepata nafuu baada ya kumuona daktari na kutumia dawa.

Lakini kinyume na hayo hata baada ya kupokea matibabu, maumivu yaliendelea, suala lililomlazimu kupata maoni mengine katika hospitali tofauti.

“Hapa nilifanyiwa chunguzi kadhaa ikiwa ni pamoja na wa mkojo na damu, ambapo daktari alishuku kwamba nilikuwa na kansa ya uboho.”

Habari hizi zilimshangaza kiasi cha kumsukuma kutafuta maoni mengine katika hospitali ya Nairobi West ambapo miezi miwili baadaye, ilithibitishwa kwamba kwa kweli alikuwa na kansa hii.

“Kufikia hapa madaktari waliniambia kwamba ilikuwa lazima nianze matibabu haraka. Pia wakati huu kuna daktari ambaye aliniuliza iwapo ningekubali kujumuishwa kwenye foleni ya wagonjwa ambao walikuwa wamepangiwa kufanyiwa utaratibu huu katika hospitali hiyo,” aeleza.

Anasema kwamba alifurahi kusikia kwamba angefanyiwa utaratibu huo humu nchini.

“Hii ni kwa sababu nilikuwa nimefanya utafiti wangu tayari kuhusu matibabu haya na kugundua kwamba ningelazimika kwenda ng’ambo,” aongeza.

Kwa hivyo, baada ya kukubaliana, shughuli ya matibabu zilianza lakini kuna masuala kadha wa kadha ambayo madaktari wangeangazia.

“Ilibidi madaktari wanikalishe chini na kuniandaa kwa kuzungumzia masuala kama vile utaratibu huo, madhara ya kiafya ambayo yangeambatana nayo, vile vile gharama ya matibabu.”

Kuhusu gharama, bila shaka matibabu hayangetarajiwa kuwa bei rahisi, lakini Bw Gaitho asema hangeweza kamwe kuilinganishwa na gharama ya kutibiwa ng’ambo.

“Nilifanya utafiti katika baadhi ya hospitali nchini India ambapo niligundua kwamba gharama ya matibabu ilikuwa ikifikia $40,000, sawa na zaidi ya Sh5 milioni, kwa matibabu pekee. Hii inamaanisha kwamba kulikuwa na gharama za ziada za usafiri na malazi, miongoni mwa zingine,” aongeza.

Maandalizi ya kumfanyia Bw Gaitho utaratibu wa autologous stem transplant yaling’oa nanga rasmi. Utaratibu huu ulikuwa wa pili hospitalini humo tangu matibabu hayo yazinduliwe rasmi Oktoba 2022.

“Autologous stem cell transplant ni aina ya matibabu ya kuhamisha uboho ambapo seli zinazounda damu zinakusanywa kutoka kwa damu au uboho kabla ya matibabu, na kuhifadhiwa kisha kurejeshewa mwilini mwa mgonjwa baada ya utaratibu huu. Seli hizi hutolewa ili kuzuia zisiharibike wakati wa matibabu ya tibaredio au dozi nyingi za tibakemia, kisha baadaye kurejeshwa ili zijiunde upya katika sehemu hii ya mwili,” aeleza Dkt Rohini Radia, Mwanahematolojia na daktari wa matibabu ya uboho katika hospitali ya Nairobi West.

Dkt Rohini Radia, mwanahematolojia na daktari wa matibabu ya uboho (Bone Marrow) katika hospitali ya Nairobi West. PICHA | HISANI

Kulingana na Dkt Radia, utaratibu huu hutumika kutibu aina ya kansa za damu kama vile leukemia na lymphoma.

Kwa hivyo, mwezi Julai mwaka jana, Bw Gaitho alianza kupokea matibabu ya tibakemiaa kama maandalizi ya utaratibu huu.

“Ni utaratibu ambao uliendelea kwa miezi mitano ambapo nilipokea dozi tisa kali za tibakemia kando na kuendelea kufanyiwa uchunguzi wa damu,” asema.

Utaratibu huu ulifanywa chini ya kikundi cha madaktari ambacho kilihusisha daktari mkuu Dkt Guarav Dixit, kutoka India, vile vile Dkt Radia.

“Kisha kulikuwa kikundi hiki kingine kilichohusisha mwanahematolojia wangu kutoka Hospitali Kuu ya Kitaifa ya Kenyatta na kikundi chake, vile vile madaktari wengine kutoka hospitali ya Nairobi West, waliokuwa wakifuatlia hali yangu ya kiafya,” aeleza Bw Gaitho.

Kulingana na Dkt Radia, kama daktari, wakati wa kumkagua mgonjwa ambaye anafaa kufanyiwa BMT utahitaji maelezo zaidi kuhusu maradhi anayougua.

“Kuanzia kwa utambuzi na matibabu ya maradhi hayo miongoni mwa mambo mengine, sharti ujadiliane na daktari ambaye amekuwa akimshughulikia mgonjwa. Hii ni muhimu kwani husaidia wataalam wahusika kupata fursa ya kujadliana na kutambua ikiwa kwa kweli mgonjwa atahitaji kufanyiwa BMT.”

Bw Gaitho alifanyiwa BMT Novemba mwaka jana, utaratibu uliochukua saa kadhaa ambapo baadaye alihitajika kuendelea kupokea matibabu huku akiwa ametengwa kwa siku.

“Mgonjwa anapofanyiwa utaratibu huu hutengwa kabisa kutokana na mazingira ya nje kwani wakati huu kingamwili yake huwa chini sana,” aeleza Dkt Radia.

Wakati huo, familia ya Bw Gaitho haikuruhusiwa kumuona japo walipokea taarifa za kila mara kutoka kwa daktari kila siku.

“Ilikuwa rahisi kwetu kama familia kuja kumuona baadaye pindi baada ya daktari kuruhusu,” aeleza Bi Loise.

Dkt Radia asema hii ni faida ingine ya kufanyiwa utaratibu huu karibu na nyumbani.

“Kwa familia ni ngumu kuwa na mpendwa anayepokea matibabu pasipo kuweza kumuona kwa muda mrefu, lakini utaratibu huu unapofanyiwa nchini huwa rahisi kumuona pindi daktari anaporuhusu kufanya hivyo, pasipo kufikiria masuala ya usafiri na gharama zingine.”

Dkt Radia pia anasema kwamba mgonjwa anapofanyiwa utaratibu huu nyumbani huwa rahisi kwa madaktari kumkagua kila wakati.

“Ni muhimu kufuatilia mgonjwa ambaye amefanyiwa utaratibu huu kwa sababu huenda akakumbwa na matatizo, na hivyo itakuwa rahisi kudhibiti tatizo likitokea.”

Kwa sasa Bw Gaitho anasubiri kurejea hospitalini kwa ukaguzi mwingine unaotarajiwa kufanywa Machi 7 (leo), huku akiendelea kupokea dawa za kuzuiamaambukizi.

Kulingana na Prof Andrew Gachii, Mkurugenzi mkuu wa matibabu katika hospitali ya Nairobi West, tatizo la kufikia huduma bora za karibu kwa bei nafuu limekuwa donda sugu kwa wagonjwa wengi hapa nchini, ambao wengi hulazimika kusafiri ng’ambo kwa matibabu kama vile BMT.

“Kuwa na utaratibu huu hapa nchini utafaidi sana wagonjwa wanaohitaji,” aongeza.

  • Tags

You can share this post!

Chap Chap hatutamezwa na UDA – Mbunge

Gachagua: Nilinunuliwa suruali yangu ya kwanza nikiwa Form 2

T L