• Nairobi
  • Last Updated September 26th, 2023 10:25 PM
SHINA LA UHAI: Safari yake kushughulikia mtoto wake mwenye utindio wa ubongo

SHINA LA UHAI: Safari yake kushughulikia mtoto wake mwenye utindio wa ubongo

NA PAULINE ONGAJI

MIAKA mitatu iliyopita, Bi Ednah Mokeira, 35, mkazi wa mtaa wa Kasarani, Kaunti ya Nairobi, aliingia hospitali ya akina mama huku akiwa na matumaini ya kujifungua baada ya miezi tisa ya subira.

Lakini mambo hayakuenda sawa na matarajio yake, kwani mwanawe, Michael Shujaa, alianza kukumbwa na matatizo muda mchache baadaye, shida ambayo miezi michache baadaye ilithibitishwa kuwa utindio wa ubongo (cerebral palsy).

Katika kipindi chake cha ujauzito, Bi Mokeira asema mambo yalikuwa ya kawaida na hakukuwa na tatizo lolote.

“Wakati wa kujifungua hata hivyo, nilikumbwa na uchungu wa uzazi kwa muda wa zaidi ya saa 12. Wakati huu lango la uzazi halikuwa limefunguka vilivyo ambapo daktari alisema nipelekwe chumba cha upasuaji ili kufanyiwa upasuaji,” asema.

Lakini muda mchache baada ya mwanawe kuondolewa tumboni mwake kupitia upasuaji, Bi Mokeira alianza kukumbwa na wasiwasi baada ya kushuhudia dalili zisizo za kawaida. “Mwanangu hakulia kama ilivyo kawaida, na hakuwekewa oksijeni kama inavyotarajiwa. Pia, hakuanza kunyonya kama kawaida,” aeleza. Kulingana na Bi Mokeira, hapo ndipo alipoanza kushuku kwamba mambo hayakuwa sawa. Mambo yalikuwa mabaya hata zaidi siku iliyofuatia, mwanawe alipoanza kuonyesha dalili zilizompa wasiwasi hata zaidi. “Macho yake yaligeuka na kuwa rangi ya manjano na kujibingirisha. Pia, alianza kuwa na mtikiso,” aeleza.

Bado kufikia wakati huu, asema, daktari hawakumwambia kwamba mwanawe alikuwa anahitaji kuwekewa oksijeni. “Ilitubidi kutafuta maoni ya ziada na kufikia uamuzi wa kwenda katika hospitali nyingine. “Pindi baada ya kufika hapo, mwanangu aliwekwa kwenye oksijeni na matibabu ya zaidi, lakini bado hakupata na nafuu.”

“Wiki tatu baadaye, Shujaa aliruhusiwa kuenda nyumbani lakini bado hakukuwa na mabadiliko. “Kinachoshangaza ni kwamba wakati huu wote madaktari waliomshughulikia hawakunipa majibu. Nilikuwa na wasiwasi na ningeuliza iwapo kulikuwa na wasiwasi wa mwanangu kukumbwa na hali hii, lakini walinipa matumaini kwamba hali ingebadilika,” asema Bi Mokeira.

Kufikia miezi sita, bado Shujaa hangeweza dhibiti kichwa chake wala kukaa chini. “Kufikia hapa nilitafuta ushauri zaidi kutoka kwa daktari mwingine aliyenishauri aanze kufanyiwa tibamaungo. Ni hapa ndipo aligundulika rasmi kuwa na utindio wa ubongo, na kuanzishiwa matibabu yanayoambatana na hali hii,” aeleza.

“Kwa hivyo kila mwezi lazima nimpeleke kwa mwananyurolojia ili afya yake ikaguliwe. Aidha, mwanangu anahitaji matibabu yanayohusisha dawa za kukabiliana na mtikiso, vijalizo, miongoni mwa zingine. Kisha kuna huduma za tibamaungo ambazo lazima apate kila wiki, suala ambalo limenigharimu pakubwa kiuchumi.” Bi Mokeira anasisitiza kwamba iwapo wakati wa kujifungua madaktari wangemshughulikia mwanawe kama inavyohitajika, basi hangekumbwa na tatizo hili. Utindio wa ubongo ni tatizo linaloathiri mwelekeo wa misuli. Mara nyingi huathiri uwezo wa mwili kusonga na misuli kupatana kama kawaida. Aidha, hali hii huathiri shughuli za mwili kama vile mwendo wa misuli, kupumua, kudhibiti mkojo na kinyesi, kula na kuzungumza.

Kuna aina tatu za utindio wa ubongo: spastic cerebral palsy, husababisha misuli kuwa migumu na hivyo kusababisha matatizo ya mgonjwa kusonga.

Kwa upande mwingine dyskinetic (athetoid) cerebral palsy humsababisha mgonjwa kushindwa kudhibiti mwendo wa viungo, na ataxic cerebral palsy huathiri uthabiti wa viungo vya mwili.

Kulingana na Dkt Lincoln Kasakhala, mtaalam wa Idara ya tiba ya magonjwa ya akili katika Chuo Kikuu cha Nairobi, mara nyingi hali hii hutokana na uharibifu wa ubongo kabla, wakati au baada ya kuzaliwa, au kati ya miaka mitatu na mitano ya kwanza ya mtoto. “Uharibifu huu wa ubongo waweza sababisha matatizo kama vile kuona, kusikia na kujifunza.”

Aidha, anasema kwamba majeraha ya ubongo husababishwa wakati wa mama kujifungua. “Hapa yaweza tokana na mama kukumbwa na uchungu wa uzazi wa muda mrefu pasipo kushughulikiwa, suala linalosababisha kiunga mwana kujifunga kwenye shingo la mtoto. Hii huzuia ubongo kukosa oksijeni ya kutosha na hivyo kusababisha uharibifu wa ubongo,” aeleza.

Hali ya tatu, anasema kwamba husababishwa iwapo baada ya kuzaliwa, mtoto atakumbwa na maradhi na kutopokea matibabu kama inavyohitajika, suala ambalo pia laweza athiri ubongo.

“Aidha, baada ya mtoto kuzaliwa anaweza kumbwa na majeraha ya ubongo pengine akiangushwa kisha kichwa chake kigonge sehemu ngumu na hivyo kusababisha jeraha kwenye ubongo.

Kulingana na Shirika la Afya duniani, WHO, kila wakati watoto 1,000 wanaozaliwa katika mataifa yanayostawi, ikiwa ni pamoja na Kenya, wanne hukumbwa na hali hii.

Humu nchini hakuna takwimu rasmi kuhusiana na maradhi haya, lakini kuna baadhi ya wataalamu wanaokadiria kwamba kati ya watoto 100 nchini, watatu wanakumbwa na maradhi haya.

Hii ni idadi kubwa ikilinganishwa na nchi kama Amerika, ambapo takwimu zinaonyesha kwamba hali hii hutokea kwa mtoto mmoja kati ya 500 wanaozaliwa. Kulingana na Bw George Kakala, ambaye wakati mmoja alikuwa mwenyekiti wa shirika la Cerebral Palsy Society of Kenya CPSK, ongezeko la visa hivi humu nchini hasa linatokana na ulegevu wa wahudumu katika hospitali.

“Tafiti kadhaa ambazo tumefanya katika hopitali mbali mbali zimeonyesha kwamba hali hii imekithiri sana ambapo sababu kuu imeonekana kuwa kutelekezwa na akina mama wakati wa kujifungua,” aeleza.

Aidha, anasema tatizo hili humu nchini husababishwa na akina mama wasiohudhuria huduma za kliniki wakati wa ujauzito.

“Hapa inakuwa ngumu kwa wahudumu kukagua mkao wa mtoto akiwa tumboni, suala ambalo mara nyingi husababisha matatizo wakati wa kujifungua,” aeleza. Kulingana na Bw Kakala, hili ni tatizo ambalo laweza kabiliwa humu nchini.

“Serikali inapaswa kuingilia kati na kuhakikisha kwamba idadi hii inarudishwa chini vilivyo. Hii itafanikishwa kwa kuhakikisha kwamba mafunzo zaidi yanatolewa kwa wakunga na wahudumu wengine wa kiafya,” aongeza.

  • Tags

You can share this post!

Raia kuendelea kuumia zaidi

Pasta Ezekiel ataka agizo la kuzima kituo chake cha runinga...

T L