• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 6:47 AM
Shirleen analenga kutamba kinoma katika uigizaji

Shirleen analenga kutamba kinoma katika uigizaji

NA JOHN KIMWERE 

PENYE nia pana njia.

Ndivyo wahenga walivyolonga na tangia zama zile ndivyo hali ilivyo hadi sasa. Ni msemo unaonekana kuwa na mashiko kwa kiwango fulani miongoni mwa jamii.

Pia ni msemo unaendelea kuthibitishwa na vijana wengi wavulana kwa wasichana wanaojitosa kuchangamkia shughuli tofauti kwenye jitihada za kusaka riziki.

Shirleen Njeri Gathigia ni kati ya waigizaji wa kike wanaoibukia wanaopania kutinga hadhi ya kimataifa miaka ijayo. Anasisitiza kuwa amepania makubwa katika tasnia ya uigizaji.

Kando na uigizaji, binti huyu aliyezaliwa mwaka 2001 anatarajia kuhitimu kwa shahada ya diploma kama mwana habari kwenye Taasisi ya NIBS College.

Anashikilia kuwa anakaribia kutimiza ndoto yake ya tangia akiwa mdogo alikopania kuwa mwana habari.

”Ingawa sijapata mashiko nilianza kushiriki uigizjai nikiwa mdogo kanisani lakini kitaaluma nilianza mwaka 2019 na kundi la Auto-Frames Entertainment,” amesema.

Anaongeza kuwa amepania kufuata nyayo zake mwimbaji na mwanamaigizo, Sanaipei Tande.

Hapa nchini angependa kujikuta jukwaa moja na waigizaji kama Sarah Hassan ‘Plan B’ na ‘Zora’ pia Sanaipei Tande ‘Aziza,’ na ‘Kina’.

Anasema Afrika angependa kufanya kazi na mwana muziki pia mwigizaji maarufu kama Mimi Mars (Marianne Mdee) mzawa wa Tanzania aliyeshiriki filamu zilizopata umaarufu sio haba kama  ‘You again’ na ‘Jua Kali’.

Anashikilia kwamba akitinga upeo anaolenga katika uigizaji ndio atawazia pengine kuwa produsa ama kuanzisha brandi yake. ”Kulingana na changamoto nyingi ambazo waigizaji wanaokuja hupitia ningependa kumiliki brandi yangu huku nikilenga kusaidia wasanii chipukizi,” akasema.

Katika mpango kutwa amepania kuibuka kati ya waigizaji mahiri nchini ndani ya miaka mitano ijayo. Anaamini kuwa uigizaji ni ajira kama nyingine.

Msanii chipukizi Shirleen Njeri Gathigia. PICHA | JOHN KIMWERE

Anaomba Wakenya wawe na uzalendo na kuwashika mkono waigizaji wa humu nchini.

Kipusa huyu mwenye tabasamu ya kuvutia anajivinia kushiriki filamu kama ‘Date my family Kenya’, ‘Love Crisis’, ‘Betrayal’ na ‘Forbidden Love,’ kati ya nyingine.

Anashikilia kuwa imekuwa vigumu kwa waigizaji wanaokuja kwenye gemu kupata nafasi ilhali kila mmoja anatamani kuonyesha ujuzi wake. Kwa ujumla sekta ya uigizaji ina ushindani mkali kwa kuzingatia mara nyingi waliotangulia ndio hupata nafasi.

Hata hivyo si mchoyo wa mawaidha. Anawaambia wasanii wenzake kuwa: ”Akili sio vikombe vya wageni; tumia vile inafaa.”

Pia anasema hakuna kinachopatikana rahisi kwani ni lazima kila kitu kifanyiwe kazi kwa kujituma.

Anawataka wasanii wajiheshimu bila kusahau kuwaheshimu waliowatangulia.

Anawahimiza kuwa endapo wanahisi wana kipaji, hawapaswi kuvunjika moyo wala kukata tamaa baada ya kukosa nafasi mara kadhaa.

”Jambo jingine ningependa kuwapa wenzangu ni kuwa wasiwe wepesi wa kutaka kupata umaarufu hasa kwa kukubali kuingia kwenye mahusiano ya kimapenzi na maprodusa ambao hupenda kuwashusha wanawake,” akasema.

  • Tags

You can share this post!

Faith Mwende asema yuko ngangari akijiandaa kukwea Mlima...

Pasta matatani kukwamilia pikipiki aliyoazima imsaidie...

T L