• Nairobi
  • Last Updated October 2nd, 2023 10:18 AM
TAHARIRI: Wizara ifuatilie ili pesa zisichelewe

TAHARIRI: Wizara ifuatilie ili pesa zisichelewe

KITENGO CHA UHARIRI

SHULE zinapofunguliwa tena leo Jumatatu baada ya karibu miezi kumi, jambo kubwa zaidi litakuwa ni jinsi gani wazazi wanalipa karo.

Jumapili waziri wa Elimu, Profesa George Magoha aliwaagiza walimu wakuu wa shule wafanye ukaguzi wa kina na kubaini kuwatambua wanafunzi kutoka familia zisizojiweza kifedha na kutowalipisha karo.

Agizo hilo la waziri huenda likazua sokomoko katika shule nyingi nchini. Wazazi wengi ambao kabla ya kuzuka kwa janga la Corona walikuwa na uwezo wa kupa karo, sasa hivi wanapitia wakati mgumu. Baadhi hata hawawezi kukimu mahitaji ya kimsingi ya familia zao. Kwa hivyo, wazazi watapeleka watoto shuleni mikono mitupu.

Hali huenda isiwe ngumu kwa shule za msingi za umma, lakini kwa zile za upili, huenda walimu watakapoachiwa jukumu la kuzisimamia wakawa na wakati mgumu kuwalisha wanafunzi.

Rais Uhuru Kenyatta alitangaza kwamba walimu na wafanyikazi wa shule waliotimiza umri wa miaka 58 na juu hawatahitajika shuleni. Wengi wa hao ni walimu wakuu.

Ina maana kuwa walimu wa umri wa chini ya hapo ndio watakaoachiwa mamlaka hayo ya kusimamia shule, na kukumbana na mzigo wa kuweka wanafunzi shuleni bila pesa za kununua chakula kati ya huduma nyingine.

Kwa hivyo tangazo la Profesa Magoha kwamba pesa zitafika kwenye akaunti za shule za upili kufikia Ijumaa yafaa liwe la kweli.

Si kwamba tunashuku uwezo wa waziri huyo, lakini serikali imekuwa na mtindo wa kuchelewesha pesa za huduma muhimu. Ni juzi tu ambapo Baraza la Magavana lililalama kuwa kaunti zilikuwa hazijapokea pesa za miezi miwili.

Pesa za kupelekwa shuleni zilifaa kuwekwa kwenye akaunti hata kabla ya sherehe za Mwaka Mpya, kwa kuwa ilijulikana mapema kwamba shule zingefunguliwa leo.

Ahadi ya kuwa Sh4 bilioni za shule za msingi zitakuwa kwenye akaunti kesho pia lisiwe jambo la mzaha. Kumekuwa na mazoea ya serikali kutangaza kwamba pesa zimefika shuleni, huku walimu wakuu wakiendelea kuhangaika.

Waziri ahakikishe kwamba maafisa wa wizara yake wanafuatilia kwa karibu na wenzao wa wizara ya Fedha, ili pesa hizo zisichelewe.

You can share this post!

Papa Francis akubali kujiuzulu kwa Kadinali John Njue...

Wanafunzi 110 walazimika kurudi nyumbani baada ya kukosa...