• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 10:55 AM
TALANTA: Kiongozi wa nyimbo

TALANTA: Kiongozi wa nyimbo

NA PATRICK KILAVUKA

UKAKAMAVU, ujasiri na kujiamini vimekuwa vigezo ambavyo vimemfaa zaidi katika jitihada za kuongoza nyimbo katika tamasha za muziki na shuleni hususan siku za sherehe za utamaduni na hafla nyinginezo.

Isitoshe, misakato na sauti mithili ya ninga husisimua wengi anapoongoza nyimbo.

Ana azma ya kuzamia uimbaji siku za majaliwa akifahamu fika kwamba usanii ni ajira.

Tunayemrejelea ni kiongozi wa nyimbo Loicey Nyamwira, 9, ambaye ni mwanafunzi wa gredi ya nne katika shule ya msingi ya Cherry Child Education Centre, kaunti ndogo ya Kibra, Nairobi.

Nyawira anasisitiza kwamba mwimbaji na kiongozi mpevu na mwenye talanta anapaswa kuwa mwepesi wa kuelewa au kukariri nyimbo kutoka jamii yoyote ile.Yeye ni mwana wa tatu katika jamii ya watoto wanne wa Bw Elphas Amwai na Bi Merclynne Kaveri.

Alianza tu kuimba nyimbo kama uraibu akiwa nyumbani. Anasema kwamba hali hii ilimfungua mzazi wake macho na kutambua kuwa mwanawe alikuwa na kipaji ambacho kinafaa kukuzwa. Alimhimiza ajitahidi katika kukikuza. Nyota yake ya jaha iliendelea kung’aa pale ambapo mwalimu wake shuleni Florence Fariji aliitambua zaidi talanta yake na kuanza mikakati ya kumweka katika mkondo mkali wa mazoezi ili kumwezesha kuwa kiongozi wao katika mashindano ya tamasha za muziki.

“Alionesha ukakamavu, ujasiri na kuwa mwepesi wa kuelewa nyimbo. Isitoshe, ni mkariri mzuri na alinitia moyo kwamba angeweza licha ya umri wake mdogo,” anasema mkufunzi Fariji.

Alifanya kweli katika mashindano ya tamasha za muziki za shule za msingi za kaunti ndogo ya Kibra na kuibuka wa kwanza katika kitengo chao.

Kiongozi wa nyimbo za kitamaduni Loicey Nyamwira akiongoza wenzake kufanya mazoezi wakati wa mashindano ya tamasha za nyimbo na drama katika Kanda ya Nairobi yaliyoandaliwa katika Shule ya Msingi ya Westlands. PICHA | PATRICK KILAVUKA

Yeye na kikundi chake walifuzu kushiriki mashindano ya Kanda ya Nairobi ambayo yaliandaliwa katika shule ya msingi ya Westlands na kutwaa nafasi ya tatu bora kikanda.Nyawira ana ndoto kwamba siku moja ataongoza kikundi cha shule hadi ngazi ya kitaifa na kutumbuiza katika ikulu.

Ili kujiongezea mazoezi zaidi, yeye huimba na kushiriki katika ibada za watoto – Sunday School kanisa la Mwembeni Friends Mashimoni, Kibera.

Aidha, yeye huchota maarifa ya kiufundi kutokana na kutazama kipindi cha The Music Festival, Citizen.

Nyawira angependa kufuata nyayo za shangaziye mwimbaji Morine Kamula kutokana na sauti yake nyororo na mawaidha ya kumhimiza

.Changamoto ambayo yeye hukumbana nayo ni kwamba kuna nyimbo nyingine ambazo zinafaa mtu amakinike zaidi ndiposa azielewe kabla ya kuanza kuzikariri.

Vilevile, ipo haja ya kusawazisha muda wa masomo na ukuzaji wa talanta.

Ushauri wake ni kwamba, mtaala wa umilisi unafaa sana katika kuwekea msingi talanta. Mbali na hayo, anahimiza kwamba ipo haja kwa waliobarikiwa kwa vipaji wavikuze kwani ya kesho ni huwezi kuyajua. Ni Mungu ndiye mpaji wa talanta na karama.

  • Tags

You can share this post!

Pique aagana rasmi na Barcelona na kustaafu soka

Simba Queens yaingiza Afrika Mashariki nusu-fainali CAF

T L