• Nairobi
  • Last Updated February 26th, 2024 11:50 AM
UJASIRIAMALI: Alitalii, akapata wazo la kuuza utalii na hajuti

UJASIRIAMALI: Alitalii, akapata wazo la kuuza utalii na hajuti

NA PETER CHANGTOEK

SASHA Seraphine Mbote alijiuzulu kutoka kwa kazi aliyokuwa akifanya kama meneja wa ‘Spa’ na kuanzisha kampuni yake ya utalii nchini Zanzibar, mnamo 2015.

Wazo la kuianzisha kampuni yake ya Maridadi Tours lilimjia akilini baada ya kutalii mno maeneo tofauti.

Baada ya kutalii, alikuwa akipakia picha za safari hizo mitandaoni, na wengi wakaanza kupendezwa mno, na kuanza kuulizia kuhusu jinsi ambavyo wangepata huduma kama hizo.

Sasha akawa anawaelekeza kwa kampuni za kutoa huduma za utalii. Hata hivyo, changamoto zozote zilipotokea, watu walikuwa wakimjia maadamu yeye ndiye aliyekuwa akiwaelekeza.

“Niligundua kuwa huo ulikuwa uharibifu wa muda kwa wateja na wenyeji wangu, ndiposa nikaamua kuanzisha kampuni yangu ya utalii,” asema.

“Kwa kuwa nilikuwa nchini Tanzania, nikashirikiana na wanawake wawili, kuambatana na kanuni za nchi hiyo, ambapo kama wewe si mwenyeji, ni lazima ushirikiane na mwenyeji. Ushirikiano huo uliisha na ikabidi nianze upya peke yangu,” aeleza Sasha.

Anaongeza kuwa, kampuni hiyo ina afisi nchini Kenya, ambapo inashirikiana na kampuni nyingine kutoa huduma za utalii.

Kwa sasa, Sasha huuza huduma za utalii nchini za Kenya, Uganda, Rwanda, Tanzania, Zambia, Botswana, Zimbabwe, Namibia, Afrika Kusini na Ghana.

“Nimejifunza kwamba, unapoendesha biashara na watu katika nchi tofauti, unafaa kuwachagua kwa hekima; iwapo utashirikiana na watu wasiofaa, kuwa tayari kupitia majaribu, jinsi nilivyopitia mwanzoni,” aonya Sasha, akiongeza kuwa, alipoanza kuwapata wateja kwa wingi, washirika wake wakaanza kumgeuka.

Anasema kuwa, wateja wake wengi ni Waafrika kutoka ughaibuni, ambao wanataka kujifunza mengi kuhusu Afrika.

Miongoni mwa hoteli ambazo yeye huwapeleka wateja wake ni pamoja na; Mt. Meru mjini Arusha, DoubleTree, inayosimamiwa na Hilton, Zanzibar.

Elephant Valley nchini Botswana, Kingdom Hotel na Victoria Falls chini Zimbabwe, ni kati ya vivutio vinavyopendwa na watalii. Isitoshe, Kendwa Rocks ni mojawapo ya hoteli anazowapeleka wateja wake.

“Nchini Kenya, mimi huchagua hoteli za Serena na Sarova kwa sababu huduma zao ni za kiwango cha juu,” asema, akiongeza kuwa, ni nadra mno kupata malalamiko kutoka kwa wateja.

Anaongeza kuwa, mbali na kuuza huduma za utalii aina ya safari, kuna utalii ambapo watalii hutembezwa kujionea utamaduni wa Afrika.

“Utalii wa utamaduni si kuhusu Wamasai pekee, nchini Tanzania, kuna watu wa Hadzabe, wanaoishi msituni na kulia msituni.”

Sasha anasema kuwa, amekuwa akitumia mitandao ya kijamii kutangaza biashara yake ya utalii. Pia, amekuwa katika makundi mengi ya Facebook.

“Wanderlust (Dkt Amakove Wala), ni jukwaa jingine ambalo Wakenya hutumia kuwatuma wateja kwangu. Jacqueline Gu ni Mkenya mwingine ambaye ninamshukuru; amekuwa akitangaza kampuni yangu kule Dubai anakofanya kazi,” asema Sasha.

Sasha Seraphine Mbote, mmiliki wa Maridadi Tours akiogelea na baadhi ya wateja. PICHA | PETER CHANGTOEK

Changamoto moja ambayo amewahi kupitia ni ugonjwa wa Covid-19, ulioathiri biashara nyingi.

Awali, alikuwa na wafanyakazi 20, lakini akasalia na 5.

“Kwa wateja wetu wanaotumia huduma zetu, Maridadi Tours, tuna zawadi – tuna shuka za Wamasai, zilizotengenezwa vizuri na dadangu, Sheila Mbote,” afichua.

  • Tags

You can share this post!

MITAMBO: Hiki hapa kipima ubora wa kahawa

Mateso ya polisi aliyepata upofu akiwa kazini

T L