• Nairobi
  • Last Updated September 28th, 2023 10:25 PM
UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Sifa bainifu za lugha kama kiambajengo muhimu cha mawasiliano

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Sifa bainifu za lugha kama kiambajengo muhimu cha mawasiliano

Na MARY WANGARI

JINSI tulivyokwisha eleza, lugha ni kiungo muhimu kinachotumiwa na binadamu katika karibu shughuli zao zote za kimaisha.

Bila shaka nafasi ya lugha kama nyenzo kuu ya mawasiliano kwa binadamu haiwezi ikasisitizwa vya kutosha.

Lugha ni mfumo – Mfumo wa lugha una maana kwamba lugha inahusisha vipashio muhimu anuai.

Vipashio au viambajengo vya lugha ni kama vile neno, sauti, na sentensi.

Vinaposhirikishwa pamoja, vipashio huunda tungo ambazo ni sharti ziwe na maana ili kuwasilisha ujumbe katika lugha husika na kuwezesha mawasiliano.

Iwapo tungo hazina maana, basi haziwezi kuwa lugha wala kupitisha maana yoyote inayoeleweka hivyo basi mawasiliano hayawezi kutokea.

Sifa bainifu za lugha

Lugha inasheheni sifa fulani za kimsingi ambazo zinapatikana katika lugha zote jinsi tutakavyoziorodhesha ifuatavyo:

Lugha hubadilika – Lugha yoyote ile hupitia mchakato wa mabadiliko kutoka na mpito wa wakati, mazingira, maendeleo katika nyanja ya teknolojia, habari na mawasiliano.

Mabadiliko katika lugha huweza kujitokeza kwa njia zifuatazo:

Kifonolojia – Mabadiliko kifonolojia yanahusisha kubadilika kwa kanuni na mfumo wa matamshi katika lugha husika.

Aghalabu, mabadiliko hayo hutokana mtindo wa lugha kukopa misamiati iliyo na sauti zisizopatikana katika lugha asilia ikiwemo mabadiliko mengineyo.

Kimofolojia – Mabadiliko kimofolojia hutokea wakati utaratibu wa lugha kimaumbo unapobadilika hasa kuhusiana na kanuni za uundaji wa maneno.

Kimantiki na kileksia – Mabadiliko haya hujitokeza katika maana au leksimu ya lugha husika.

Kuongezeka kwa leksimu hutokana na mbinu au njia zote za uundaji wa maneno.

Leksimu inapoongezeka maana huongezeka vilevile kwa sababu huambatana na dhana inayowakilishwa.

Kisintaksia – Mabadiliko ya lugha kisintaksia husababisha utaratibu wa lugha ulio tofauti na ule wa awali.

Lugha huweza kuathiri na kuathiriwa – Ni muhimu kufahamu kwamba lugha yoyote ile inaweza ikaathiri utaratibu wa lugha nyingine katika kiwango fulani au viwango vyote vya lugha.

Aidha, lugha hupitia mfumo wa kuishi sawia na binadamu jinsi inavyoashiriwa hapa:

Lugha huzaliwa – Huu ni wakati ule lugha inapochipuka kwa mara ya kwanza.

Lugha hukua – Lugha hukua kuambatana na maendeleo na mabadiliko mbalimbali katika mazingira yake.

Lugha inaweza kufa – Huu ni wakati ambapo lugha hudidimia na kukoma kutimiza dhima yake miongoni mwa wanajamii.

[email protected]

You can share this post!

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Fasili ya lugha kama nyenzo ya...

COVID-19: Kocha Jurgen Klopp akosa kusafiri Ujerumani...