• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
USHAURI NASAHA: Yazue mabadiliko chanya masomoni mwako wakati huu

USHAURI NASAHA: Yazue mabadiliko chanya masomoni mwako wakati huu

NA HENRY MOKUA

KUANZA ni muhimu.

Hata unapoona hujajiandaa vilivyo, anza.

Nakisia una mambo mawili matatu ya kukusababisha uchelee kuanza lakini anza tu; angaa hivi hivi. Waweza kufikiri ndiwe tu una ugumu wa kuanza lakini ningependa ufahamu kwamba kila unayemhusudu alianza vivyo hivyo, kwa hivyo nawe anza.

Ewe mwanafunzi unayewazia kuubadili mkondo wako wa masomo na kuufikilia uwezo wako halisi, jikaze ukate pingu za udhalili.

Ni kawaida kujihisi mnyonge wakati ukitaka kuuchukua mkondo huu lakini mambo yatatengenea pale utakapoanza kubuni mikakati ya kuzua mabadiliko na kuifuatilia.

Njia moja hakika ya kuzikata pingu za unyonge ni kuungana na mwanafunzi mwenzio ambaye anajiamini, amepiga hatua mbele na yupo tayari kukusaidia.

Ikiwa utaridhishwa na nidhamu yake, maono yake, bidii yake na mikakati yake, sema naye na kumwomba kukushika mkono ili nawe ufikilie pa kujiamini. Kumbuka huwezi kuifikia hatua hii ikiwa hutaichukua hatua ya awali na kuanza kujikomboa.

Huenda unachelea kufeli. Labda umeshakimbia pale mbele ukaona utakavyofeli utakavyochekwa na kusimangwa.

Tulia… kufeli hakutokei ghafla hivyo! Waweza kukuonea mbali na kukwepa. Kwani hata ukafeli utakuwa wa kwanza?

Hujawaona wengi waliofeli lakini wakainuka na kukimbia kwa kasi wasiweze kufikiliwa tena!

Nisikilize kwa makini ewe mwanafunzi wangu: waweza kuanza kuutekeleza mkakati wako usifeli. Ikiwa utafeli, muradi umeyafanya yote kadri ya uwezo wako, huna sababu ya kujilaumu.

Vema zaidi, upo uwezekano mkubwa kwamba hata mkakati wako ukikosa kufaulu kwa kiasi ulichokiwazia, bado una nafasi nyingine ya kuyanyoosha mambo; muhimu ni uanze kwanza!

Ikiwa unakosa hamasa au kichocheo cha kuanza, wahitaji kuuwazia mustakabali wako kwa makini kuanzia sasa. Je ungependa kuishi maisha na namna gani katika siku za halafu? Ikiwa ungependa kuishi maisha ya kutamanika na uwe mtu wa kutegemewa, anza kwa namna fulani kuiwania ndoto hii.

Anza kuyawazia mabadiliko maishani mwako na kuibuka na mikakati mwafaka ya kuyafikilia.

Je ungependa kuishi kwenye jumba kubwa na la kupendeza? Anza kuliwekea msingi thabiti tokea sasa hivi. Ungependa uwe na kaya (compound) kubwa na yenye bustani ya kupendeza? Anza kuutafuta leo uwezo wa kuifanikisha ndoto hii.

  • Tags

You can share this post!

Kura: Baadhi ya kampuni Industrial Area zaruhusu...

KAULI YA MATUNDURA: Uandishi ndio njia aula zaidi ya kuacha...

T L