• Nairobi
  • Last Updated May 22nd, 2024 6:07 PM
Utalii Lamu unavyoyumbishwa na mfumko wa bei ya mafuta ya petroli

Utalii Lamu unavyoyumbishwa na mfumko wa bei ya mafuta ya petroli

NA KALUME KAZUNGU

WATALII na wageni wanaozuru Pwani ya Kenya, hasa Lamu tayari wameanza kuhisi ugumu wa gharama ya juu ya maisha unaochochewa na ongezeko la bei ya mafuta.

Hii ni kufuatia kuongezeka kwa bei ya mapochopocho, hasa yale ya samaki hotelini na mikahawani eneo hilo.

Kwa kawaida, bakuli la mlo wa samaki kwenye hoteli za kifahari zipatikanazo Lamu huuzwa kati ya Sh3,000 na Sh3,500.

Katika hoteli na mikahawa ya kawaida, sinia ya mlo wa samaki huuzwa kienyeji kwa kati ya Sh700 na Sh1500.

Uchunguzi uliofanywa na Taifa Leo Dijitali mwishoni mwa juma ulibaini kuwa tangu nyongeza ya mafuta kutangazwa na serikali wiki jana, wenye hoteli na mikahawa kisiwani Lamu na viungani mwake wamelazimika kuongeza bei ya vyakula, hasa vile vya baharini kutokana na kwamba wamiliki hao wa hoteli wamekuwa wakinunua bidhaa ya samaki kutoka kwa wavuvi kwa bei ghali.

Mwenyekiti wa Bodi ya Utalii Lamu (LTA), Ghalib Alwy, anasema walikuwa wakinunua kilo ya samaki wa kawaida kwa kati ya Sh200 na Sh500 pekee ilhali kilo ya samaki maalum kama vile kambakoche ikiuzwa kwa kati ya Sh800 na Sh1,200.

Tangu bei mpya ya mafuta kutangazwa aidha, samaki wamekuwa wakinunuliwa kwa bei ghali na wenye mahoteli, wavuvi wakidai kulazimika kuongeza bei kutokana na mfumko wa bei ya mafuta unaoathiri matumizi ya mashua na boti wanazotumia kuvulia samaki baharini.

Bw Alwy alieleza hofu kwamba huenda kukashuhudiwa uhaba wa samaki hotelini na mikahawani Lamu ikiwa bei ya mafuta haitapunguzwa.

Bw Alwy, ambaye pia ni mmiliki wa hoteli ya kifahari ya Bush Gardens Seafront Hotel and Restaurant kisiwani Lamu, alisema baadhi ya wanabiashara wa hoteli tayari wameanza kukwepa kuuza mlo wa samaki kutokana na ughali wa kununua na kutayarisha bidhaa hiyo kutoka kwa wavuvi.

“Samaki wamekuwa ghali kiasi kwamba hata ukaongeza bei kwa mteja baada ya kuandaa mlo huo hotelini pia utaambulia patupu. Wavuvi wanatuuzia samaki bei ghali na hatuwalaumu kwani bei ya juu ya mafuta imezidisha gharama kwa kila sekta,” akasema Bw Alwy.

Wavuvi kisiwani Lamu wakiwasili kutoka baharini. PICHA|KALUME KAZUNGU

Kufikia juma hili, bakuli la kitoweo cha samaki kwenye hoteli za kifahari kisiwani Lamu, Shella na viungani mwake tayari lilikuwa likiuzwa kwa kati ya Sh3,700 na Sh4,000 hali ambayo wateja, hasa watalii walikiri kufinywa kimfuko.

Kwenye hoteli za kawaida, bei ya kienyeji ya kitoweo cha samaki ilikuwa kati ya Sh1,000 na Sh1,700, hali ambayo wateja waliilalamikia.

Fridah Njeri ambaye ni mmiliki wa Lamu Floating Bar and Restaurant, alikiri kuwa wengi wa wamiliki wa hoteli, mikahawa na maeneo mengine ya kujivinjari wanakabiliwa na kipindi kigumu cha kuendesha biashara zao kutokana na kupanda kwa gharama ya maisha kila wakati.

Bi Njeri alisema ikiwa hali ya uchumi haitadhibitiwa, huenda baadhi yao wakaanza kuwapunguza au hata kuwafuta kazi wafanyakazi hotelini kutokana na ugumu uliopo wa maisha.

Aliiomba serikali kumzingatia mwananchi wa kawaida katika kila maamuzi yanayoafikiwa.

“Ushuru umekuwa mwingi. Gharama ya maisha nayo inapanda kila kukicha. Kuongezwa kwa bei ya mafuta kumeharibu kila kitu sasa. Kilichobakia kwetu ni kuwarudisha nyumbani wafanyakazi na kufunga hoteli zetu. Hali ni ngumu. Samaki hawanunuliki. Tunaumia,” akasema Bi Njeri.

Baadhi ya wavuvi waliozungumza na Taifa Leo Dijitali walisema wamelazimika kusitisha shughuli baharini na kuegesha vyombo vyao, ikiwemo mashua, jahazi na boti za uvuvi maskani kwani hawawezi kukimu gharama ya juu ya mafuta kusafiri baharini kuvua.

Safari moja ya kwenda bahari ya kina kirefu kuvua humgharimu mvuvi wa Lamu kati ya lita 60 na lita 100 za mafuta ya petroli ya kuwekwa chomboni ili kusafiria kunakohitajika kuvua na kurudi mjini.

Ongezeko la bei ya mafuta ya petroli limeshinikiza wavuvi kuegesha mashua na boti zao. PICHA|KALUME KAZUNGU

Mwenyekiti wa Muungano wa Wavuvi wa Kisiwa cha Lamu (BMU), Abubakar Twalib alisema awali walikuwa wakinunua mtungi mmoja wa lita 20 kwa Sh4,400 lakini tangu bei mpya ya mafuta kutangazwa, wamekuwa wakiuziwa mtungi mmoja wa lita 20 kwa Sh4,800.

Bw Twalib anasema hali hiyo ni ngumu kwa wavuvi wa Lamu ambao wengi wao ni maskini.

“Ukitazama hapa utapata mashua, jahazi na boti nyingi za uvuvi zikiwa zimepakishwa bila kazi. Wavuvi hawawezi tena kukimu gharama ya juu ya petroli. Kwenda baharini tuligharimika Sh13,200 hadi Sh22,000. Leo safari hiyo hiyo lazima uwe na Sh14,400 na Sh24,000 za kugharimia petroli ya kutumika kwenye mashua. Wenye hoteli wasitulaumu kuwauzia samaki bei ghali kwani sisi pia tunaumia,” akasema Bw Twalib.

Bunu Vae, mmoja wa wavuvi tajika kisiwani Lamu, anasema yeye binafsi amelazimika kusitisha uvuvi na kugeukia biashara nyingine baada ya kushindwa kustahimili ughali wa mafuta ya kusafiria baharini kuvua.

“Nimegeukia biashara ya usafirishaji mizigo kwa kutumia punda ili kujipatia kipato. Uvuvi umeshindikana kutokana na bei ghali ya mafuta. Kuna wenzetu wengine ambao kwa sasa wamegeukia biashara ya kuvunja mawe na kuchonga matofali kukimu familia zao. Serikali ishukishe hiyo bei ya mafuta la sivyo sekta kama uvuvi, hoteli na uchukuzi zitasambaratika. Hali ni ngumu,” akasema Bw Vae.

Baadhi ya familia za Lamu zilizohojiwa na Taifa Leo Dijitali zilikiri kubadili mlo wao wa kila siku, ambapo wengi hukwepa kitoweo cha samaki ambacho ni ghali.

“Ninaishi mkabala na Bahari Hindi lakini nimeshindwa kukimu bei ya juu ya samaki. Samaki ninawaona tu kwa macho. Familia yangu sasa imegeukia ulaji wa mboga kwa wingi badala ya samaki. Inabidi tuzoee kukosa samaki mezani,” akasema Bi Fatma Aboud.

Lamu ni kaunti ambayo uvuvi na utalii ni uti wa mgongo kwa uchumi wake.

 

  • Tags

You can share this post!

Mudavadi ahofia majanga zaidi yatazuka bara Afrika

Wavuvi wauana kwa sababu ya sigara ya Sh15

T L