• Nairobi
  • Last Updated February 29th, 2024 6:55 PM
Viambajengo muhimu katika lugha kama chombo cha mawasiliano

Viambajengo muhimu katika lugha kama chombo cha mawasiliano

Na MARY WANGARI

Lugha huundwa kwa sauti ambazo huunganishwa ili kuunda neno au sehemu ya neno, kisha maneno huungana kuunda miundo mikubwa zaidi yenye maana kama vile virai, vishazi, sentensi na aya.

Kwa mfano: Mkulima (N) + Anavuna(T) = Mkulima anavuna

Hata hivyo, muungano huu wa maneno huwa haufanyiki shaghala baghala maadamu kuna kanuni na sheria zinazodhibiti mfuatano wa kila kipashio.

Katika kila lugha, kuna kanuni maalum zinazodhibiti ama mfuatano wa sauti, mafimu, maneno au hata sentensi.

Kwa mintarafu hii, ndiposa tunahoji kuwa lugha ya binadamu ni mfumo wenye kanuni, sheria na taratibu mahsusi ambazo endapo zitakiukwa, hakutakuwa na utimilifu wa lugha husika.

Wanajamii au ukipenda watumiaji wa lugha fulani huweza kuelewana kupitia kanuni hizo maalum zinazodhibiti mpangilio wa viunzi vya lugha husika.

Lugha ni mfumo wa sauti nasibu – Kiambajengo hiki kina maana kwamba hakuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya neno na kitu chenyewe kinachotumika katika ujenzi na matumizi mengine (maana na kirejelewa).

Inamaanisha vilevile kuwa ishara na maumbo ya kiisimu hayana uhusiano wowote au mfanano wowote na maana ambazo tunayapatia.

Kwa mfano, neno ‘jiwe’ hakuna watu waliokaa na kusema kuanzia leo hili litaitwa jiwe.

Aidha, hakuna uhusiano wowote kati ya neno “jiwe” na umbo linalorejelewa, ila uhusiano wake ni wa nasibu tu na hutofautiana kutoka na lugha moja hadi nyingine.

Lugha ni maalumu kwa mwanadamu – Lugha ni chombo cha mawasiliano kinachotumika miongoni mwa binadamu pekee ambapo hakuna kiumbe mwingine ambaye si binadamu mwenye uwezo wa kutumia lugha wala kuzungumza.

Kwa kuzingatia hoja hii, ni bayana kuwa kuna sifa maalum za lugha ya binadamu ambazo hazipatikani kwa kiumbe mwingine yeyote yule isipokuwa mwanadamu.

Tofauti kati ya lugha ya binadamu na viumbe wasio binadamu

Japo viumbe wasio binadamu mathalan wanyama na nyuni wanaweza kuwasiliana, mawasiliano yao huwa ni ya sauti au ishara ambazo kimsingi si lugha.

Aidha, mawasiliano haya hudhibitiwa na hisia kama vile uchungu, hofu, njaa,hamu au ishara za kutoa taarifa fulani.

Isitoshe, binadamu ana uwezo wa kujifunza lugha mbalimbali na kuitumia katika mazingira yake jambo ambalo wanyama, nyuni na viumbe wengine hawawezi.

Kwa mfano, ukimchukua mbwa wa Japan na kumleta Kenya atabweka kwa njia ile ile ya mbwa wa Kenya kueleza shida au ishara husika.

[email protected]

You can share this post!

Lugha kama chombo cha mawasiliano baina ya binadamu

Adhabu ya kadi nyekundu dhidi ya David Luiz wa Arsenal...