• Nairobi
  • Last Updated April 15th, 2024 2:15 PM
WALIOBOBEA: Ndwiga, waziri mtulivu aliyechapa kazi vyema

WALIOBOBEA: Ndwiga, waziri mtulivu aliyechapa kazi vyema

KWA HISANI YA KENYA YEAR BOOK

PETER Njeru Ndwiga, waziri wa Ustawi wa Vyama vya Ushirika katika Baraza la Mawaziri la Kwanza la Mwai Kibaki alikuwa mmoja wa mawaziri waaminifu zaidi na asiyependa mizozo.

Mbunge huyo wa eneobunge la Manyatta, pia alikuwa waziri wa pekee wakati huo kutoka wilaya za Embu na Mbeere.

Ushirikiano wa kisiasa kati ya Kibaki na Ndwiga ulifikia kilele katika uteuzi wake katika Baraza la Mawaziri ulianza mwaka wa 1991, katika siku za mwanzo za chama cha Democratic Party (DP), ambacho Kibaki aliunda na kuongoza.

Ndwiga alikuwa amejitolea kumuunga Kibaki na alifanya bidii kuhakikisha maeneo bunge manne katika eneo hilo – Siakago na Gachoka katika Mbeere na Manyatta na Runyenjes katika wilaya ya Embu – yalimuunga Kibaki alipogombea urais mwaka wa 1992.

Ndwiga alikuwa mmoja wa wabunge walioingia Bunge kwa tikiti ya DP mwaka huo baada ya kuchaguliwa mbunge wa eneobunge la Runyenjes.

Alihifadhi kiti hicho katika uchaguzi mkuu wa 1997 kupitia tikiti ya chama hicho.

Wakati DP iliungana na vyama vingine vya upinzani kuunda muungano wa National Rainbow Coalition (NARC) kwa maandalizi ya uchaguzi mkuu wa 2002, Ndwiga aliandamana na Kibaki.

Ni baada ya kushinda kiti hicho kwa kura nyingi kwa tikiti ya NARC, kwamba Kibaki alimteua katika Baraza la Mawaziri.

Miongoni mwa aliyoafikia akiwa waziri wa ustawi wa vyama vya ushirika ni kufanya kahawa kutoka Kenya kuorodheshwa kama mojawapo ya bidhaa zinazouzwa Amerika.

Ndwiga atakumbukwa kwa juhudi zake za kutekeleza Sheria ya Vyama vya Ushirika na kufanikisha uunganishaji wa vyama vya ushirika.

Mwaka wa 2007, Ndwiga aligombea kiti cha ubunge cha Manyatta akiwa kifua mbele kwa kuwa alikuwa amekikalia. Wakati huo alikuwa amekikalia kwa miaka 15.

Lakini katika uchaguzi huo alishindwa na mfanyabiashara Emilio Kathuri. Kushindwa kwake kulimfanya aondoke katika Baraza la Mawaziri la Kibaki na wizara ya vyama vya ushirika ikakabidhiwa Joseph Nyagah mwaka wa 2008 katika serikali ya muungano ambayo Kibaki alikuwa rais na Raila Odinga akiwa waziri mkuu.

Mwaka wa 2008 alipoulizwa kuhusu Kibaki akihojiwa na gazeti moja la humi nchini, Ndwiga alimtaja rais kama kiongozi anayefanya maamuzi huru.

Kulingana naye, Kibaki hakukubali watu wa kusengenya wengine. Badala yake, alitafuta ushauri mara kwa mara kutoka kwa watu aliohisi walistahili kwa wakati na mazingira fulani.

Ndwiga alizaliwa Januari 4, 1954 katika Manyatta, Embu na kusomea shule ya msingi ya Kibugu kabla ya kujiunga na Kamama na kisha Siakago High School. Alisomea diploma katika masuala ya usimamizi wa biashara katika Chuo Kikuu cha Cooperative University.

Mwaka wa 2014, Rais Uhuru Kenyatta alimteua kuwa mwenyekiti wa Bodi ya Tanathi Water Services Board na mwaka wa 2017, Ndwiga alirudi Bungeni alipochakuliwa seneta wa kaunti ya Embu.

  • Tags

You can share this post!

Uswahilini sihami, niende wapi na ndo nimeshafika!

MIKIMBIO YA SIASA: Itabidi watorokao Azimio ‘wajipange’

T L